Tafuta

Kardinali Robert Sarah amemwandikia waraka maalum Kiongozi wa kijeshi wa Guinea Luteni-Kanali Mamady Doumbouya kuhusu mambo msingi yanayopaswa kuzingatiwa wakati huu! Kardinali Robert Sarah amemwandikia waraka maalum Kiongozi wa kijeshi wa Guinea Luteni-Kanali Mamady Doumbouya kuhusu mambo msingi yanayopaswa kuzingatiwa wakati huu! 

Kardinali R. Sarah "Amtwanga" Barua Kiongozi wa Kijeshi Guinea!

Kiongozi wa kijeshi wa Guinea Luteni-Kanali Mamady Doumbouya ameandikiwa waraka maalum na Kardinali Robert Sarah anayekazia: Utawala wa sheria na demokrasia shirikishi. Ni wakati wa kupambana na umaskini, ujinga na maradhi, ili wananchi wa Guinea waanze kucharuka katika maendeleo fungamani ya binadamu; kwa kukazia utu, heshima na haki msingi za binadamu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. –Vatican.

Kardinali Robert Sarah, Mwenyekiti mstaafu wa Baraza la Kipapa la Ibada na Nidhamu ya Sakramenti za Kanisa kutoka nchini Guinea amemwandikia Kiongozi wa kijeshi wa Guinea Luteni-Kanali Mamady Doumbouya barua maalum! Katika barua hii anakazia umuhimu wa utawala wa sheria na demokrasia shirikishi. Ni wakati wa kujifunga kibwebwe kupambana na umaskini, ujinga na maradhi, ili wananchi wa Guinea waanze kucharuka katika maendeleo fungamani ya binadamu; kwa kukazia utu, heshima na haki msingi za binadamu katika ujumla wake. Ni muda muafaka wa kuanza kuunda kada ya wanasiasa watakaojisadaka kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu katika ujumla wake. Rushwa ni adui wa haki, utu na heshima ya binadamu, kiongozi huyu awe mstari wa mbele kupambana na rushwa inayopekenya na kusigina utu na haki msingi. Kabla ya kufikiria uchaguzi mkuu wa Rais na Wabunge, Kamati ya Kitaifa ya Maridhiano na Maendeleo iweke msingi madhubuti wa uchumi; ijenge na kuimarisha umoja wa Kitaifa kwa kuwaruhusu wananchi wa Guinea waliko nje ya nchi kurejea na kujiunga katika mchakato wa ujenzi, ustawi na maendeleo ya nchi yao. Siasa za chuki, uhasama na mauaji hazina nafasi tena nchini Guinea, bali wananchi wajenge umoja na udugu wa kibinadamu, kwa kuheshimiana na kuthaminiana licha ya tofauti zao msingi!

Kardinali Robert Sarah anasema, Kamati ya Kitaifa ya Maridhiano na Maendeleo imefanya mapinduzi ya kijeshi hapo tarehe 5 Septemba 2021 na kuifanya historia ya Guinea kujirudia tena kama ilivyojitokeza kunako mwaka 1948, mwaka 1984 na Mwaka 2008. Haya ni mapinduzi ambayo watu wengi wanaona mwanga wa matumaini ya kurejea tena kwa kwa misingi ya haki, amani, ustawi, maendeleo na utawala wa sheria. Guinea imebahatika kuwa na utajiri mkubwa wa maliasili na madini, lakini bado wananchi wake wanaogelea katika dimbwi la umaskini, magonjwa na njaa. Huu ni wakati wa kuandika historia mpya ya Guinea na kuepuka makosa yaliyofanywa na serikali zilizokuwa chini ya utawala wa Rais Ahmed Sékou Touré, Rais Lansana Contè, Rais Moussa Dadis Camara pamoja Alpha Condè, walishindwa kuwaletea wananchi wa Guinea furaha na matumaini ya maisha bora zaidi. Huu si wakati wa “kushona kiraka cha nguo mpya katika vazi kuukuu” Rej. Mk 2:21-22. Huu ni wakati muafaka wa kupyaisha kada ya wanasiasa nchini Guinea. Wanapaswa kutambua kwamba, haki na usawa; tabia ya kuheshimiana na kuthaminiana kama binadamu; ukweli, uwazi na uaminifu ni tunu msingi zinazoboresha siasa safi.

Mwanasiasa bora ni yule anayetambua dhamana na wajibu wake kwa jamii; anayeaminika na kuthaminiwa na jamii; ni kiongozi anayejitaabisha kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi; mwaminifu katika ahadi zake kwa wananchi waliomchagua, daima akijitahidi kujenga na kudumisha umoja na mshikamano, tayari kuchochea mageuzi katika maisha ya watu; kwa kuwasikiliza na kutenda kwa ujasiri! Siasa safi inayojikita katika ujenzi wa amani inatambua karama za watu na inaendeleza majadiliano na watu kuaminiana na kuthaminiana badala ya kuangaliana kwa “jicho la kengeza.” Kardinali Robert Sarah anasema kwamba, Guinea inahitaji wanasiasa wazalendo, wanaoweza kusimama kidete kuunganisha nguvu zao kwa ajili ya mchakato wa ujenzi wa haki, amani na umoja wa Kitaifa, ili kudumisha udugu wa kibinadamu na kuondokana siasa za chuki na kutaka kulipizana kisasi. Jeshi litekeleze wajibu wake wa kulinda usalama wa raia na mali zao kwa kuwarejeshea tena demokrasia na utawala wa sheria; utu, heshima na haki zao msingi.

Huu si muda kwa wanajeshi kujitarisha wenyewe na kusahau umaskini, magonjwa na baa la njaa linalosigina wananchi wa Guinea. Watu wanahitaji huduma bora za afya, elimu na ustawi wa jamii. Wananchi wamechoka na rushwa na ufisadi wa mali ya umma; wanahitaji kuona viongozi wazalendo, waadilifu, wanyofu na wa kweli kwa nchi yao. Kuweza kuwa na viongozi wazalendo na wenye uchungu wa maendeleo kwa nchi yao, anapaswa kufungua akili, uzoefu na historia ya Guinea ili kutafuta watu watakaomsaidia kupyaisha maisha ya wananchi wa Guinea. Kiongozi wa kijeshi wa Guinea Luteni-Kanali Mamady Doumbouya, asikubali kupelekeshwa “mkuku” na baadhi ya wanasiasa wenye uchu wa mali na madaraka. Kabla ya kufikiria uchaguzi mkuu wa Rais na Wabunge, Kamati ya Kitaifa ya Maridhiano na Maendeleo iweke msingi madhubuti wa uchumi; ijenge na kuimarisha umoja wa Kitaifa kwa kuwaruhusu wananchi wa Guinea waliko nje ya nchi kurejea na kujiunga katika mchakato wa ujenzi, ustawi na maendeleo ya nchi yao.

Wananchi wa Guinea wasikubali kutumbukizwa katika utamaduni wa kifo kwa maandamano yasiyokuwa na tija, mshiko wala mvuto! Kila mwananchi atambue kwamba, anao wajibu wa kujenga na kuboresha maisha yake mwenyewe na wala hakuna mwanasiasa atakayewaletea hali nzuri ya uchumi au furaha ya maisha bila kuwajibika na kufanya kazi kwa juhudi na maarifa. Kila mwananchi lazima ajifunge kibwebwe kupambana na umaskini wa hali na kipato sanjari na mmong’onyoko wa maadili na tunu msingi za kijamii. Kardinali Robert Sarah, Mwenyekiti mstaafu wa Baraza la Kipapa la Ibada na Nidhamu ya Sakramenti za Kanisa anasema anapenda kuhitimisha barua hii, kwa kumwomba kwa heshima na taadhima kumtunza Rais Alpha Condé aliyepinduliwa kutoka madarakani kwa heshima na kama inawezekana basi amwachie huru mara moja!

Itakumbukwa kwamba, Umoja wa Mataifa, Umoja wa Afrika, Jumuiya ya Kiuchumi ya Nchi za Afrika Magharibi (ECOWAS), Marekani na Ufaransa zilishutummu na kulaani vikali mapinduzi ya kijeshi nchini Guinea na kutaka Rais Rais Alpha Conde kuachiliwa huru mara moja. Bwana Jean Claude Brou, Rais wa Jumuiya ya Kiuchumi ya Mataifa ya Afrika Magharibi ECOWAS, alisema viongozi wakuu wa Mataifa ya Afrika Magharibi wamesisitiza pia kwamba hakupaswi kuwepo na haja ya kipindi kirefu cha mpito kwa taifa hilo kurejea kwenye mkondo wa kidemokrasia. Hivyo katika miezi sita, uchaguzi unapaswa kufanyika ili kurejeshwa kwa utaratibu wa kikatiba katika jamhuri ya Guinea. Umoja wa Afrika wamesimamisha uanachama Guinea kwa muda. ECOWAS imetoa wito pia kwa Umoja wa Afrika, Umoja wa Mataifa na Umoja wa Ulaya kuunga mkono vikwazo dhidi ya utawala wa kijeshi, unaojulikana kama Kamati ya Kitaifa ya Maridhiano na Maendeleo au kwa kifupi, CNRD.

ECOWAS ilikuwa imetuma ujumbe nchini Guinea hivi karibuni ili kukutana na kiongozi wa mapinduzi Luteni Kanali Mamady Doumbouya, na ilikuwa inasubiri kuchukuwa uamuzi juu ya namna ya kuushinikiza utawala wa kijeshi kurejea tena kwenye utawala wa kikatiba. Rais Alpha Condé aliyepinduliwa kutoka madarakani alitaka kupindisha Katiba ya nchi kwa kujiongezea muhula wa tatu wa uongozi kinyume cha Katiba ya nchi. Rais Alpha Condé aliyeondolewa madarakani kwa mapinduzi ya kijeshi aliingia madarakani kunako mwaka 2010 baada ya kushinda Uchaguzi wa kwanza wa kidemokrasia nchini Guinea tangu walipojipatia uhuru kutoka kwa Wafaransa mwaka 1958.

Kardinali Sarah
20 September 2021, 15:28