Monsinyo Simone Renna Katibu Mkuu Msaidizi Baraza La Wakleri
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Baba Mtakatifu Francisko amemteua Monsinyo Simone Renna, kuwa Katibu mkuu Msaidizi wa Baraza la Kipapa la Wakleri. Hadi kuteuliwa kwake, Monsinyo Simone Renna alikuwa ni Afisa mwanadamizi katika Baraza la Kipapa la Wakleri. Itakumbukwa kwamba, Monsinyo Simone Renna anachukua nafasi ya Monsinyo Andrea Ripa aliyeteuliwa hivi karibuni na Baba Mtakatifu Francisko kuwa Katibu mkuu wa Mahakama Kuu ya Kitume “Segnatura Apostolica” na kumpandisha hadhi na kuwa Askofu. Monsinyo Simone Renna, Katibu mkuu Msaidizi wa Baraza la Kipapa la Wakleri alizaliwa tarehe 10 Julai 1974 Jimbo kuu la Lecce, Kusini mwa Italia.
Baada ya masomo na majiundo yake ya Kikasisi, tarehe 29 Juni 2004 akapewa Daraja Takatifu ya Upadre. Baadaye, alijiendeleza katika masomo ya juu kuhusu “Sheria na Taratibu za Uendeshaji wa Kesi Mahakamani” “Giurisprudenza katika Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha “Sacro Cuore” Milano na hatimaye, akajipatia Shahada ya Uzamivu katika Sheria za Kanisa kutoka Chuo Kikuu cha Kipapa cha Lateran. Katika maisha na utume wake kama Padre, amewahi kuwa: Paroko, Mkurugenzi wa Idara ya Utume kwa Vijana pamoja na Idara Kichungaji Chuo Kikuu, Hakimu wa Mahakama ya Kikanisa na Chancellor. Kuanzia tarehe 1 Oktoba 2019 aliteuliwa kuwa Ofisa Mwandamizi Baraza la Kipapa la Wakleri na tarehe 9 Februari 2022 Baba Mtakatifu Francisko akamteuwa kuwa Katibu mkuu msaidizi Baraza la Kipapa la Wakleri.