Je watu wanaweza kujikomboa dhidi ya vita vya wenye nguvu?
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Katika mchakato wa safari ya maisha, watu wameteseka sana kwa sababu ya vita vya wenye nguvu. Ni wathirika wangapi wasio na hatia, machozi mangapi, uchungu kiasi gani kwa sababu ya vita vilivyopiganiwa na wadhaifu kwa ajili ya wenye nguvu. Vita ambavyo vimewafanya watu wadhaifu kuwa wadhaifu zaidi na wenye nguvu kuwa wenye nguvu zaidi. Katika siku hizi zinaashiria uwezekano wa vita ya tatu ya dunia. Na hii inatisha kusikia tu inazungumzwa juu yake. Ndivyo anaandika Dk. Sergio Centofanti Makamu Mhariri wa Baraza la Kipapa la Mawasiliano katika maoni yake kuhusu suala upepo unaovuma wa kivita kati ya Urusi na Ukraine.
Kwa mara nyingine tena unasikikia bado leo hii ule wito wa kinabii wa Mtakatifu Yohane Paulo II, wakati wa Noeli ya mwaka 1990, kabla ya kuzuka kwa Vita vya Ghuba kwamba: “Na washawishiwe wanaohusika kwamba vita ni tukio lisilo na kurudi! Hata leo hii, baada ya zaidi ya miaka 30, tunalipa matokeo ya vita hivyo: jeuri, vurugu, ugaidi, vita vingine, watu wengine wanaoteseka.
Akiendelea na ufafafanuzi wa maoni yake Dk. Centofanti anaandika kuwa leo tunasikiliza sauti ya wakuu wanaozungumza juu ya vita. Tunahitaji kusikiliza sauti ya watoto wadogo wanaozungumza juu ya amani. Tayari imetokea katika historia. Gandhi alihamasisha watu waliojumuisha wingi wa wadogo, mamilioni ya wadogo walioungana walishinda kwa amani na wakati ilikuwa inaonekana kuwa haiwezekani. Pia katika karne iliyopita, tawala za kidikteta zenye nguvu zilionekana kuwa haziwezi kushindwa, zilianguka bila vurugu, kwa sababu ya watu wasio na ulinzi waliasi.
Kwa kuhitimisha Dk. Sergio Centofanti anandika kuwa Injili inatangaza kuwa “heri wapatanishi na wahudumu wa amani”. “Vita ni wazimu”, alisema Papa Francisko kwa sababu huleta mateso na uharibifu kwa watu. Lakini je, Watu wanaweza kujikomboa dhidi ya vita vya wenye nguvu? Hapana. “Lazima wajikomboe”.