Tafuta

Caritas Poland Caritas Poland 

Caritas Internationalis:Ukraine iko katika hatari ya janga la kibinadamu!

Shirikisho la upendo la Caritas Internationalis,lililoundwa mnamo 1951 ili kuhakikisha ulinzi na hupatikanaji wa msaada wa kibinadamu,linasisitiza na kuomba kuwepo na uhuru wa kuzunguka na kuhakikishwa wale ambao wanakimbia vita nchini Ukraine."Hatuwezi kupuuza athari mbaya za kibinadamu za vita hivi,”Katibu Mkuu wa Caritas Internationalis Aloysius John,alisema.

Na Angella Rwezaula – Vatican.

Matukio yaliyoanza mapema asubuhi ya alhamisi 24 Februari 2022  bila shaka yatasababisha janga kubwa la kibinadamu. Haiwezekani kuamini kuwa katika karne ya 21, katikati ya Ulaya, watu wanapaswa kuamka saa 11 alfajiri kwa milipuko na sauti za ving'ora vya uvamizi wa anga. Haya ni maneno ya Tetiana Stawnychy, rais wa Caritas Ukraine, baada ya shambulio hilo kubwa lililofanyika alfajiri ya kuamkia alhamisi 24 Februari, nchini humo. Caritas Internationalis ilionesha wasiwasi wake kwa idadi ya watu wa Ukraine katika taarifa, ambayo tayari iko katika hali mbaya miaka minane baada ya kuanza kwa mzozo ambao ulisababisha vifo vya zaidi ya 14,000 na watu wengine milioni 1.5 kuhama makazi yao.

Caritas Intenationalis yazindua Wito wa kusaidia kazi ya Caritas Ukraine

Shirikisho la Caritas limezindua wito wa dharura ili kusaidia kazi ya Caritas Ukraine. Mpango huo unalenga kusaidia walioathirika na mgogoro huo kwa chakula, maji safi, makazi salama na vifaa vya usafi, pamoja na kuhakikisha usafiri wa uhakika kwa watu wanaoishi katika mazingira magumu ili kuwafikia wapendwa wao na maeneo salama. “Tunahitaji msaada wako ili kuweza kukabiliana na mzozo wa kibinadamu na kusaidia watu walioathiriwa na vita.” Tayari tangu mwisho wa msimu wa joto wa 2021, hasa mashariki mwa Ukraine, Caritas imetayarisha jibu la kibinadamu kwa uwezekano wa kuongezeka kwa mzozo huo ili kuimarisha mtandao wake na kuongeza uwezo wake pamoja na kutoa mafunzo kwa wafanyikazi na watu wa kujitolea. Kwa kuongezea, vituo vimewekwa tayari kwa muda ili kuchukua na kuhakikisha usaidizi kwa wakimbizi wa ndani, idadi ambayo itaongezeka sana kufuatia kuanza kwa uingiliaji wa kijeshi. Idadi za dharura tayari ni za kushangaza kwani kabla ya shambulio la pande zote mbili  tayari kulikuwa na watu milioni 2.9 waliokuwa wakihitaji msaada wa kibinadamu. Sasa idadi hii itaongezeka zaidi.

Kila mmoja anaitwa kuchuka hatua

Caritas Ukraine inaungwa mkono na mashirika 36 ya Shirikisho la Caritas katika kusaidia watu wenye kuhitaji. “Hatuwezi kupuuza athari mbaya za kibinadamu za vita hivi,” Katibu Mkuu wa Caritas Internationalis Aloysius John alisema. Ni wajibu wa jumuiya ya kimataifa kuwalinda watu wa Ukraine na kuhakikisha kwamba wanapata usaidizi wa kibinadamu.” Caritas Internationalis inasisitiza haja ya watu wote, hawa walio hatarini zaidi, kupata msaada wa kibinadamu na uhuru wa kutembea kuhakikishwa kwa wale wanaokimbia mzozo. “Sote tumeitwa kuchukua hatua. Kinachotokea Ukraine kinahatarisha utulivu na amani ya kimataifa na kama Baba Mtakatifu alivyosisitiza, ni kudharau sheria za kimataifa. Kwa yeyote anayetaka kuunga mkono kazi ya Caritas Ukraine anaweza kufanya hivyo kupitia tovuti hii: questo sito internet.

25 February 2022, 16:42