Vipaumbele vya Serikali ya Zambia: Elimu, Umoja na Mapambano Dhidi ya Rushwa
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Elimu maana yake ni mchakato unaowajengea wanafunzi matumaini ya kuondokana na ubinafsi wao; kwa kutambua, kuheshimu na kuthamini tofauti msingi zinazojitokeza, ili hatimaye kujenga na kudumisha: utamaduni wa ukarimu, mshikamano, mafungamano na hofu ya Mungu. Upyaisho wa mfumo wa elimu katika ulimwengu mamboleo utawasaidia watu wa Mungu kupambana na changamoto zinazojitokeza kwa wakati huu, ili kujenga leo na kesho yenye matumaini. Elimu ni upendo unaowajibisha na kurithishwa kutoka kizazi kimoja hadi kingine, ili kuondokana na ubinafsi unaopelekea watu kutokuthaminiana. Kuna haja ya kujenga umoja na mshikamano unaosimikwa katika kipaji cha kusikiliza, kujadiliana na maelewano. Mabadiliko ya mfumo wa elimu duniani yanapaswa kuwahusisha wadau mbali mbali katika sekta ya elimu, ili kuondokana na ukosefu wa haki jamii; kwa kukazia utu, heshima na haki msingi za binadamu, ili hatimaye, kuweza kupambana na umaskini pamoja na tabia ya watu kutowajali wengine. Baba Mtakatifu Francisko anasema, huu ni mchakato fungamanishi unaopania kujenga madaraja yanayowakutanisha watu, ili kuondokana na upweke hasi, kwa kuwajengea vijana wa kizazi kipya matumaini. Hali hii itawasaidia vijana wengi kuondokana na ugonjwa wa sonona; utumwa mamboleo, chuki, uhasama, matusi, ukatili pamoja na uonevu na unyanyasaji mitandaoni.
Rais Hakainde Hichilema wa Zambia, Jumamosi tarehe 19 Februari 2022 amekutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko pamoja na viongozi waandamizi mjini Vatican. Baadaye alifanya mahojiano maalum na Vatican News kwa kuishukuru Vatican kwa mchango wake kwa watu wa Mungu Barani Afrika, Elimu kwa wote kama kipaumbele cha Serikali yake, Umoja wa Kitaifa sanjari na mapambano dhidi ya rushwa na ufisadi wa mali ya umma, saratani inayomeng’enya utu, heshima na haki msingi za binadamu! Rais Hakainde Hichilema amemshukuru na kumpongeza Baba Mtakatifu Francisko kwa mchango wake katika ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu Barani Afrika, lakini kwa namna kwa namna ya pekee kabisa Zambia. Uhuru wa kidini na uhuru wa kuabudu ni kati ya mambo ambayo ameshirikishana na Baba Mtakatifu Francisko katika mazungumzo yao ya faragha. Lengo ni kuhakikisha kwamba, dini zote nchini Zambia zinasaidia mchakato wa ustawi, maendeleo na mafao ya wengi: kiroho na kimwili.
Rais Hakainde Hichilema amemwelezea Baba Mtakatifu kwamba, yeye ni kati ya watu waliofaidika na mfumo wa elimu bure uliokuwa unatolewa nchini Zambia enzi zake na kwamba, kwa sasa Serikali yake inajielekeza zaidi katika mfumo wa elimu bure, ili kutoa nafasi hata kwa “watoto wa wakulima” kuweza kuboresha maisha yao kwani elimu ni ufunguo wa maisha. Serikali imeanza kutoa elimu ya bure kuanzia shule ya msingi hadi sekondari na kwamba, kwa siku za usoni, hata elimu ya taasisi za elimu ya juu na vyuo vikuu itakuwa inatolewa bure. Elimu bora na makini kwa wananchi wa Zambia itasaidia kukoleza mchakato wa ustawi, maendeleo na mafao ya wengi kwa kuboresha kilimo na uchumi katika ujumla wake. Rais Hakainde Hichilema amesema, Serikali yake inaendelea kujielekeza katika mchakato wa ujenzi wa umoja, mshikamano na mafungamano ya kitaifa. Zambia imebahatika kuwa na makabila 72 yenye historia, asili na lugha zao. Wote hawa wanapaswa kuunganishwa ili kujenga na kuimarisha umoja wa kitaifa. Baba Mtakatifu Francisko katika Ujumbe wa Siku ya 52 ya Kuombea Amani Duniani kwa Mwaka 2019 anasema: Amani ni sawa na matumaini yanayosongwa na changamoto pamoja na magumu yanayowaandama walimwengu.
Yote haya ni matokeo ya: Uchu wa mali, madaraka na utajiri wa haraka haraka na matokeo yake ni matumizi mabaya ya madaraka na uvunjwaji wa haki msingi za binadamu. Siasa safi inafumbatwa katika unyenyekevu, kielelezo makini cha huduma katika ngazi mbalimbali za maisha ya binadamu. Lengo ni kukuza na kudumisha dhamana, utu, heshima na tunu msingi za maisha zinazoiwezesha jamii kutekeleza mafao ya wengi. Kumbe, utekelezaji makini wa siasa safi ni changamoto endelevu kwa viongozi wanaopewa dhamana ya kuongoza, kwani wanapaswa kuwalinda raia wao; kwa kushirikiana kikamilifu ili kuboresha maisha ya wananchi wao katika misingi ya haki, uhuru, utu na heshima ya binadamu na kwa njia hii, siasa safi inakuwa ni chombo cha upendo! Baba Mtakatifu anakaza kusema, upendo na fadhila za kiutu ziwe ni kwa ajili ya siasa safi inayohudumia haki msingi na amani, kila mtu akijitahidi kujikita katika mafao ya wengi, kama sehemu ya ujenzi wa mji wa Mungu hapa duniani, ili kuendeleza historia ya maisha ya familia ya binadamu. Haki na usawa; tabia ya kuheshimiana na kuthaminiana kama binadamu inapaswa kudumishwa.
Ukweli, uwazi na uaminifu ni tunu msingi zinazoboresha siasa safi na kwamba, mwanasiasa bora ni yule anayetambua dhamana na wajibu wake kwa jamii. Ni kiongozi anayeaminika na kuthaminiwa na jamii na kwamba anajitaabisha kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Ni mwaminifu katika ahadi zake kwa wananchi waliomchagua, daima akijitahidi kujenga na kudumisha umoja na mshikamano, tayari kuchochea mageuzi katika maisha ya watu; kwa kuwasikiliza na kutenda kwa ujasiri! Baba Mtakatifu anasema, hivi ni vigezo muhimu sana wakati wa kufanya chaguzi mbalimbali, ili kuhakikisha kwamba, haki, dhamana na wajibu vinatekelezwa kikamilifu. Kwa upande wake Rais Hakainde Hichilema wa Zambia anapenda kuhakikisha kwamba, Zambia linakuwa Taifa moja na watu wamoja. Aliwahi kusema kwamba, huu ni wakati wa kujenga na kuimarisha umoja, upendo na mshikamano pamoja na msamaha, kwa kujielekeza katika utawala bora unaozingatia na kuheshimu sheria, taratibu na kanuni msingi za Zambia.Vita ya kiuchumi inahitaji umoja na mshikamano wa kitaifa, ili kunogesha kasi ya ukuaji wa uchumi pamoja na kutengeneza fursa za ajira kwa vijana wa kizazi kipya.
Rushwa, ufisadi na ubadhirifu wa mali ya umma ni vitendo ambavyo vimeacha madonda makubwa katika maisha ya kijamii na vinaendelea kumong’onyoa misingi bora ya uchumi; kanuni maadili na utu wema. Rushwa na ufisadi wa mali ya umma ni vitendo vinavyowajengea watu ombwe la kutaka kupata utajiri wa mali na fedha kwa njia ya mkato, lakini madhara yake ni makubwa kwa watu wengi zaidi. Ni vitendo ambavyo vinaendelea kumong’onyoa taratibu hali ya watu kuaminiana, umuhimu wa utekelezaji wa utawala bora unaozingatia kanuni, sheria na taratibu za nchi. Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Francisko anasema, rushwa na ufisadi ni mambo ambayo yanapekenyua: utu, heshima na haki msingi za binadamu. Jamii inapaswa kusimama kidete kupambana na saratani ya rushwa na ufisadi katika mifumo yake mbalimbali. Mwelekeo wa wananchi kutokuwa na imani na Serikali zao, ni chanzo cha kudhohofisha mchakato wa ujenzi wa demokrasia. Ustawi, mafao na maendeleo ya wengi ni mambo msingi yanayopaswa kulindwa na kusimamiwa. Katika hali na mazingira kama haya, Serikali zinapaswa kutekeleza vyema dhamana na wajibu wake mkamilifu kwa kuhakikisha kwamba, utawala bora na unaozingatia sheria za nchi unafuatwa na wote. Rais Hakainde Hichilema wa Zambia anasema rushwa ni hatari sana kwa ustawi, maendeleo na mafao ya wengi kwani inawapoka watu wa Mungu rasilimali na utajiri ambao ungeweza kutumika katika maboresho ya sekta mbalimbali za maisha ya watu wa Mungu nchini Zambia. Uongozi ni huduma na wala si kichaka cha kutafuta mali na utajiri wa haraka haraka.