Viongozi wa Makanisa sehemu mbalimbali za dunia wanalaani vikali vitisho vya Urussi kutaka kuivamia Ukraine. Viongozi wa Makanisa sehemu mbalimbali za dunia wanalaani vikali vitisho vya Urussi kutaka kuivamia Ukraine. 

Mshikamano wa Makanisa Dhidi ya Uvamizi wa Ukraine

Askofu mkuu Sviatoslav Shevchuk, anamshukuru na kumpongeza Papa Francisko kwa kuiombea Ukraine. Ni matumaini ya watu wa Mungu kutoka sehemu mbalimbali za dunia kwamba majadiliano katika ukweli sanjari jitihada za kidiplomasia, amani itaweza kutawala tena nchini Ukraine na hivyo kuvuka mgogoro huu unaweza kugeuka na kuwa ni Vita Kuu ya Tatu ya Dunia.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Jitihada za kidiplomasia kati ya viongozi wakuu wa Nchi za Umoja wa Ulaya, Marekani na Urussi zimekuwa zikiendelea lakini bila mafanikio. Wananchi wengi wana hofu kuhusu usalama wa maisha yao. Viongozi wa Makanisa nao wamekuwa mstari wa mbele ili kuhakikisha kwamba, Vita ya maneno inakoma na majadiliano ya diplomasia yanachukua mkondo wake, vita inakoma, haki, amani na utulivu vinatawala tena. Watu wakumbuke kwamba, vita haina pazia na majanga yake ni makubwa. Ni katika muktadha huu, Askofu mkuu Sviatoslav Shevchuk, Mkuu wa Kanisa Katoliki la Kigiriki nchini Ukraine, Jumatatu tarehe 14 Februari 2022 amezungumza kwa njia ya simu na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican, akimpongeza na kumshukuru Baba Mtakatifu Francisko, Vatican pamoja na Kanisa zima kwa kuonesha mshikamano wa upendo wa udugu wa kibinadamu kwa familia ya Mungu nchini Ukraine.

Diplomasia ya amani inahitajika kuepusha vita
Diplomasia ya amani inahitajika kuepusha vita

Hiki ni kipindi kigumu sana chenye changamoto nyingi, zinazofumbatwa katika hofu na wasi wasi wa Ukraine kuweza kuvamiwa kijeshi na Urussi. Katika kipindi hiki kigumu cha maisha na historia ya Kanisa Katoliki la Kigiriki nchini Ukraine, bado linaendelea kujizatiti katika huduma kwa watu wa Mungu. Askofu mkuu Sviatoslav Shevchuk, Mkuu wa Kanisa Katoliki la Kigiriki nchini Ukraine, anamshukuru na kumpongeza Baba Mtakatifu Francisko kwa kusali na kuiombea Ukraine. Ni matumaini ya watu wa Mungu kutoka sehemu mbalimbali za dunia kwamba majadiliano katika ukweli na uwazi sanjari jitihada za kidiplomasia, amani itaweza kutawala tena nchini Ukraine na hivyo kuvuka mgogoro huu unaweza kugeuka na kuwa ni Vita Kuu ya Tatu ya Dunia. Kwa upande wake, Kardinali Pietro Parolin, amewahakikishia watu wa Mungu nchini Ukraine mshikamano wa udugu wa kibinadamu na sala kwa wote.

Wakati huo huo, Baraza la Maaskofu Katoliki Poland, linawaalika viongozi wa Makanisa nchini Urussi na Ukraine kuunganisha nguvu zao za sala, ili kumlilia Mwenyezi Mungu aweze kuepusha janga la uvamizi wa kijeshi nchini Ukraine, ambalo linaweza kusababisha maafa makubwa kwa watu na mali zao. Vita ni chanzo kikuu cha mateso na mahangaiko ya watu wasiokuwa na hatia. Kumbe, kuna haja ya kuheshimu sheria za Kimataifa na uhuru wa wananchi wa Ukraine kujiamria mambo yao yenyewe. Kimsingi vita inadhalilisha utu, heshima na haki msingi za binadamu sanjari na kukoleza chuki na uhasama kati ya watu wa Mataifa. Kamwe vita si suluhu ya matatizo na changamoto zinazoyaandama Mataifa.

Amani ya kweli inasimikwa katika utu, heshima na haki msingi za binadamu
Amani ya kweli inasimikwa katika utu, heshima na haki msingi za binadamu

Kwa upande wake, Baraza la Maaskofu Katoliki Italia, CEI, linawaalika viongozi wakuu wa pande zote zinazohusika na mgogoro wa uvamizi wa kijeshi wa Urussi nchini Ukraine, kujikita katika mchakato wa majadiliano katika ukweli na uwazi, ili kulinda: utu, heshima, haki msingi za binadamu, amani na utulivu. Vitisho vya uvamizi wa kijeshi, vinatia kichefuchefu, vinasumbua dhamiri na utulivu wa watu na hivyo kuongeza hofu na mashaka pamoja na hali ngumu. Watu wengi wanateseka kutokana na maambukizi makubwa ya Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19. Si busara kufumua vita tena kwa nyakati hizi. Katika ulimwengu mamboleo, hakuna tena nafasi ya vita katika historia ya mwanadamu. Jambo la msingi ni kunogesha majadiliano, ushirikiano na mafungamano ya kiuchumi, kijamii na kiutu!

Uvamizi Ukraine

 

 

15 February 2022, 14:50