Tafuta

Baraza la Maaskofu Tanzania linamshukuru na kumpongeza Askofu mkuu Marek Solczyński, aliyekuwa Balozi wa Vatican nchini Tanzania kwa huduma na utume. Baraza la Maaskofu Tanzania linamshukuru na kumpongeza Askofu mkuu Marek Solczyński, aliyekuwa Balozi wa Vatican nchini Tanzania kwa huduma na utume. 

Maaskofu Katoliki Tanzania: Askofu mkuu Marek, Shukrani Kwa Utume

Askofu mkuu Marek Solczyński ameshiriki na kufanikisha mchakato kwa kupatikana Maaskofu wapya saba (7). Maaskofu wengine sita wakihamishwa kwenda mahali walipohitajika zaidi. Ameongoza mchakato wa kupandishwa hadhi eneo moja la Kanisa la Tanzania kuwa Jimbo Kuu, huku Majimbo makuu matatu yakipata Maaskofu wakuu: Arusha, Mbeya na Jimbo kuu la Mwanza.

Na Askofu Flavian Matindi KASSALA, - Jimbo Katoliki la Geita, Tanzania.

Askofu Flavian Matindi Kassala wa Jimbo Katoliki Geita, ambaye pia ni Makamu wa Rais Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania anapenda kumshukuru na kumpongeza Askofu mkuu Marek Solczyński katika maisha na utume wake, kielelezo cha mchungaji mwema na mwombaji wa wachungaji. Sasa ni wakati wa kwenda kwenye vijijini vingine ili kutangaza na kushuhudia wema, utakatifu na ukuu wa Mungu kwa waja wake. Askofu Flavian Matindi Kassala aandika akisema: Ilikuwa ni tarehe 25 Aprili 2017 tulipopata habari njema ya furaha kuu kwa watu wote wa Mungu kwamba, Baba Mtakatifu Francisko amemteuwa na kumtuma Askofu mkuu Marek Solczyński kama mwakilishi wake katika nchi na Kanisa la Tanzania. Mtumishi huyu wa Kanisa aliyejitoa bila kujibakiza kulitumikia Kanisa la ulimwengu, alifika nchini na kuanza mara utume wake, huku akijikabidhi kwa hali zote kwa utendaji wa Kanisa, bali kujali upya wa tamaduni za hapa kwetu na huko alikotoka kiutumishi, na hata za nyumbani kwao Poland. Habari hii njema imeishia tarehe 2 Februari 2022 wakati ambapo mamlaka ya juu ya Kanisa iliona tunu hii ya Kanisa ikaangaze katika mazingira ya Uturuki na Azerbaijan. Kwa kipindi cha utume wake nchini Tanzania tumepata nafasi ya kumsoma na kumfahamu Askofu mkuu Marek, ambaye kabla ya yote yeye ni Askofu mkuu wa Jina (Titular Archbishop) wa Kaisaria ya Mauritanis (Caesarea in Mauretania). Mbali na hilo, utumishi wake umedhihirisha alivyo mbobezi katika masuala ya Diplomasia na Uongozi wa Kanisa.

Alishiriki kikamilifu katika maisha na utume wa Kanisa la Tanzania
Alishiriki kikamilifu katika maisha na utume wa Kanisa la Tanzania

Askofu Mkuu Marek – ‘Mswahili kweli kweli’: Pamoja na upya aliokutana nao katika lugha ya Kiswahili, Askofu mkuu Marek hakuchukua muda mrefu kuingia katika ulimwengu wa Kiswahili. Akianza na umahili katika kujua kukisoma Kiswahili na kutamka kwa ufasaha maneno yake, hasa yale yaliyohusika na maadhimisho ya Ibada Takatifu, bado hakusita kutupia maneno machache ya Kiswahili hata pale alipokuwa akiongea Kiitalia au Kiingereza, lugha alizotumia kikazi. Juhudi hii ilimpatia matunda ya haraka kuingia katika kufahamu Lugha ya Kiswahili na hata alipochomekea aliyaweka maneno au sentensi za Kiswahili mahali palipostahili kabisa. Alikuwa na hata kufikia kumudu adhimisho la Misa Takatifu na hata utoaji wa Sakramenti ya Kipaimara kwa lugha ya Kiswahili fasaha kabisa. Mara kadhaa, Askofu Mkuu Solczyński amediriki hata kusoma Nyaraka za Kipapa zilizohusu uteuzi wa Maaskofu (Papal Bull) kwa tafsiri ya Kiswahili. Yote katika yote, ni pale alipoongoza Ibada ya Kuwekwa Wakfu, kama mwadhimishaji mkuu, pale Jimboni Morogoro, kwa lugha ya Kiswahili. Kwa kifupi, anaondoka akiwa ‘Mswahili’ kabisa kati yetu Waswahili.

Askofu Mkuu Solczyński – ‘Mchungaji Mwema’: Askofu Mkuu Solczyński sanjari na kupenda sana Lugha ya Kiswahili, amejitahidi sana kufuatilia na kujua mira na desturi za watu wa Tanzania katika mazingira yao kwa kuwatembelea na kutoa huduma za kichungaji. Mahusiano ya kichungaji ya Askofu mkuu Marek katika Tanzania hayakufungwa tu na Jimbo Kuu la Dar Es Salam, mahali alipokuwa akiishi. Amaonekana sehemu mbali mbali za nchi kwa ajili huduma za kichungaji. Ni wazi kwamba alipaswa kuhudhuria Ibada mbalimbali hasa za kuweka wakfu na kusimikwa maaskofu. Lakini juu ya hayo yote, hakusita kutoa huduma za kichungaji pale palipokuwa na upungufu wa wachungaji wakuu katika majimbo kadhaa nchini. Aliongoza Ibada za Juma Kuu, na Kubariki Mafuta Matakatifu katika mjimbo kadhaa nchini kulipotokea dharura ya kutokuwepo Mchungaji mkuu wa jimbo. Ameshiriki pia katika kazi mbalimbali za kuchungaji, hasa katika Jimbo Kuu la Dar Es Salam, ikiwemo utoaji wa Sakramenti ya Kipaimara, sambamba na kutekeleza vyema utume wake wa Kibalozi. Anaondoka akiacha sura hiyo ya Mchungaji Mwema aliyewajua Kondoo wake na kujitoa bila kujibakiza kwa ajili yao.

Alijenga na Kuimarisha Urika wa Maaskofu na Khalifa wa Mtakatifu Petro.
Alijenga na Kuimarisha Urika wa Maaskofu na Khalifa wa Mtakatifu Petro.

Askofu Mkuu Marek Solczyński – ‘Mwombaji wa Wachungaji’: Bwana wetu Yesu Kristo alituagiza kumwomba Bwana wa Mavuno apeleke watendakazi katika shamba lake (Rej. Mt. 9:38). Kwa kipindi cha utume wake, Askofu Mkuu Marek Solczyński amedhihirisha kuwa mmoja wapo waliozingatia agizo hilo la Kristo. Ameishi na kutenda katika kuomba wachungaji bila kuchoka. Katika uwepo wake Tanzania ameyagusa kwa namna pekee makanisa mahalia kadhaa katika kuungana nayo kumwomba Bwana wa mavuno apeleke watenda kazi katika mavuno yake. Ameshiriki na kufanikisha mchakato kwa kupatikana Maaskofu wapya saba (7). Wakati huo huo, Maaskofu wengine sita wakihamishwa kwenda mahali walipohitajika zaidi. Ameongoza mchakato wa kupandishwa hadhi eneo moja la Kanisa la Tanzania kuwa Jimbo Kuu, huku maeneo matatu nchini yakipata Maaskofu Wakuu (Arusha, Mbeya na Mwanza). Hakusita pia kuwapumzisha ndugu zake walioonekana kuwa na uhitaji huo, hali wengine akiendelea kuwatia moyo waendelee na utume hata kama wakati wa mapumziko ulikuwa umefika. Kwa ufupi, pamoja na kuwa na mahusiano mazuri na maaskofu wote nchini, Askofu Mkuu Marek Solczyński ameyagusa kwa namna ya kipekee maisha ya kichungaji ya maaskofu 16 yaliyohusu uteuzi, uhamisho, na ustaafu.

Askofu mkuu Marek: ‘Ni Wakati Wa Kwenda Vijiji Jirani.’ Bado pamoja na kuwa uhamisho wake uko katika taratibu za kiutendaji katika nafasi yake na asili ya utume wake kwa Kanisa la Tanzania, Askofu Mkuu Marek Solczyński anaonekana kama ameondoka mapema kabla ya wakati. Uzoefu aliojichumia kwa kipindi hiki kifupi ulifanya tujisikie kuwa shughuli yake na mahusiano naye ni suala jepesi kihivyo. Askofu Mkuu Marek amehusiana kwa ukaribu sana na Maaskofu kwa kiasi kikubwa. Amekuwa sehemu ya utatuzi wa changamoto mbalimbali katika Kanisa la Tanzania, kwa kuona fursa na kujenga matumaini makubwa. Hata hivyo, lazima tukubali kuwa ni wakati kwa kwenda katika vijiji vingine pia akahubiri huko nako, kwani ni kwa hayo alikuja (Rej. Mk 1:38). Letu ni kumtakia kila jema katika utendaji wake huo mpya. Anatuachia hazina ya mema yote aliyolitendea Kanisa la Tanzania; mema ambayo tunaamini ni mbegu itakayoendela kuzaa na kukua. Tunaomba shukrani zetu zimsindikize na kumtia nguvu zaidi katika yaliyo mbele yake.

+ Flavian M. Kassala, Jimbo Katoliki la Geita.

Balozi wa Vatican

 

21 February 2022, 15:57