Simameni Kidete Kutangaza Injili Ya Uhai Dhidi ya Utamaduni wa Kifo!
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. –Vatican.
Baba Mtakatifu Francisko hivi karibuni alizungumza na wajumbe wa Mkutano mkuu wa Chama cha Madaktari wa Saratani Nchini Italia “AIOM, yaani “Associazione Italiana di Oncologia Medica” kilichoanzishwa kunako mwaka 1973. Aliwaambia kwamba, mgonjwa anapaswa kuheshimiwa na kuthaminiwa hasa kutokana na ukali wa mateso anayokabiliana nayo. Kila huduma ya matibabu inayotolewa kwa mgonjwa iwe ni chemchemi ya huruma na upendo kwa wagonjwa wanaoteseka. Maendeleo ya sayansi na teknolojia ya tiba ya afya ya mwanadamu yanapaswa kuwa kweli ni chombo cha huduma kwa wagonjwa na wala si vinginevyo. Kamwe mgonjwa asionekane kuwa ni mzigo mzito, kiasi cha kuanza kuhalalisha kisheria mchakato wa kifolaini. Kwa haraka haraka anasema Baba Mtakatifu, jambo hili linaweza kuonekana kuwa kama sehemu ya uhuru wa mtu binafsi; lakini ndani mwake, uhuru huu unafumbata ubinafsi unao thubutu kupima: haki, heshima na utu wa mtu kutokana na umuhimu wake. Kifolaini hakimsaidii mtu kupunguzia maumivu.
Askofu mkuu Vincenzo Paglia tarehe 15 Agosti 2016 aliteuliwa na Papa Francisko kuwa Mkuu wa Taasisi ya Kipapa ya Maisha. Na ilipogota tarehe 8 Oktoba 2016 Baba Mtakatifu akapitisha kanuni mpya za uendeshaji wa taasisi ya Kipapa kwa ajili ya Maisha. Lengo la taasisi hii ni kusimama kidete kulinda na kutetea thamani ya maisha na utu wa binadamu mintarafu Mafundisho Jamii ya Kanisa. Taasisi hii itakuwa na dhamana ya kutafiti, kuunda utamaduni wa maisha dhidi ya utamaduni wa kifo na kuhabarisha wadau mbalimbali changamoto zinazojitokeza katika mchakato wa kulinda na kudumisha Injili ya uhai duniani! Taasisi hii ina dhamana na wajibu wa kufanya tafiti za kitaaluma na kisayansi, ili kusaidia kusimama kidete kulinda na kutetea na kudumisha maisha ya binadamu. Itakuwa na kazi ya kusaidia kuwafunda waamini na watu wote wenye mapenzi mema katika utamaduni wa maisha mintarafu Mafundisho Jamii ya Kanisa.
Taasisi ya Kipapa ya Maisha, inawajibika kusimama kidete: kulinda, kutetea na kudumisha uhai wa binadamu, utu na heshima yake, tangu pale mtoto anapotungwa mimba tumboni mwa mama yake hadi mauti ya kawaida inapomfika kadiri ya mpango wa Mungu pamoja na kudumisha heshima kati ya vizazi. Ni wajibu wa taasisi hii kusaidia mchakato wa maboresho ya maisha ya binadamu; kwa kuendeleza tunu msingi za maisha: kiroho na kimwili, ili kudumisha Ikolojia ya binadamu kwa kumpatia mwanadamu nafasi yake katika kazi ya Uumbaji. Askofu mkuu Vincenzo Paglia anasema, katika kipindi cha miaka mitano iliyopita Injili ya uhai imekuwa ikitishiwa na utamaduni wa kifo unaofumbatwa katika dhana ya kifolaini na mitazamo hasi ya tunu msingi za maisha ya ndoa na familia. Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19 umekuwa na athari kubwa katika maisha ya ndoa na familia katika ujumla wake. Changamoto mamboleo na tunu msingi za maisha ya ndoa na familia ni mambo yanayopaswa kuvaliwa njuga katika sera na mikakati ya shughuli za kichungaji!
Baba Mtakatifu Francisko anasema ni dhamana na wajibu wa madaktari kuhakikisha kwamba, wanawasaidia wagonjwa kupata nafuu katika mahangaiko yao; kwa kujenga na kudumisha utamaduni unaothamini utu, heshima na haki msingi za binadamu; chemchemi ya matumaini katika maisha ya mwanadamu! Madaktari wawe ni mashuhuda na vyombo vya matumaini kwa wagonjwa waliokata tamaa; kwa kusaidia kuzuia magonjwa; kwa kufanya uchunguzi wa kina pamoja na kuwaheshimu wagonjwa wenyewe kwani wameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Katika kipindi cha miaka ya hivi karibuni dhana ya kifolaini inazidi kushika kasi ndani na nje ya Italia. Kuna watu ambao wanadhani kwamba, maisha ya jirani zao ni “mzigo mzito” usiovumilika wala kubebeka. Kwa wale ambao wamezaliwa na vilema mwilini hawana nafasi katika ualimwengu wa sasa. Kwa mtoto mwenye kasoro anahukumiwa kunyongwa hata kabla ya kuzaliwa. Hii ni sumu kali sana dhidi ya Injili ya uhai duniani. Mama Kanisa anapenda kuwakumbusha waamini na watu wote wenye mapenzi mema kwamba: udhaifu na magonjwa ni sehemu ya maisha ya mwanadamu kama anavyokaza kusema, Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wa Kitume "Fratelli tutti": Yaani “Wote ni Ndugu”: Kuhusu Udugu na Urafiki wa Kijamii”
Italia katika miaka ya hivi karibuni anasema Baba Mtakatifu Francisko imejikuta ikiwa na idadi ndogo sana ya watoto wanaozaliwa na matokeo yake, idadi ya wazee nchini Italia inazidi kuongezeka maradufu. Idadi ya watoto waliozaliwa kwa Mwaka 2020 imekuwa ni chini sana ikilinganishwa na miaka mingine. Hii si kwa sababu ya janga la Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19, peke yake, bali ni ukame ambao umeanza kuonesha makali yake katika maisha ya watu. Baba Mtakatifu anawaalika watu wa Mungu nchini Italia kuwekeza katika watoto, kwani watoto ni kumbukumbu inayoielekeza jamii kwa leo na kesho iliyo bora zaidi. Misigano inayotokea maeneo ya kazi, majumbani na shule kwa upande wa watoto, wanaookoa jahazi ni babu na bibi! Kumbe, kuna haja ya kuwekeza katika familia, kwa kuhakikisha kwamba, vijana wanapata fursa za ajira, ili waweze kuanzisha na kuzitegemeza familia zao. Umefika wakati wa kuondokana na vitendo vinavyowatweza wanawake wenye mimba katika ulimwengu wa wafanyakazi.
Watoto ni amana na utajiri wa jamii, kumbe, familia zinapaswa kuwezeshwa kiuchumi. Familia inapaswa kupewa kipaumbele cha kwanza kwa sasa na kwa siku za usoni, ili kufufua hali ya Italia katika sekta mbalimbali za maisha. Baba Mtakatifu anasema, maisha ni zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu inayopaswa kupokelewa kwa moyo wa shukrani na hivyo kuijengea mazingira ya kuweza kuwarithisha wengine. Wazazi wanapaswa kuwa na subira ya kupata mtoto na kumpenda kadiri ya uwezo wao! Idadi ndogo ya watoto wanaozaliwa ni dalili za uchoyo na ubinafsi na matokeo yake, ni idadi ya wazee kuongezeka maradufu. Watu wajenge utamaduni wa kuthamini maisha zaidi na wala si vitu! Watoto ni amana na utajiri wa jamii, kumbe, kuna haja ya kuwa na ujasiri wa kuchagua Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo. Maisha ni zawadi ya kwanza kabisa kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Kuna haja ya kujenga mafungamano endelevu kati ya vizazi, kwa kuwajengea vijana imani na matumaini ya leo na kesho iliyo bora zaidi, kwa kubadili hali na mtazamo kuhusu tunu msingi za maisha ya ndoa na familia!
Akili Bandia “Artificial Intelligence tayari imeanza kutumika kuboresha huduma za afya hasa katika maeneo yenye uhaba wa madaktari. Na Baraza la Kipapa la Maisha limeanzisha Mfuko wa Akili Bandia na kwamba, tema ya mkutano mkuu wa Baraza la Kipapa la Maisha inayofanyiwa kazi kwa sasa ni “Kanuni Maadili ya Kiulimwengu” “Global ethical”. Lengo ni kuwawezesha wataalam kutumia Akili Bandia kwa kuzingatia kanuni, sheria, maadili na utu wema. Huu ni wakati kwa wanataalimungu na wanasayansi kushirikiana kwa karibu zaidi kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Kwa pamoja kuna haja ya kujenga na kudumisha mafungamano mapya kati ya Talimungu na Sayansi, ili kujenga madaraja ya kukutana na kujadiliana katika ukweli na uwazi!