2020.12.28 Watoto watakatifu mashahidi 2020.12.28 Watoto watakatifu mashahidi 

Papa Francisko:Herode wapya wa siku zetu wanaangamiza watoto wasio na hatia

Katika siku ambayo Mama Kanisa kila tarehe 28 Desemba ya kila mwaka anaadhimisa Siku Kuu ya Watoto Watakatifu mashihidi walioangamizwa na Mfalme Herode,Papa Francisko katika ujumbe mfupi katika mtandao wa kijamii anaomba kusali kwa ajili ya watoto,na kuwalinda watakatifu wasio na hatia.Herode wapya wa siku zetu wanaangamiza watoto wasio kuwa na hatia chini ya vivuli utumwa na ukahaba.

Na Sr. Angela Rwezaula - Vatican

Tarehe 28 Desemba ya kila Mwaka Mama Kanisa anaadhimisha Sherehe ya Watoto Mashahidi ambao waliomshuhudia Kristo Yesu hata kama hawakuwa na maneno lakini kwa maisha yao kutokana na ukatili wa Mfalme Herode. Mama Kanisa amekuwa akitetema maisha kwani ni zawadi kutoka kwa Mungu. Watoto waliuwawa kikatili kwa upanga mara baada ya Herode kusika kwamba amezaliwa Mfalme katika mji wa Betlehemu baada ya kuuliza hasa walipoondoka mamajusi bila kurudi kwake kumpa taarifa. Katika fursa hiyo Papa Francisko kwa ujumbe mfupi katika mtandao ya kijamii, amegusa maangamizi hayo kutoka kwa Herode kutokana na mtoto aliyezaliwa Bethlehemu, yaani nyumba ya mkate. Papa ameandika kuwa: “Herode wapya wa siku zetu wanaangamiza watoto wasio kuwa na hatia chini ya vivuli vya kazi za utumwa, ukahaba, unyonyaji, katika vita na uhamiaji wa kulazimasha. Kwa maana hiyo tuombe kwa pamoja leo hii na kusali kwa ajili ya watoto hao, kwa kutetea na kuwalinda watakatifu wasio kuwa na hatia”.

Ndugu msikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican na msomaji, kwa kutazama ujumbe mfupi wa Papa katika mitandao ya kijamii tunaweza kutafakari kwa kina siku hii ya watoto watakatifu mashidi au wafiadini ambao kwa sababu ya Herode mwenye hofu ya mfalme wa amani, mwenye ukatili dhidi ya mafanikio ya wengine, mwenye roho mbaya na kutojali kwamba wapo maherode wa nyakati zetu. Herode ni wengi mno, kuanzia ndani ya familia zetu, jirani zetu, mitaani kwetu, vitongoji kwetu, miji yetu, walio na tabia hizi za chuki, hasira, husuda, wivu, ubinafsi, ukatili, ushirikina, ujambazi, ugumu wa mioyo na kila aina na matukio ambayo yanakwenda kinyume na maisha ya mwanadamu aliyeumwa kwa mfano wa Mungu.

Wapo Herode wengi ambao hawalali kwa sababu ya kupanga njia potofu za ukatili, ndani ya giza, hata baada ya kugunduliwa, licha ya kuonywa na ndugu na mjariani wema, lakini bado wengine hawasikii wanaendelea na tabia za ukatili, za kuua, za kuharibu watoto wa ndugu zao, majirani na marafiki vijana wengi. Katika siku kuu hii ya Watoto Watakatifu mashahidi, kwa hakika inaibua kwa upya ndani  mwetu hisia kali na ya uchungu kwa kishiriki kile ambacho kimeelezwa katika Injili ya Matayo:“Ndipo lilipotimia neno lililonenwa na nabii Yeremia, akisema, Sauti ilisikika Rama, Kilio, na maombolezo mengi, Raheli akiwalilia watoto wake, Asikubali kufarijiwa, kwa kuwa hawako” (Mt 2,17-18). Ni kutokana na kushuhudia kila kikicha na matukio machafu sana katika mitandao ya kijamii, (kwa mfano hivi majuzi wameonesha mtoto anayedaiwa kufa mnamo 2017,  sehemu moja ya Tanzania na akapatikana tena katika maeneo mengine mzima na hawezi kuzungumza kwa sababu alikatwa sehemu ya ulimi,na  habari hiyo bado inazunguka na upelelezi wa Polisi unaendelea kutekelezwa), lakini pia hata yale ambayo hatuyaoni kwenye mitandao ya kijamii au vyombo vya habari, kwamaana ni mengi mno kila kitongoji, kijiji au mijini, ikiwa ni kudhihirisha kuwa maherode wapo wengi mno kila kona ya ulimwengu.

Ndugu msomaji ni kwa mara nyingine tena, tarehe 28 Desemba katika siku hii muhimu, inatukumbusha kwa mara nyingine tena kuwa ni wakati wa uongofu maana mbele ya Mungu wote watahukumiwa, kama ambavyo wanalaamiwa wale wote watendao ukatili wa matendo yao mabaya hapa duniani, laana watakutana nayo mbinguni. Kuna msema wa kiitaliano usemao “Kitanda ukitandikavyo kama hakuna mtu wa kukiharibu unakikuta hivyo hivyo”, ikiwa na maana ya kwamba laana unajiandalia mwenyewe. Ni wakati wa kuongoka weewe unayeandaa mitego kuwaharibu watoto na vijana katika makuzi yao(kama alivyosema Papa, kuwafanya watumwa, kuwaweka kwenye ukahaba, kuwanyonya, kuwakeka katika vita na kuwalazimisha kuhama. Hama kweli Herode wa nyakati zetu ni wengi). Ni mwaliko  wa kuondoa ndani ya myo uherode wako, maana  katika nyakati hizi tunawaona Herode wengi ambao wanawinda watoto wengi wachanga, aidha kuwaiba, au wakiwemo hata bado tumboni mwa Mama zao na kutoa mimba. Kwa upande wa vijana wasichana ni maswali ya kujiuliza je mnaogopa nini kuwa mama? Je mnafikiri mtaharibika uzuri wenu? Ni jambo la kusikitisha na kuhuzunisha!

Kwanini muue watoto na mbaki mnatembea na makaburi yaliyopakwa rangi? Damu ya watoto hao inabubujika. Je unaweza kujitofautisha na Herode?  La hasha! maana Wewe ni zaidi ya Herode, kwa sababu unaua kiumbe ulicho nacho tumboni mwako. Ni watu wangapi pia wanauza madawa ya kutoa mimba, wanatoa ushauri kwa wengine kutoa mimba kwa sababu ya madai mimba imepatikana kusiko na muafaka. Ni kweli Herode wa wakati wetu ni wengi mno! Ni wakati sasa wa kulinda na kutetea maisha ya watoto wachanga tangu Kutungwa kwake hadi kufika kifo chake cha kawaid. Hatuwezi kuendelea kuangamiza maisha ya wengine. Ni Mungu pekee yake mwenye kuleta uhai na mwenye mamlaka ya kuyachukua. Sisi hatuna mamlaka ya kufanya hivyo kama Herode aliyetumia upanga, kwani kwa kutumia upanga nawe utaangamia kwa upanga.

Mtakatifu Matayo katika Unjili yake anasema: “Watu wale waliokaa katika giza Wameona mwanga mkuu, Nao waliokaa katika nchi na uvulivu wa mauti Mwanga umewazukia” (Mt 4, 16). Ni wazi kabisa kwamba hata leo hii wengi wanaishi katika giza, wanatembea katika giza, mioyo yao iko gizani, wanavaa vizuri na kung'ara usoni, lakini mioyo yao imegubikwa na Herodi... na BWANA mungu aliyejifanya mtoto ili kuja kama nuru ituangazie lakini bado hatujaguswa. Mwinjili Yohane anasema: “Kulikuwako Nuru halisi, amtiaye nuru kila mtu, akija katika ulimwengu. Alikuwako ulimwenguni, hata kwa yeye ulimwengu ulipata kuwako, wala ulimwengu haukumtambua.” (1, 9-13).  Mwinjili Yohane anamtofautisha Yesu, kuwa ndiye nuru ya kweli inayokuja ulimwenguni. Kwa maana hiyo ikiwa sisi tunatamani kutembea katika nuru, katika iliyo kweli, basi leo hii tunaalikwa kumpokea Yesu.  Neno wa Mungu aliyefanyika mwili, hasa kwa kulishika Neno lake kwa hakika ili tuweze kutembea katika nuru na kweli. Ni jambo la kusikitisha sana pamoja na ujio wa nuru ya kweli, lakini bado si wote wamempokea na ndiyo maana Herode ni wengi leo hii!  Mwinjili Yohane alisema: “Alikuja kwake, wala walio wake hawakumpokea. Bali wote waliompokea aliwapa uwezo wa kufanyika watoto wa Mungu, ndio wale walioaminio jina lake; waliozaliwa sio kwa damu, wala si kwa mapenzi ya mtu, bali kwa Mungu.”

Ndugu msomaji katika siku kuu ya watoto watakatifu Mashaidi kwa hakika tuguswe na tunaguzwa kila pembe na hali ya mwanadamu  na ili tupate kubadilika na kuwa na uongofu wa kweli. Neno la Mungu linakujia kwa unyenyrkevu wa kitoto kichanga kikiwa horini na kukueleza, usiende kumwambudu  ukiwa  na moyo wa kiherode, kwa maana anakuona kama unavyojiona nafsi yako na dhamiri yao na hawa wale ambao wamekuzunguka na wanaona matendo yako. Jitakase, usiwadanganye, maana unajidanganya mwenyewe. Siku zaja, hakutasalia hata mlima wowote wa kiburi, utakuwa majivu maana hukupenda kusikia neno la Bwana.  Nabii Yeremia anasema: “Tazama, siku zinakuja, asema BWANA, nitakapolitimiza neno lile jema nililolinena, katika habari za nyumba ya Israeli na katika habari za nyumba ya Yuda (Yer 33:14)”, pia Bwana anasema “Amin, nawaambieni, Halitasalia hapa jiwe juu ya jiwe ambalo halitabomoshwa. Heri mtumwa yule, ambaye Bwana wake ajapo atamkuta akifanya hivyo.Amin, nawaambieni, atamweka juu ya vitu vyake vyote”, (Mt 24, 1-2.46- 47).

HERODE NI WENGI
28 December 2021, 17:18