Bw. Eduard Heger, Waziri Mkuu wa Slovakia Akutana na Papa Francisko
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Baba Mtakatifu Francisko, Jumatatu tarehe 14 Machi 2022 amekutana na kuzungumza na Bwana Eduard Heger, Waziri mkuu wa Slovakia na baadaye, alibahatika pia kukutana na kuzungumza na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican aliyekuwa ameambatana na Askofu mkuu Paul Richard Gallagher, Katibu mkuu wa mambo ya nchi za nje na ushirikiano wa Kimataifa mjini Vatican. Itakumbukwa kwamba Hija ya Kitume ya Baba Mtakatifu Francisko nchini Slovakia kuanzia tarehe 12 hadi tarehe 15 Septemba 2021 ilinogeshwa na kauli mbiu “Pamoja na Bikira Maria na Mtakatifu Yosefu Njia ya Kwenda kwa Yesu.”
Viongozi hawa wawili katika mazungumzo yao, wamekumbushia hija hii ya Kitume iliyopata mafanikio makubwa. Kwa pamoja wameridhika na uhusiano wa kidiplomasia uliopo kati ya nchi hizi mbili sanjari na mchango wa Kanisa katika ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu nchini Slovakia. Baba Mtakatifu pamoja na Waziri mkuu Eduard Heger, wakati wa mazungumzo yao ya faragha, wamegusia pia kuhusu vita inayoendelea nchini Ukraine na madhara yake kitaifa na kimataifa mintarafu hali ya wananchi wa Ukraine pamoja na huduma zinazotolewa kwa wakimbizi wa vita kutoka nchini Ukraine.