Rais wa Poland Akutana na Kuzungumza na Papa Francisko: Wakimbizi Wa Ukraine
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Baba Mtakatifu Francisko, Ijumaa tarehe 1 Aprili 2022 amekutana na kuzungumza na Rais Andrzej Duda wa Poland, ambaye baadaye alibahatika kukutana na kuzungumza pia na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican aliyekuwa ameambatana na Askofu mkuu Paul Richard Gallagher, Katibu mkuu wa mambo ya nchi za nje na ushirikiano wa Kimataifa mjini Vatican. Baba Mtakatifu Francisko na mgeni wake pamoja na mambo mengine wamezungumza kwa kina kuhusu vita kati ya Urussi na Ukraine, Usalama, Amani na Utulivu Barani Ulaya.
Ni katika muktadha huu, katika mazungumzo yao, wamejikita zaidi kuhusu hatma ya wakimbizi wa kivita kutoka Ukraine sanjari na huduma msingi wanazopaswa kupatiwa. Takwimu za Umoja wa Mataifa zinaonesha kwamba, zaidi ya wakimbizi wa kivita milioni 4.1 kutoka Ukraine wanapatiwa hifadhi nchini: Poland, Belarus, Slovakia, Hungaria, Romania, Moldova, Italia, Belarus na Urussi. Kati ya wakimbizi hao wote Poland imetoa hifadhi kwa wakimbizi wa kivita 2, 337, 000. Hizi ni takwimu hadi kufikia tarehe 31 Machi 2022. Kuna watu zaidi ya milioni 6.5 ambao hawana makazi maalum nchini Ukraine hadi kufikia tarehe 18 Machi 2022.