Kardinali Michael Czerny anawataka wafanyakazi wa Caritas Cambodia kupandikiza mbegu ya haki, amani na matumaini ili kuwashirikisha wengine furaha ya Injili. Kardinali Michael Czerny anawataka wafanyakazi wa Caritas Cambodia kupandikiza mbegu ya haki, amani na matumaini ili kuwashirikisha wengine furaha ya Injili. 

Mafungo ya Kiroho Kwa Caritas Cambodia: Haki, Amani na Matumaini

Kardinali Michael F. Czerny, S.J anakazia umuhimu wa kusia mbegu ya haki, amani na matumaini, kwa kuwashirikisha wengine furaha ya Injili. Ukuaji wa mbegu hii, usimikwe katika: furaha huruma na upendo. Wajitahidi kujenga na kupyaisha ulimwengu unaojikita katika haki na amani, daima wakitambua kwamba, wao ni mashuhuda na vyombo vya huruma na upendo wa Mungu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, maendeleo fungamani ni mchakato wa utekelezaji wa sera na mikakati ya maendeleo inayomgusa na kumwambata binadamu mzima, aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Maskini na “akina yakhe pangu pakavu tia mchuzi” wanapaswa kupewa upendeleo wa pekee, ili kuwaonjesha huruma na upendo unaobubujika kutoka kwa Mama Kanisa. Katika muktadha huu, Kanisa linataka kujipambanua kuwa ni mdau mkuu wa maendeleo fungamani ya binadamu, dhana inayokwenda kinyume kabisa na utandawazi usiojali wala kuguswa na mahangaiko ya wengine. Baba Mtakatifu anasikitika kusema kwamba, ubaguzi mbaya kabisa dhidi ya maskini ni ukosefu wa huduma za maisha ya kiroho.

Hii inatokana na ukweli kwamba, maskini mara nyingi ni wepesi sana kukumbatia zawadi ya imani na wanayo kiu ya kutaka kukutana na Mwenyezi Mungu katika maisha yao. Maskini waonjeshwe urafiki na Neno la Mungu; washirikishwe katika maadhimisho ya Sakramenti za Kanisa sanjari na safari ya kukua na kukomaa katika imani. Upendeleo kwa maskini unapaswa kutafsiriwa hasa kama huduma ya kiroho iliyo bora zaidi na inayopaswa kupewa kipaumbele cha pekee! Baba Mtakatifu anasema, ushirika ni kiini na tafsiri ya Kanisa linalopata chimbuko lake kwa kukutana na Kristo Yesu, Mwana wa Mungu, ambaye kwa njia ya kutangaza na kushuhudia Neno lake, linaweza kuwafikia watu wengi zaidi na hivyo kujenga ushirika katika Fumbo la Utatu Mtakatifu.

Ni wakati wa kupanda mbegu ya haki, amani na upatanisho
Ni wakati wa kupanda mbegu ya haki, amani na upatanisho

Ni katika muktadha huu, Kardinali Michael F. Czerny, S.J. Mwenyekiti wa muda wa Baraza la Kipapa la Huduma ya Maendeleo Endelevu na Fungamani ya Binadamu amewatumia ujumbe kwa njia ya video, wafanyakazi wa Shirika la Misaada la Kanisa Katoliki nchini Cambodia, Caritas Cambodia, wakati wa mafungo ya kiroho kuanzia tarehe 16-17 Februari 2022. Mafungo haya yananogeshwa na kauli mbiu “Kwa pamoja kukuza utamaduni wa kutunza na udugu wa kibinadamu. Katika ujumbe huu, Kardinali Michael F. Czerny, S.J anakazia umuhimu wa kusia mbegu ya haki, amani na matumaini, kwa kuwashirikisha wengine furaha ya Injili. Ukuaji wa mbegu hii, usimikwe katika: furaha ya kweli, huruma na upendo. Wajitahidi kujenga, kudumisha na kupyaisha ulimwengu unaojikita katika haki na amani, daima wakitambua kwamba, wao ni mashuhuda na vyombo vya huruma na upendo wa Mungu. Wasimame kidete kulinda na kudumisha utu, heshima na haki msingi za binadamu; bila kusahau mshikamano wa udugu wa kibinadamu, kiini cha Injili ya Kristo Yesu na ushirika wa familia kubwa ya binadamu, wito unaopaswa kutekelezwa na wote.

Cambodia

 

16 February 2022, 16:35