Watanzania Italia Waadhimisha Misa Kuombea Haki Na Amani Duniani
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Askofu mkuu Protase Rugambwa, Katibu wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa watu, Dominika tarehe 27 Februari 2022 ameongoza Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya kuombea amani ndani na nje ya Tanzania. Ibada hii imeadhimishwa kwenye Parokia ya “Corpo e Sangue Di Cristo” Jimbo kuu la Roma. Watanzania wamemwomba Mwenyezi Mungu kuwaangalia watanzania wanaohesabika kati ya Mataifa ya dunia, awajalie kuishi maisha mema kadiri inavyowastahili wana wa Mungu. Awaangaze viongozi wa Tanzania watu sheria zitakazowafaidia kwa mambo mema hapa duniani, zilingane na Sheria za Mungu aliyeuwaumba kwa ajili yake. Awakirimie watu wote paji la imani kwa kutambua uwepo wake endelevu, awaimarishe ili waweze kupambana na maovu yanayoweza kuwafikia kutoka ndani au nje ya nchi. Mwenyezi Mungu awakirimie hekima ya kutafuta ukweli katika mambo yote, na kuishi kwa uaminifu katika Amri za Mungu.
Mwenyezi Mungu apende kuwasha moto wa mapendo kati ya watanzania, ili kushinda utengano, ushindani usiokuwa na tija wala mashiko, chuki ya ukabila au utaifa. Mwenyezi Mungu Aawaunganishe watanzania wote ili wawe ndugu wamoja katika unaobubujika kutoka katika Fumbo la Utatu Mtakatifu. Ameomba baraka ya Mwenyezi Mungu, ili Tanzania iweze kustawi na kuishi na amani na mataifa mengine jirani. Awaongoze viongozi wa Tanzania kutimiza wajibu wa kazi zao kadiri inavyostahili. Wawasaidie raia wao kuboresha maisha yao hapo walipo. Awajalie watanzania kufikia ukomo aliowatayarishia Mwenyezi Mungu, yaani kuwa raia wa Ufalme wa Mbinguni, anapoishi na kutawala milele na milele. Mungu Baba Ibariki Nchi Yetu.
Ibada hii ya Misa Takatifu iliandaliwa na Umoja wa Watanzania Wakatoliki Italia pamoja na mambo mengine, ilikuwa ni kwa ajili ya kuombea Amani nchini Tanzania na kuhudhuriwa na Balozi Mahmoud Thabit Kombo, Balozi wa Tanzania nchini Italia pamoja na ujumbe wake. Askofu mkuu Protase Rugambwa katika mahubiri yake, Dominika ya VIII ya Kipindi cha mwaka C wa Kanisa, amemshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuwawezesha tena watanzania na watu wenye mapenzi mema kukutana na kumshukuru baada ya kukabiliana na changamoto za kiafya zilizosababishwa na maambukizi makubwa ya Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19. Askofu mkuu Protase Rugambwa pamoja na mambo mengine amekazia mafundisho ya Kristo Yesu kuhusu: Heri kama dira na mwongozo wa maisha adili na matakatifu. Amekumbushukia kuhusu fadhila ya upendo inayosimikwa katika huruma na msamaha, kiasi hata cha kuthubutu kuwasamehe adui zao, upya wa mafundisho ya Kristo Yesu kwa wafuasi wake wote.
Askofu mkuu Protase Rugambwa, amewataka watu wa Mungu nchini Tanzania watambue kwamba, wema na utakatifu wa maisha unapata chimbuko lake kutoka kwa Kristo Yesu, Mwalimu wa ukamilifu wote na elimu makini inayowasaidia kuwa waaminifu tayari kuchuchumilia toba, wongofu na ukamilifu wa maisha. Waambate elimu makini kutoka kwa Kristo itakayowasaidia kutokana na upofu, kwa kuchota fadhila kutoka katika hazina ya nyoyo zao. Kama miti, daima watambulikane kwa matunda adili na utakatifu wa maisha, mambo yanayohitaji toba na wongofu wa ndani. Kumbe, busara, hekima, uadilifu na utakatifu wa maisha yapate chimbuko lake kutoka katika undani wa maisha ya mwamini, tayari kujitosa bila ya kujibakiza kwa ajili ya kujenga Kanisa, jumuiya na jamii inayowazunguka, ili isimikwe katika furaha, umoja, udugu wa kibinadamu, amani, upendo na mshikamano, changamoto pevu katika ulimwengu mamboleo. Katika Ibada hii ya Misa Takatifu imekuwa pia ni fursa ya kuombea haki, amani na maridhiano sehemu mbalimbali za dunia lakini zaidi huko DRC, Afghanistan na Ukraine ambako kwa sasa moto wa vita unawaka na athari zake zimeanza kuonekana, kwa watu wasiokuwa na hatia.