Padre Mbuyisa,C.M.M ni askofu mteule wa Kokstad Afrika Kusini
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Jamanne tarehe 6 Machi 2022, Baba Mtakatifu Francisko amemteua Askofu mpya wa jimbo Katoliki la Kokstad nchini Afrika Kusini, Padre Thulani Victor Mbuyisa, C.M.M., ambaye hadi uteuzi huo alikuwa ni Mkuu wa Shirika la Wamisionari wa Mariannhill. Askofu mteule Thulani Victor Mbuyisa, C.M.M, alizaliwa tarehe 13 Februari 1973 huko Exobho, wilaya ya KwaZulu-Natal, Jimbo kuu katoliki la Durban. Alijiunga katika Shirika la Wamisionari wa Mariannhill mnamo mwaka 1992, na kufunga nadhiri za daima, mnamo tarehe 2 Februari 1997. Aliendelea na masomo yake ya kijandokasisi ya kifalsafa (1994-96) na kitaalimungu mnamo (1996-99) katika Taasisi ya Kitaalimungu ya Mtakatifu Yosefu huko Cedara nchini Afrika Kusini.
Alipewa daraja la Upadre mnamo tarehe 4 Machi 2000, na baadaye alishika nyadhifa mbali mbali kama vile: Padre wa utume wa Mtakatifu Mikaeli, Padre katika utume Chuo Kikuu cha Kitaalimungu cha Mangosuthu na Chuo cha Mtakatifu Francisko cha Mariannhill na Makamu Mkurugenzi wa Wanovisi (2001-2002). Alihitimu masomo yake katika Sheria za Kanoni katika Chuo Kikuu cha Mtakatifu Paulo huko Ottawa, Canada mnamo (2002-2004); Msimamizi wa Kikanisa cha Chuo Kikuu cha Kitaalimungu cha Mangosuthu na Makamu Mkurugenzi wa Wanovisi (2005-2007); Mkuu na mtayarishaji katika nyumba ya Malezi ya Nivard huko Nairobi, Kenya mnamo (2007-2010); Mkuu wa Wamisionari wa Mariannhill wa Afrika Mashariki, Nairobi, Kenya (2010); Katibu Mkuu (2010-2012), wa Shirika la Wamisionari wa Mariannhill (2012-2016). Kuanzia Oktoba 2016 hadi uteuzi wake kuwa Askofu mpya alikuwa ni Mkuu wa Shirika lao la Mariannhill.