Mchakato wa Sinodi:Kanisa liko wazi na utajiri wa ulemavu!
Na Angella Rwezaula - Vatican.
Kipindi cha usikilizaji kwa njia ya mtandaoni kilichukua takriban saa mbili alasiri siku ya Alhamisi 19 Mei 2022 kwa kujikita na mafa juu ya “Kanisa ni nyumba yako. Mchango wa watu wenye ulemavu katika Sinodi”, iliyoahamaishwa na Baraza la Kipapa la Walei familia na Maisha kwa ushirikiano na sekretarieti kuu ya Sinodi ya Maaskofu. Kikao hicho kilichohudhuriwa na wawakilishi wa Mabaraza ya Maaskofu na vyama vya kimataifa ambapo kilikuwa na lengo la “kutoa sauti” moja kwa moja kwa watu wenye ulemavu, waamini mara kwa mara walioko pembezoni mwa Makanisa. Ingawa wengi wao tayari wameshiriki katika mikutano inayohamasishwa na maparokia, majimbo na vyama, mkutano huo kwa hakika ulikuwa ni uzinduzi wa mchakato halisi wa sinodi ya kimataifa iliyowekwa kwa ajili yao.
Je Roho anauliza nini kwa Kanisa letu?
Katika mazungumzo yenye nguvu, takriban washiriki 30 wenye ulemavu wa hisia, kimwili au utambuzi, waliounganishwa kutoka zaidi ya nchi 20 duniani kote na ambao waliweza kujieleza katika lugha zao (pamoja na lugha tatu za ishara) kwa kuzingatia utayarishaji wa pamoja wa hati ya kujibu swali msingi la Sinodi (yaani kitendea kazi): Tunatembeaje pamoja na Yesu tukiwa pamoja na ndugu ili kumtangaza? Kwa ajili ya kesho, Roho anauliza nini kwa Kanisa letu kukua katika safari pamoja na Yesu na pamoja na ndugu kumtangaza?
Shuhuda kutoka Liberia, Ukraine, Ufaransa na Mexico
Shuhuda nne zenye kusisimua kutoka Liberia, Ukraine, Ufaransa na Mexico zilivuta hisia kwenye hitaji la kushinda ubaguzi, kutengwa, ubaguzi wa kinababa. Maneno ya katekista Mfaransa aliye na ugonjwa wa Utindi wa Ubongo uligusa moyo sana kwa wasikilizaji: “Nilipozaliwa, ningeweza kutolewa mimba. Nina furaha kuishi. Ninapenda kila mtu na namshukuru Mungu kwa kuniumba”, alisema. Hapo mwanzo, Kardinali Mario Grech, katibu mkuu wa sekretarieti ya Sinodi ya Maaskofu, alieleza uzoefu wake binafsi: “Nina deni kwa watu wenye ulemavu. Ni mmoja wao aliyeniweka kwenye njia ya wito wa ukuhani wangu. Ikiwa uso wa kaka au dada mlemavu umetupwa, ni Kanisa ambalo huwa mlemavu”.
Muda wa kimya ni muhimu kusikiliza Roho
Katibu wa Baraza la Kipapa la Walei, Familia na Maisha Padre Alexandre Awi Mello aliwaambia washiriki wa mkutano huo kuwa katika mchakato wa harambee hiyo changamoto iliyopo ni “kuondokana na chuki yoyote ya wale wanaoamini kuwa wenye matatizo ya kujieleza hawana mawazo kweli, wala chochote cha kuvutia kuwasiliana ". Kwa kumalizia, Sista Nathalie Becquart, katibu msaidizi wa Sekretarieti ya Sinodi ya Maaskofu, alipendekeza kwa washiriki kuzingatia muda wa kimya, ili kusikiliza jinsi Roho Mtakatifu alivyozungumza na kila mtu, alisistiza. Kuna hazina za ubinadamu ambazo zimeshirikiswa na kutolewa kwa Kanisa.
Umuhimu wa kufafanua Waraka kwa miezi ijayo
Washiriki walialikwa kufafanua waraka wa pamoja katika miezi ijayo kuanzia na uzoefu wao na ujuzi wa ulimwengu wa ulemavu ambao wamekomaa kibinafsi na kupitia kujitoa kwao kichungaji. Hati hiyo itakabidhiwa kwa sekretarieti kuu ya Sinodi ya Maaskofu ili kuizingatia katika muendelezo wa safari ya sinodi. Mkutano huo ni sehemu ya njia iliyoanzishwa mwezi Desemba 2021 na Baraza la Kipapa la Walei, Familia na Maisha kwa kampeni ya video #IamChurch, kuhusu uongozi wa kikanisa wa watu wenye ulemavu na inalenga kuwa jibu la wito wa Papa katika Waraka wa Fratelli Tutti yaani Wote ni Ndugu( n.98) anapowaalika wanajamii “watoe sauti” kwa wale wasio na sauti walio tengwa au waliojifichika “... wanaojiona wapo bila kumilikiwa na bila kushiriki”. Lengo la Baba Mtakatifu sio kutoa msaada tu, lakini kushiriki kikamilifu katika jumuiya ya kiraia na kikanisa. Mchakato huo utakamilika katika miezi ijayo kwa mkutano wa ana kwa ana jijini Roma.