Waraka Kwa Mapadre Kuhusu Maadhimisho Ya Sinodi ya XVI Ya Maaskofu
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Maadhimisho ya Sinodi ya XVI ya Maaskofu yananogeshwa na kauli mbiu “Kwa Ajili ya Kanisa la Kisinodi: Umoja, Ushiriki na Utume.” Ni maadhimisho ambayo yamezinduliwa mwaka 2021 kwa ngazi za kijimbo na yatahitimishwa Oktoba 2023 kwa ngazi ya Kanisa la Kiulimwengu. Ni maadhimisho yanayoamsha shauku na mshangao wa Kanisa katika mapambazuko ya Millenia ya Tatu ya Ukristo kuweza kutembea kwa pamoja. Huu ndio mwelekeo wa maisha na utume wa Kanisa kama ulivyobainishwa na Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican, kwani Kanisa na Sinodi ni visawe. Huu ni mwaliko wa kujenga na kudumisha umoja na mshikamano wa udugu wa kibinadamu, kwa kumsikiliza Roho Mtakatifu na kuendelea kujikita katika mchakato wa kupyaisha imani, ili kuwashirikisha watu wa Mungu katika mchakato wa kutangaza na kushuhudia Injili ya Kristo. Baba Mtakatifu Francisko anasema mchakato wa maadhimisho ya Sinodi ya XVI ya Maaskofu ni kutaka kuonesha ile sura ya Kanisa kama nyumba ya ukarimu, yenye milango wazi na inayokaliwa na watu. Na kwa njia hii, Mwenyezi Mungu anapenda kuhuisha mahusiano na mafungamano ya kidugu. Huu ni mwaliko kwa watu wa Mungu kuwa makini ili kamwe wasitumbukie katika hatari ambazo zimebainishwa na Baba Mtakatifu Francisko yaani: Urasmi unaofifisha Sinodi na kuwa kauli mbiu tupu; kiakili kwa kuifanya Sinodi kuwa ni tafakari ya kinadharia juu ya matatizo na kutohamaki na matokeo yake ni kukosa mabadiliko yanayokusudiwa.
Huu ni wakati muafaka kwa watu wa Mungu kufungua malango ya nyoyo zao na kusikiliza kile ambacho Roho Mtakatifu anapendekeza kwa Makanisa. Katika safari hii, ni wazi kuna hofu ambayo inaweza kuwashambulia Mapadre. Hii ni sehemu ya Waraka Kwa Mapadre uliondikwa na Kardinali Mario Grech, Katibu mkuu wa Sinodi za Maaskofu akishirikiana na Askofu mkuu Lazzaro You Heung Sik, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Wakleri kama mwaliko kwa ajili ya maadhimisho ya Sinodi ya XVI ya Maaskofu. Viongozi hawa wawili wanatambua mzigo mkubwa wa shughuli za kichungaji zinazotekelezwa na Mapadre sehemu mbalimbali za dunia. Kumbe, Sinodi si mzigo mwingine wanaotwisha Mapadre, bali ni mwaliko wa kutafakari na Kanisa kwa kujikita katika umoja, ushiriki na utume wa Kanisa; mambo ambayo tayari yameanza kukita mizizi katika jumuiya mbalimbali za Kikanisa. Mchakato wa maadhimisho ya Sinodi katika ngazi ya kijimbo unapania kukusanya utajiri wa uzoefu wa Sinodi hai, kwa kukutana, kusikilizana na kujifunza kutoka kwa wengine kama sehemu ya uzoefu usio rasmi unaojikita katika maisha ya kawaida. Ni wakati wa kusikilizana kwa kina, kujifunza na kuthamini karama za watu wengine. Ni mwaliko kwa kusaidiana na hatimaye kufanya maamuzi kwa pamoja kama kielelezo cha ushuhuda wa Sinodi inayomwilishwa katika vitendo kama sehemu ya utendaji wa Kanisa na Watu wa Mungu katika ujumla wao.
Huu ni mwaliko wa kuondoa vikwazo vinavyowekwa katika Ukuhani wa jumla wa waamini na juu ya ufahamu wa imani ya watu wa Mungu “Sensus fidei” hususan kuhusu utambulisho wao kama wahudumu waliowekwa rasmi na Mama Kanisa? Ni furaha na shangwe kubwa kupata ndugu wanaoshiriki katika kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu. Ikumbukwe kwamba, Makuhani wa Daraja wamepewa dhamana ya kuongoza, kufundisha na kuwatakatifuza watu wa Mungu, huduma ambayo inaweza kupyaishwa zaidi. Mapadre wanahimizwa kupyaisha shauku ya Maandiko Matakatifu yanayofunua upya wa Mungu na kukoleza upendo. Ni wakati wa kumwilisha Neno la Mungu katika matendo ili kujenga nyumba katika mwamba, daima wakijiaminisha katika maongozi ya Kristo Mfufuka kama ilivyokuwa kwa wale wafuasi wa Emau. Maadhimisho ya Sinodi iwe ni safari ya kusikilizana na kubadilika, kwa kuthamini mikutano ya maadhimisho ya Sinodi ya XVI ya Maaskofu, kwa kuondokana na ubinafsi na tabia ya kujirejelea. Upendo wa dhati uwe ni utambulisho wa wafuasi wa Kristo Yesu. Huu ni mwaliko kwa viongozi wa Kanisa kuganga na kuponya majeraha ya mahusiano na mafungamano ya Kanisa ambayo mara nyingi huathiri muundo wa Kanisa.
Lengo ni kujenga na kuimarisha ile furaha ya udugu wa ukuhani. Maadhimisho ya Sinodi ni muda muafaka kwa Mapadre kutoka ili kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu, kwa kujihusisha na majeraha ya binadamu; kwa kutembea, kusikiliza na kuwahudumia maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa vipaumbele vya jamii, ili kujenga ushirika na mafungamano ya kijamii. Huu ni mwaliko wa kukuza na kudumisha majadiliano ya kidini na kiekumene na watu wote wenye mapenzi mema ili kumwilisha tunu msingi za Kiinjili katika mazingira wanamoishi. Vipaumbele hivi ni changamoto kwa Mapadre kusoma alama za nyakati mintarafu maadhimisho ya Sinodi kwa sababu Sinodi ni wito wa Mungu kwa Kanisa la Milenia ya Tatu. Hii ni dira na mwelekeo wenye changamoto zake zinazojikita katika maswali, uchovu na vikwazo, lakini lengo ni kurejea tena katika mchakato wa uinjilishaji, kwa kuvuka vikwazo vyote kama ilivyokuwa kwa Sinodi ya Kwanza ya Yerusalemu. Kardinali Mario Grech, Katibu mkuu wa Sinodi za Maaskofu akishirikiana na Askofu mkuu Lazzaro You Heung Sik, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Wakleri wanahitimisha Waraka wao kwa Mapadre wakiwahimiza kujikita katika mchakato wa kusikiliza kwa makini, kujadiliana pamoja na utambuzi wa uwepo wa Jumuiya ambamo kila mtu anaweza kushiriki na kuchangia.
Hii ni Sinodi inayopania kupanda ndoto, kuchota unabii na maono; kwa kuruhusu matumaini kustawi na kushamiri, kukoleza ari na moyo wa uaminifu; kuganga na kuponya majeraha; kujenga na kuimarisha mahusiano; kupyaisha matumaini ya mapambazuko, kujifunza kutoka kwa wengine na hivyo kujenga ustadi angavu na hivyo kutoa nguvu mpya.