Tafuta

Maadhimisho ya Siku ya Pili ya Udugu wa Kibinadamu tarehe 4 Februari 2022: Ujumbe kutoka kwa viongozi wa Jumuiya ya Kimataifa. Maadhimisho ya Siku ya Pili ya Udugu wa Kibinadamu tarehe 4 Februari 2022: Ujumbe kutoka kwa viongozi wa Jumuiya ya Kimataifa. 

Maadhimisho ya Siku ya Pili ya Udugu wa Kibinadamu: Mshikamano!

Waraka wa Kitume wa Baba Mtakatifu Francisko "Fratelli tutti": Yaani “Wote ni Ndugu”: Kuhusu Udugu na Urafiki wa Kijamii” unachota utajiri mkubwa kutoka katika Hati ya Udugu wa Kibinadamu kwa Ajili ya Amani na Utulivu uliotiwa saini kati ya Baba Mtakatifu Francisko na Dr. Ahmad Al-Tayyib, tarehe 4 Februari 2019 huko Abu Dhabi, Umoja wa Falme za Kiarabu. Mshikamano wa udugu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Rais Joseph Robinette Biden Jr. wa Marekani, katika Maadhimisho ya Siku ya Pili ya Kimataifa ya Udugu wa Kibinadamu tarehe 4 Februari 2022, anawaalika watu wote kushikamana na kushirikiana ili kukabiliana na changamoto katika ulimwengu mamboleo katika mshikamano wa udugu wa kibinadamu, ili kukoleza majadiliano katika ukweli na uwazi, ili kudumisha maridhiano, ujenzi wa jamii jumuishi na uelewa. Waamini wa dini mbalimbali duniani wajenge utamaduni wa upendo, wasimame kidete kuwalinda na kuwahudumia maskini na wanyonge ndani ya jamii; ili kudumisha utu, heshima na haki msingi za binadamu. Kwa njia ya mshikamano wa udugu wa kibinadamu, Jumuiya ya Kimataifa inao uwezo wa kujenga ulimwengu bora zaidi unaosimikwa katika haki msingi za binadamu, kwa kuwanyanyua na kuwaendeleza binadamu, ili kudumisha amani na usalama kwa watu wote. Itakumbukwa kwamba, Waraka wa Kitume wa Baba Mtakatifu Francisko "Fratelli tutti": Yaani “Wote ni Ndugu”: Kuhusu Udugu na Urafiki wa Kijamii” unachota amana na utajiri mkubwa kutoka katika Hati ya Udugu wa Kibinadamu kwa Ajili ya Amani na Utulivu uliotiwa saini kati ya Baba Mtakatifu Francisko na Dr. Ahmad Al-Tayyib, Imam Mkuu wa Msikiti wa Al- Azhar, ulioko mjini Kairo, nchini Misri, tarehe 4 Februari 2019 huko Abu Dhabi, Umoja wa Falme za Kiarabu. Rais Joseph Robinette Biden Jr. wa Marekani anawapongeza viongozi hawa wa kidini walioasisi mchakato wa udugu wa kibinadamu, unaoadhimishwa sasa na Jumuiya ya Kimataifa.

Mshikamano wa Kimataifa ni muhimu ili kukabiliana na changamoto mamboleo
Mshikamano wa Kimataifa ni muhimu ili kukabiliana na changamoto mamboleo

Kwa upande wake, Dr. Ahmad Al-Tayyib, Imam Mkuu wa Msikiti wa Al- Azhar, ulioko mjini Kairo, nchini Misri, katika ujumbe wake kwa njia ya video anakazia zaidi kuhusu: maridhiano, udugu wa kibinadamu, mshikamano na ushirikiano wa kidugu, ili kuweza kukabiliana na changamoto mamboleo zinazomwandama mwanadamu katika ulimwengu mamboleo. Lengo ni kutangaza na kushuhudia upendo kwa watoto yatima, wanaoishi katika mazingira magumu na hatarishi; maskini, wakimbizi, wahamiaji na watu wasiokuwa na makazi ya kudumu bila kuwasahau watu wanaoteseka kutokana na hali ngumu ya maisha kiuchumi, kijamii na kisiasa kutokana na uchu wa fedha, mali na madaraka. Dr. Ahmad Al-Tayyib, anawapongeza viongozi mbalimbali wa kidini ambao wamejipambanua katika mchakato wa ujenzi wa utamaduni wa udugu wa kibinadamu na amani, ili kuondokana na kinzani, migogoro na vita inayosababisha maafa makubwa kwa watu na mali zao. Ni wakati wa kushikamana ili kupambana kikamilifu na janga la Ugonjwa wa Virus vya Korona, UVIKO-19, ili kuwajengea watu wa Mungu matumaini mapya. Udugu wa kibinadamu usaidie kukomesha vita, kujenga na kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano. Jumuiya ya Kimataifa inahitaji ushirikiano na mshikamano wa udugu wa kibinadamu ili kujenga madaraja yanayowakutanisha watu ili kupambana na changamoto zinazotishia amani, usalama, ustawi na maendeleo ya wengi.

Udugu wa Kibinadamu unasimikwa katika majadiliano ya kidini, kiekumene na kitamaduni
Udugu wa Kibinadamu unasimikwa katika majadiliano ya kidini, kiekumene na kitamaduni

Hizi ni juhudi zilizotekelezwa kwa kushirikiana na Kamati Kuu ya Utekelezaji wa Hati ya Udugu wa Kibinadamu: Wajumbe wa Kamati hii ni pamoja na Kardinali Miguel Angel Ayuso Guixot, Rais wa Baraza la Kipapa la Majadiliano ya Kidini, Professa Mohamed Hussein Mahrasawi, Mkuu wa Chuo cha Al Azhar na Monsinyo Yoannis Lahzi Gaidi, Aliyekuwa Katibu muhtasi wa Baba Mtakatifu Francisko. Wengine katika kamati hii ni Jaji Mohamed Mahmoud Abdel Salaam, mshauri mkuu wa Mufti mkuu. Wajumbe wengine ni wale walioteuliwa kutoka Serikali ya Umoja wa Falme za Kiarabu, Baraza la Wazee wa Kiislam Umoja wa Falme za Kiarabu pamoja na watu maarufu katika tasnia ya habari Umoja wa Falme za Kiarabu.

Jumuiya ya Kimataifa
04 February 2022, 14:41