Kumbe, kauli mbiu inayonogesha tafakari za kipindi cha Kwaresima kwa Mwaka 2022 ni: “Twaeni mle; huu ni mwili wangu.” Kumbe, kauli mbiu inayonogesha tafakari za kipindi cha Kwaresima kwa Mwaka 2022 ni: “Twaeni mle; huu ni mwili wangu.”  

Tafakari za Kipindi cha Kwaresima 2022: Katekesi Kuhusu Ekaristi

Katika Kipindi cha Kwaresima, kila Ijumaa, kuanzia tarehe 11, 18, 25 Machi pamoja na tarehe 1 na 8 Aprili 2022 kutakuwa na Tafakari za Kipindi cha Kwaresima kuhusu Fumbo la Ekaristi Takatifu. “Walipokuwa wanakula, Yesu akatwaa mkate, akamshukuru Mungu, akaumega, akawapa wanafunzi wake akisema, “Twaeni mle; huu ni mwili wangu.” Lengo ni kupyaisha Katekesi kuhusu Ekaristi.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mababa wa Kanisa wanathibitisha kwamba, kwa nguvu ya imani ya Kanisa na uwezo wa Neno la Kristo Yesu, na tendo la Roho Mtakatifu, kwamba, mageuzo ya Mkate na Divai yanakuwa ni Mwili na Damu Azizi ya Kristo, yaani Ekaristi Takatifu. Kumbe, Ekaristi Takatifu ni Sakramenti na shule ya Upendo; ni zawadi na sadaka ya Kristo Yesu Msalabani. Ni kielelezo cha huduma inayomwilishwa na kuwasha mapendo kwa Mungu na jirani. Ekaristi Takatifu ni chachu ya kukuza na kudumisha umoja, mshikamano na udugu wa kibinadamu kati ya waamini, kwa kuwa na jicho la upendo kwa maskini na wale wote wanaoteseka kutokana na sababu mbalimbali za maisha. Ekaristi Takatifu ni chachu makini ya Injili ya familia inayokumbatia Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo unaofumbatwa katika sera za utoaji mimba na kifo laini. Ekaristi Takatifu, inalisukuma Kanisa kutembea bega kwa bega na vijana wa kizazi kipya kwa njia ya utume kwa vijana, lakini zaidi kwa njia ya ushuhuda wenye mvuto na mashiko kama sehemu ya ujenzi wa Kanisa la Kisinodi linalosimikwa katika: Umoja, Ushiriki na Utume.

Baba Mtakatifu Francisko anawaalika waamini kujenga na kudumisha utamaduni wa kuhudhuria na kushiriki kikamilifu katika Ibada ya Misa takatifu; Ibada ya Kuabudu Ekaristi Takatifu na hatimaye, kushiriki kikamilifu kwa ibada na heshima kuu wakati wa maandamano ya Ekaristi Takatifu, kielelezo makini cha uwepo endelevu na angavu wa Kristo Yesu, katika maisha ya waja wake. Huyu ni Kristo Yesu anayeandamana na wafuasi wake, bega kwa bega na hatua kwa hatua. Waamini waoneshe moyo wa upendo kwa kushikamana na Kristo katika safari ya maisha yao, kwa kujiandaa kikamilifu, ili kuweza kumpokea! Ekaristi Takatifu inawakirimia waamini chakula cha uzima wa milele na upendo unaobubujika kutoka kwa Kristo Yesu, ili hatimaye, kuweza kushiriki katika maisha, uzima na utukufu wa Baba wa milele! Ekaristi Takatifu inajenga fumbo la Mwili wa Kristo, yaani Kanisa.

Ekaristi Takatifu ni chanzo na kilele cha maisha na utume wa Kanisa
Ekaristi Takatifu ni chanzo na kilele cha maisha na utume wa Kanisa

Ekaristi Takatifu ni Sakramenti ya Mwili na Damu yake Azizi inayotolewa kwa ajili ya kurutubisha maisha ya walimwengu. Kwa kumpokea Yesu kwa imani, mwamini anakuwa sawa na Yesu na hivyo kufanyika kuwa mwana katika Mwana. Kwa njia ya Ekaristi Takatifu, Kristo Yesu anaandamana na wafuasi wake kama ilivyokuwa kwa wale Wafuasi wa Emau! Kristo Yesu anasafiri na waja wake katika historia ili kuwakirimia imani, matumaini na mapendo; kwa kuwafariji wakati wa majaribu na magumu ya maisha; na hatimaye, kuwaunga mkono katika mchakato wa mapambano ya kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu. Fumbo la Ekaristi Takatifu ni kiini na kilele cha maisha na utume wa Kanisa; ni chemchemi ya utakatifu wa maisha ya waamini, kumbe linapaswa lisadikiwe kwa dhati, liadhimishwe kwa ibada na uchaji na limwilishwe kikamilifu katika maisha na utume wa Kanisa. Baba Mtakatifu Francisko anasema, kila Mwaka Mama Kanisa anayofuraha kubwa ya kusherehekea na kushuhudia Fumbo la Ekaristi Takatifu, chanzo na kilele cha maisha na utume wa Kanisa kwa maandamano makubwa, ushuhuda kwamba, Kristo Yesu anaendelea kuandamana na waja wake katika historia ya maisha yao ya kila siku hadi utimilifu wa dahali.

Ekaristi Takatifu ni Sakramenti ya Umoja, inayowaunganisha waamini kuwa ni mwili mmoja na watu watakatifu wa Mungu. Mwamini anayepokea Ekaristi takatifu anakuwa ni chombo cha umoja, kwani ndani mwake kunaibuka “vinasaba ya maisha ya kiroho” vinavyosaidia kujenga umoja. Mkate wa Umoja unasaidia kuvunjilia mbali tabia ya kujiona kuwa ni bora zaidi kuliko wengine; watu wanaopenda kuwagawa wengine kwa mafao binafsi; watu wenye wivu na umbea unaohatarisha umoja na mshikamano. Waamini kwa njia ya kuliishi kikamilifu Fumbo la Ekaristi Takatifu: wana mwabudu na kumshukuru Kristo Yesu, kwa zawadi hii kubwa; kumbu kumbu hai ya upendo wake unaowaunganisha wote kuwa ni mwili mmoja na kuwaelekeza katika ujenzi wa umoja.

Katika Kipindi cha Kwaresima, kila Ijumaa, kuanzia tarehe 11, 18, 25 Machi pamoja na tarehe 1 na 8 Aprili 2022 kutakuwa na Tafakari za Kipindi cha Kwaresima kuhusu Fumbo la Ekaristi Takatifu. “Walipokuwa wanakula, Yesu akatwaa mkate, akamshukuru Mungu, akaumega, akawapa wanafunzi wake akisema, “Twaeni mle; huu ni mwili wangu.” Kisha akatwaa kikombe cha divai, akashukuru, akawapa akisema, “Kunyweni nyote; maana hii ni damu yangu inayothibitisha agano, damu inayomwagwa kwa ajili ya watu wengi ili kuwaondolea dhambi.” Mt 26: 26-28. Kumbe, kauli mbiu inayonogesha tafakari hizi ni: “Twaeni mle; huu ni mwili wangu.” Hizi ni tafakari zinazotolewa kwa uwepo wa: Baba Mtakatifu Francisko, Makardinali, Maaskofu, wasaidizi wake wa karibu, yaani “Curia Roma”, Wakuu wa Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume, Magambera pamoja na wafanyakazi wa Jimbo kuu la Roma.

Tafakari hizi zinatolewa na Kardinali Raniero Cantalamessa, Mhubiri wa Nyumba ya Kipapa na Ijumaa tarehe 11 Machi 2022 anajikita zaidi katika Liturujia ya Neno la Mungu katika Ibada ya Misa Takatifu. Kardinali Cantalamessa anasikitika kusema, kati ya madhara makubwa yaliyosababishwa na maambukizi makubwa ya Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19 ni pamoja na utupu uliojitokeza kuhusu ushiriki mkamilifu katika maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu chanzo na kilele cha maisha na utume wa Kanisa. Ni katika muktadha huu, baadhi ya Majimbo na Makanisa mahalia yameamua kujizatiti kikamilifu katika Katekesi kuhusu Fumbo la Ekaristi Takatifu, ili kupyaisha hamu ya ushiriki mkalimifu wa Fumbo hili Takatifu katika maisha na utume wa Kanisa.

Kauli mbiu: Twaeni mle, huu ni mwili wangu.
Kauli mbiu: Twaeni mle, huu ni mwili wangu.

Ekaristi Takiatifu ni kiini cha maadhimisho ya Liturujia ya Kanisa na hususan katika Kipindi cha Kwaresima; muda wa: Sala na kufunga; tafakari ya kina na matendo ya huruma yanayomwilishwa katika uhalisia wa maisha kama kielelezo makini cha imani tendaji. Kipindi cha Kwaresima kinawaandaa waamini kuweza kuadhimisha Siku ile iliyotangulia kuteswa kwake, Kristo Yesu alipoweka Sakramenti ya Ekaristi Takatifu, Daraja Takatifu na huduma ya upendo kwa jirani. Uelewa wa maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu unawasaidia waamini kuweza kukua na kukomaa katika maisha ya kiroho katika ngazi ya mtu binafsi na Kanisa katika ujumla wake. Huu ni mwaliko wa kuachana na tabia ya kuadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwa mazoea. Lengo na Tafakari hizi za Kipindi cha Kwaresima Kuhusu Ekaristi Takatifu zinapania pamoja na mambo mengine, kuwasaidia waamini kufikia “Maajabu ya Kiekaristi” kama ambavyo Mtakatifu Yohane Paulo II alivyozoea kuyaita.

Tafakari za Ijumaa 2022
10 March 2022, 15:51