Mkutano Mkuu wa 19 wa SECAM, Accra, Ghana : Usalama na Wahamiaji Barani Afrika
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika na Madagascar, SECAM ni matunda ya maadhimisho ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican, uliowahamasisha Maaskofu kutoka Barani Afrika kushikamana kwa hali na mali, ili kuweza kukoleza ari na moyo wa kimisionari, tayari kujikita katika mchakato wa uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili. SECAM ikazinduliwa rasmi tarehe 31 Julai 1969 huko Kampala, Uganda. Katika kipindi cha miaka 50 iliyopita, kumekuwepo na mafanikio makubwa, changamoto, matatizo na fursa katika maisha na utume wa Kanisa Barani Afrika. Mtakatifu Paulo VI alipotembelea kwa mara ya kwanza Bara la Afrika kwa kufanya hija ya kitume nchini Uganda kwanza kabisa aliitaka familia ya Mungu Barani Afrika kuwa mashuhuda wa imani, matumaini na mapendo kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Kujenga na kudumisha ari na mwamko wa kimisionari, tayari kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu Barani Afrika. Mtakatifu Paulo VI alisema, viongozi wa kisiasa Barani Afrika wanapaswa kuwa ni vyombo na mashuhuda wa misingi ya haki, amani na maridhiano. Kanisa kwa kushirikiana na Serikali mbalimbali Barani Afrika zisaidie kukoleza mchakato wa maendeleo fungamani ya binadamu kwa: kusimama kidete kulinda na kutetea utu, heshima na haki msingi za binadamu, wanawake Barani Afrika wakipewa kipaumbele cha kwanza! Alilitaka Kanisa kuwekeza zaidi katika sekta ya elimu, afya, kilimo na huduma bora za maji safi na salama.
Katika muktadha huu, Mtakatifu Paulo VI alikazia umuhimu wa majadiliano ya kidini na kiekumene Barani Afrika, kama njia ya kukuza na kudumisha umoja, upendo na mshikamano wa kidugu. Alihimiza pia umuhimu wa kukuza na kuendeleza mashirika na vyama vya kitume ili kusaidia majiundo, malezi na makuzi ya imani, tayari kuchangia katika mchakato wa kuyatakatifuza malimwengu! Mtakatifu Paulo VI, katika hija yake ya kitume, aliwataka waamini kuiga mfano bora wa Mashahidi wa Uganda walioyamimina maisha yao kama kielelezo cha ushuhuda wa imani kwa Kristo na Kanisa lake. Akawataka wawe jasiri na thabiti katika imani, matumaini na mapendo kwa Mungu na jirani. Ujasiri wa imani unawawezesha waamini kumwilisha Neno la Mungu katika maisha na vipaumbele vyao. Waamini waendelee kuboresha imani yao kwa njia ya Sakramenti za Kanisa na Ibada mbali mbali, ambazo zitawasaidia kuwa kweli ni wafuasi wamisionari wa Kristo Yesu, kwa kuhakikisha kwamba, imani inamwilishwa katika matendo adili na matakatifu. Imani iwasaidie kuonesha upendo kwa Mungu na jirani. Mtakatifu Paulo VI, wakati alipokuwa anazungumza na Maaskofu Katoliki kutoka sehemu mbali mbali za Bara la Afrika, alikazia umoja na mshikamano katika urika wa Maaskofu katika kutekeleza dhamana na wajibu wao wa kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu.
Ili kukuza na kudumisha maisha ya Kikristo Barani Afrika kwa kutambua kwamba, tangu wakati huu, waafrika wenyewe wanapaswa kuwa ni wamisionari Barani Afrika tayari kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu kwa watu wa Mungu Barani Afrika. Dhamana hii inajikita katika ujenzi wa miundo mbinu ya Kanisa, itakayoliwezesha Kanisa kuonenana, chini ya uongozi wa Roho Mtakatifu. Kanisa kwa asili ni la kimisionari, dhamana inayopaswa kuendelezwa na kudumishwa Barani Afrika. Ni katika muktadha wa msingi wa maisha na utume wa SECAM Barani Afrika, Mababa 120 wa SECAM kuanzia tarehe 25 Julai hadi tarehe 1 Agosti 2022 wanaadhimisha Mkutano mkuu wa 19 unaonogeshwa na kauli mbiu “Umiliki wa SECAM: Usalama na Uhamiaji Barani Afrika na Visiwani.” Kardinali Luis Antonio Gokim Tagle, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa Watu, Tarehe 26 Julai 2022 ameadhimisha Ibada ya Misa Takatifu ya Ufunguzi wa Mkutano mkuu wa 19 wa SECAM, kwenye Kanisa kuu la Kristo Mfalme, Jimbo kuu la Accra, Ghana, amewataka Maaskofu Barani Afrika kujizatiti kikamilifu katika mchakato wa uinjilishaji wa kina Barani Afrika, unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili. Ni wakati wa kufanya upembuzi yakinifu na tafakari ya kina ili kuangalia uhusiano na mafungamano yao na Mwenyezi Mungu. SECAM iwe ni chombo na kielelezo cha ushirika wa watu wa Mungu Barani Afrika na kwamba, Mabaraza yote yanapaswa kukiunga mkono, ili kiweze kutekeleza dhamana na wajibu wake katika mchakato mzima wa uinjilishaji wa kina Barani Afrika. Ulinzi na usalama, vipewe kipaumbele cha pekee ili kudumisha utu, heshima na haki msingi za binadamu.
Kardinali Luis Antonio Gokim Tagle anasema, Maadhimisho ya Mafumbo ya Kanisa yasaidie kupyaisha ari na mwamko wa uinjilishaji Barani Afrika. Ni wakati mwingine tena wa kukutana na Kristo Mfufuka, tayari kwenda kumtangaza na kumshuhudia Kristo Yesu, aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu, kwa ajili ya kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti. Maadhimisho ya Mkutano mkuu wa SECAM ni fursa ya kuangalia mafanikio yaliyokwisha kupatikana, matatizo, changamoto, fursa na mapungufu yaliyopo, ili kuomba neema na baraka za Mwenyezi Mungu, tayari kuanza tena upya. Jambo hili linawezekana ikiwa kama Kristo Yesu atapewa kipaumbele cha kwanza katika maisha, sanjari na kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha utu, heshima na haki msingi za binadamu. Ni muda muafaka wa kujifunza kutoka kwa wengine; kushirikisha uzoefu na mang’amuzi; kukiri mapungufu na kuanza kuchukua hatua madhubuti zitakazosaidia mchakato wa maboresho ya sera na mikakati ya shughuli za kichungaji Barani Afrika. Mchakato wa uinjilishaji mpya unaosimikwa katika ushuhuda wa huduma ya huruma na mapendo kwa watu wa Mungu, vinginevyo ukorofi na mabavu vitatawala. Ushirika mkamilifu ni chombo madhubuti cha kusimamia: utu, heshima na haki msingi za binadamu na hivyo usalama kutawala katika maisha ya watu. Kamwe usalama na amani visitumiwe kisiasa kwani matokeo yake ni uvunjifu wa haki msingi za binadamu.
Sinodi na Ujenzi wa Kanisa la Kisinodi: Maadhimisho ya Sinodi ya 16 ya Maaskofu yananogeshwa na kauli mbiu “Kwa Ajili ya Kanisa la Kisinodi: Umoja, Ushiriki na Utume.” Dhana ya Sinodi ni wazo lililotolewa na Mtakatifu Paulo VI, linaloihusisha Familia ya Mungu katika ujumla wake. Baba Mtakatifu Francisko analitaka Kanisa kuanza kumwilisha dhana hii katika maisha ya Makanisa mahalia; Mabaraza ya Maaskofu; Mashirikisho ya Kanda hadi kufikia Kanisa la Kiulimwengu. Mtakatifu Paulo VI, Muasisi wa maadhimisho ya Sinodi mara baada ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican anasema, Sinodi ni chombo cha kimisionari na uinjilishaji mpya unaolisaidia Kanisa baada ya kutembea pamoja katika sala, tafakari, mang’amuzi na hatimaye, utekelezaji wake unaofanywa na watu wote wa Mungu kadiri ya wito na nafasi zao katika maisha na utume wa Kanisa. Sinodi ni sehemu ya vinasaba vya maisha na utume wa Kanisa. Juhudi za kichungaji na kitaalimungu zisaidie kuimarisha dhana ya Sinodi katika maisha na utume wa Kanisa mintarafu majadiliano ya kiekumene, kwa kumpokea Roho Mtakatifu ili kuweza kujifunza mengi kutoka kwa wengine na kuvuna kile ambacho Roho Mtakatifu amepanda ndani yao, ambacho kimekusudiwa kuwa ni zawadi kwa wengine.
Wakimbizi, Wahamiaji na Wanaotafuta Hifadhi ya Kisiasa. Kutokana na vita, kinzani na mipasuko y kijamii, kisiasa na kidini; umaskini, njaa na maradhi; nyanyaso na dhuluma mbalimbali, wananchi wengi Barani Afrika wamejikuta wakilazimika kuzikimbia nchi na makazi yao, ili kutafuta hifadhi, maisha bora zaidi na usalama ndani na nje ya Bara la Afrika. Kwa bahati mbaya, wakimbizi na wahamiaji hawa wamekuwa wakikabiliana na kifo uso kwa uso wanapokuwa njiani kuelekea kwenye nchi “zilizojaa maziwa na asali.” Ni makundi yanayokumbana na ukatili wa ajabu pamoja na sheria kandamizi; hali ambayo inapelekea wakimbizi na wahamiaji wengi kufa wakiwa njiani au kuishi katika mashaka na hali ya kudhaniwa vibaya. Mwelekeo kama huu aliwahi kusema Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto XVI katika Waraka wake wa Kitume Dhamana ya Afrika, “Africae munus,” huamsha matendo ya kutovumiliana, chuki na ubaguzi kwa wageni na wahamiaji; dhuluma na nyanyaso. Kanisa linapenda kutoa changamoto ya pekee kwa waamini pamoja na watu wenye mapenzi mema kuguswa na mahangaiko ya wakimbizi na wahamiaji kwa kuonesha mshikamano wa upendo; kwa kuwapatia mahali salama panapoweza kuwakirimia matumaini ya leo na kesho iliyo bora zaidi. Kanisa litaendelea kusimama kidete kuwalinda, kuwatetea na kuwahudumia wakimbizi.
Kanisa Katoliki katika sera na mikakati yake kuhusu huduma kwa wakimbizi, wahamiaji na wale wanaotafuta hifadhi ya kisiasa linapenda kukazia kwa namna ya pekee umuhimu wa: “Kuwapokea, kuwalinda, kuwaendeleza na kuwahusisha wakimbizi na wahamiaji” katika maisha ya jamii inayowapatia hifadhi. Kumbe, kuna haja ya kujenga utamaduni wa kuwapokea, kuwalinda, kuwaendeleza na kuwahusisha wakimbizi katika maisha ya jamii inayowapatia hifadhi dhidi ya utamaduni wa utandawazi usiojali wala kuguswa na mahangaiko ya wengine! Baba Mtakatifu Francisko anawapongeza na kuwashukuru watu na vyama vya kitume vinavyoendelea kujisadaka kwa ajili ya huduma makini kwa wakimbizi na wahamiaji.