Mchango wa Wanasiasa Wakatoliki Katika Masuala ya Kisiasa: Utu!
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. –Vatican.
Siasa ni sehemu ya vinasaba vya maisha ya binadamu na kwamba, siasa safi hutekelezwa kwa kufuata katiba, sheria na kanuni maadili; mambo msingi katika kukuza na kudumisha misingi ya amani, haki, ustawi na maendeleo ya wengi. Siasa safi ni kielelezo cha hali ya juu kabisa cha upendo katika jamii; ni matunda ya ukomavu yanayojikita katika uongozi bora, maridhiano, utawala wa sheria, uvumilivu, uaminifu na bidii. Kamwe tofauti za kiitikadi kisiwe ni chanzo cha vita, kinzani, vurugu na mipasuko ya kijamii inayowatumbukiza watu kwenye majanga na maafa makubwa! Baba Mtakatifu Francisko anasema, siasa safi ni huduma kwa ajili ya wananchi; inayofumbatwa katika sanaa ya kusikiliza na kushirikisha karama na mapaji kwa ajili ya ujenzi wa jamii inayosimikwa katika misingi ya haki na usawa; maskini na akina “yakhe pangu pakavu tia mchuzi” wakipewa kipaumbele cha kwanza. Lakini, ikumbukwe kwamba, amani ni tete sana inapaswa kulindwa na kuhifadhiwa kama mboni ya jicho! Huduma ya amani inajengwa katika mahusiano na mafungamano ya kijamii; kwa njia ya ushirikiano na mshikamano wa jamii na jumuiya ya Kimataifa.
Ni katika muktadha huu, hivi karibuni, wanasiasa wakatoliki wenye dhamana na utume katika medani mbalimbali za maisha, wamekuwa na mkutano wao wa pili kimataifa mjini Madrid, Hispania. Ni mkutano ulioandaliwa na Jimbo kuu la Madrid, Hispnia kwa kushirikiana na Taasisi ya Viongozi Wakatoliki wa Amerika ya Kusini “Academia Latinoamericana de Líderes Católicos” pamoja na Mfuko wa Konrad Adenauer. Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican, kwa namna ya pekee kabisa katika hotuba yake elekezi amekazia utamaduni wa watu kukutana sanjari na ujenzi wa urafiki wa kijamii kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu katika nchi husika. Leo hii, Jumuiya ya Kimataifa inakabiliwa na changamoto ya maambukizi makubwa ya Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19, tiba na chanjo yake ambayo imepokelewa kwa hisia tofauti sehemu mbalimbali za dunia. Ili kuweza kukabiliana na changamoto kama hizi kuna haja kwa Jumuiya ya Kimataifa kujikita katika diplomasia, ili kuiwezesha Jumuiya ya Kimataifa kutekeleza sera na itifaki za Kimataifa zilizokwisha kupitishwa.
Hii ni changamoto ya kujenga na kudumisha utamaduni wa watu kukutana katika siasa kama kielelezo cha huduma makini kwa watu wa Mungu, kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Janga la Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19 linahitaji mchakato utakao imarisha: Usawa wa kijamii, kuchochea na kukuza ukuaji wa uchumi sanjari na miundombinu inayopatikana katika nchi husika. Utu, heshima na haki msingi za binadamu ni mambo msingi katika kufikia ufumbuzi wa changamoto hii. Urafiki wa kijamii ni jambo linalohitajika sana, ili kweli siasa iweze kuwa ni chombo cha huduma kwa binadamu inayokita mizizi yake katika majadiliano, upatanisho na utamaduni wa watu wa kukutana. Mahusiano ya urafiki wa kibinadamu yajengeke katika misingi ya haki na udugu wa kibinadamu, vinginevyo urafiki dhaifu wa kijamii unaweza kuwa ni chanzo cha kinzani, vita na mipasuko ya kijamii na ubaguzi. Mambo yote haya katika miaka ya hivi karibuni yamebadilisha sana mwelekeo wa maisha ya kijamii kiasi cha kuvunjilia mbali miundo mbinu na tunu msingi za rejea katika mchakato wa mafungamano ya kibinadamu.
Kardinali Pietro Parolin anasema, Ili kukabiliana na changamoto mamboleo kuna haja kwa Jumuiya ya Kimataifa kujenga jamii inayosimikwa katika misingi ya haki, amani, na maridhiano, ili kamwe asiwepo mtu anayebaki nyuma katika utekelezaji wa vipaumbele vya kijamii. Utengano ni udhaifu, kwani watu wanategemeana na kukamilishana na wala hakuna mtu anayeweza kuishi kama Kisiwa peke yake. Sera na mikakati ya muda mfupi na mrefu ziandaliwe ili kukabiliana na changamoto mamboleo! Nguvu za kiuchumi zielekezwe zaidi katika ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Utu, heshima na haki msingi za binadamu zipewe uzito wa pekee. Jumuiya ya Kimataifa haina budi kuendelea kupambana na baa la njaa, ujinga na umaskini. Ubinafsi, uchoyo na utaifa usiokuwa na mvuto wa la mashiko vifutiliwe mbali. Na badala yake, Jumuiya ya Kimataifa ishikamane kikamilifu ili kulinda na kutetea ustawi, maendeleo na mafao ya wengi! Haki msingi za binadamu ziwe ni dira na nguvu yao. Urafiki wa kijamii na utamaduni wa watu kukutana katika ukweli na uwazi ni nyenzo msingi katika kupambana mambo yote yanayosigana na utu, heshima na haki msingi za binadamu. Viongozi wa Serikali waendelee kutekeleza wajibu wake kikamilifu na kwa upande wa viongozi Wakristo waongozwe pia na dhamiri nyofu!