Pete ya kiaskofu Pete ya kiaskofu 

Papa amemteua Padre Sakor Eyobo kuwa Askofu Mpya,jimbo la Yei

Papa Francisko amemteua Padre Alex Lodiong Sakor Eyobo,kuwa askofu wa Jimbo katoliki la Yei nchini Sudan Kusini.Alizaliwa mnamo tarehe 26 Januari 1971 huko Wudu jimbo katoliki la Yei na tarehe Juni 24,2001 apewa daraja la Upadre.

Na Angella Rwezaula – Vatican.

Ijumaa tarehe 11 Februari 2022 Baba Mtakatifu ameridhia kung’atuka katika shughuli za kichungaji la Jimbo la Yei nchini Sud Kusini kwa Askofu Erkolano Lodu Tombe, na wakati huo huo akamteua askofu wa Jimbo hilo hilo Msh. Padre Alex Lodiong Sakor Eyobo, ambaye hadi uteuzi alikuwa ni Mwalimu na Mweka Hazina wa Seminari Kuu ya Kitaifa ya Mtakatifu Paulo mjini Juba.

Padre Alex Lodiong Sakor Eyobo, alizaliwa tarehe 26 Januari 1971, huko  Wudu jimbo katoliki la Yei, Sudan Kusini.  Alijiunga na Seminari ndogo ya Mtakatifu Maria huko Juba (1989-1993) na kuendelea na Seminari Kuu ya Kitaifa ya Mtakatifu Paulo kwa mafunzo ya Falsafa na Taalimumungu na kupata diploma (1996) na Shahada ya Uzamili (2000). Tarehe 24 Juni 2001 alipewa daraja la Upadre Jimbo la Yei.

Baada ya kupewa daraja la upadre alitekeleza majukumu yafuatayo: Padre wa  Parokia ya Moyo Mtakatifu, Lomin-Kajo Keji (2001-2002); Diploma ya sayansi ya kompyuta katika Chuo Kikuu katoliki cha Afrika Mashariki, Nairobi, Kenya (2002-2003); Katibu Mkuu wa Jimbo la Yei (2002-2006); Masomo ya Usimamizi na Utawala wa Fedha (CORAT) Africa, Nairobi, Kenya (2006-2007); Katibu Mkuu, Mweka Hazina wa Jimbo, Mratibu wa Mawasiliano na Elimu (2006-2008); Msimamizi waVijana  Jimboni (2008-2013); Gambera wa Seminari Ndogo ya Jimbo la Mtakatifu Agostino huko Yei (2013-2014); Alihitimu katika Taalimungu ya Biblia katika Chuo Kikuu cha Kipapa cha Urbaniana, Roma (2014-2018).

11 February 2022, 16:27