Tafuta

Baba Mtakatifu Francisko amemteua Mheshimiwa Padre Simon Chibuga Masondole kuwa Askofu mpya wa Jimbo Katoliki la Bunda, nchini Tanzania. Baba Mtakatifu Francisko amemteua Mheshimiwa Padre Simon Chibuga Masondole kuwa Askofu mpya wa Jimbo Katoliki la Bunda, nchini Tanzania. 

Askofu Simon Chibuga Masondole Jimbo Katoliki la Bunda, Tanzania

Askofu mteule Simon Chibuga Masondole wa Jimbo Katoliki Bunda, alizaliwa tarehe 2 Oktoba 1972 huko Bukiko, Kisiwani Ukerewe. Tarehe 2 Julai 2006 alipewa Daraja Takatifu ya Upadre. Baadaye ajiendeleza katika masomo na Liturujia ya Kanisa Jimboni Padu na hatimaye Chuo Kikuu cha Kipapa cha Mtakatifu Anselmi na kujipatia Shahada ya uzamivu. Mwaka 2018 akarejea Jimboni Bunda.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.  – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko amemteua Mheshimiwa sana Padre Simon Chibuga Masondole wa Jimbo Katoliki la Bunda, kuwa Askofu mpya wa Jimbo Katoliki la Bunda, Tanzania, kuchukua nafasi iliyoachwa na Askofu mkuu Renatus Leonard Nkwande wa Jimbo kuu la Mwanza. Hadi kuteuliwa kwake, Askofu mteule Simon Chibuga Masondole alikuwa ni msimamizi wa Parokia, Mwenyekiti wa Umoja wa Mapadre Jimbo Katoliki la Bunda na Mkurugenzi mtendaji wa Shule ya Msingi na ya Awali ya Mtakatifu Francisko wa Assisi, Jimbo Katoliki Bunda. Askofu mteule Simon Chibuga Masondole wa Jimbo Katoliki Bunda, alizaliwa tarehe 2 Oktoba 1972 huko Bukiko, Kisiwani Ukerewe.

Kunako Mwaka 1998 alijiunga na Seminari Kuu ya Kibosho, Jimbo Katoliki la Moshi, kwa ajili ya masomo ya Falsafa na kuhitimu masomo yake mwaka 2001. Baadaye mwaka 2001 aliendelea na masomo ya Taalimungu Seminari kuu ya Segerea, iliyoko Jimbo kuu la Dar es Salaam na kuhitimu mwaka 2006. Baada ya masomo na majiundo yake ya kikasisi, tarehe 2 Julai 2006 akapewa Daraja Takatifu ya Upadre kwa ajili ya Jimbo kuu la Mwanza. Tangu wakati huo kama Padre, amewahi kuwa Paroko-usu Parokia ya Kahangara, Jimbo kuu la Mwanza, Mkurugenzi Msaidizi wa Kamati ya Liturujia Jimbo kuu la Mwanza na baadaye kati ya Mwaka 2006 hadi mwaka 2008 aliteuliwa kuwa Paroko-usu kwenye Parokia ya Nansio-Ukerewe, Jimbo Katoliki la Bunda.

Baadaye kunako mwaka 2008 alitumwa na Jimbo Katoliki la Bunda kujiendeleza zaidi katika masomo la Liturujia ya Kanisa kwenye Taasisi ya Shughuli za Kichungaji Kiliturujia ya “Santa Giustina”, Jimbo Katoliki la Padua, nchini Italia. Baadaye alijiendeleza zaidi kwenye Taasisi ya Kipapa ya Liturujia, Chuo Kikuu cha Mtakatifu Anselmi kilichoko mjini Roma ambako alijipatia Shahada ya Uzamivu katika Liturujia ya Kanisa kunako mwaka 2016. Kati ya mwaka 2015 hadi mwaka 2018 alitoa huduma ya kichungaji Jimboni Tortona, Italia. Na kunako mwaka 2018 alirejea tena kwa shughuli za kichungaji, Jimbo Katoliki la Bunda, hadi kuteuliwa kwake kuwa Askofu mpya wa Jimbo Katoliki la Bunda amekuwa akifundisha Liturujia ya Kanisa na mlezi, Seminari kuu ya Segerea. Baada ya tangazo la uteuzi huu, Segerea kuliwaka moto wa nderemo! Askofu mteule akabebwa juu kwa juu, utadhani Mbayuwayu! Tunda la Kanisa, ni wimbo uliosikika kwenye viunga vya Segerea, tarehe 6 Aprili 2021. 

Jimbo Katoliki Bunda

 

06 April 2021, 12:00