Tafuta

Mishumaa kwa ajili ya kumwombea Malkia Elizabeth II Mishumaa kwa ajili ya kumwombea Malkia Elizabeth II  

Kard.Roche,kifo cha Malkia Elizabeth:Alikuwa na imani ya Kikristo!

Imani ya Kikristo,huduma kwa taifa,ukarimu na huruma zimemfanya Elizabeth II kuwa Malkia anayependwa na wote.Haya ni maneno katika salamu za rambirambi za Kardinali Arthur Roche,Askofu Mkuu Mstaafu wa Leeds,na Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la la Ibada na Nidhamu ya Sakramenti za Kanisa kufuatia na kifo cha Malkia Elizabeth II kilichotokea tarehe 8 Septemba 2022.

Na Angella Rwezaula – Vatican.

Katika ujumbe mfupi, baada ya kupata habari za kifo cha Malkia Elizabeth II, kilichotokea Alhamisi jioni tarehe 8 Septemba 2022, Kadinali Mwingereza Arthur Roche Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Ibada na Nidhamu ya Sakramenti ya Kanisa ameelezea wasifu wa Malkia na ameonesha hisia za rambirambi kwa wote, wale wanaofanya kazi katika Vatican na wanaotoka Uingereza, Ireland ya Kaskazini na nchi za Jumuiya ya Madola. Katika taarifa yake, alisisitiza kwamba marehemu Malkia alijitolea bila kuchoka kwa huduma ya watu wake, lakini pia aliwakabidhi kwa ulinzi wa Mungu”.

Masikitiko kwa wafanyakazi wa Vatican wanaotoka Uingereza,Ireland Kaskazini na Jumuiya za Madola

Kardinali Roche alisema: "Sisi tunaofanya kazi Vatican na tunatoka Uingereza, Ireland ya Kaskazini na nchi za Jumuiya ya Madola, tumepatwa na masikitiko makubwa kwa habari za kifo cha Malkia Elizabeth II. Tangu kutawazwa kwake katika kiti cha enzi mnamo mwaka 1952, baada ya kifo cha babake Mfalme George VI, sio tu kwamba alijitoa bila ya kujibakiza kuwatumikia watu wake, lakini  pia aliwakabidhi katika ulinzi wa Mungu".

Malkia Elizabeth na Imanai ya Kikristo

Kardinali Roche akiendelea na kueleza wasifu wa Malkia mpendwa wa watu alisema kardinali  "Imani yake ya Kikristo, iliyooneshwa mara nyingi katika ujumbe wake wa kila mwaka katika siku kuu ya Kuzaliwa kwa Bwana na katika matukio mengine, ulikuwa unaonesha  nyakati za ushuhuda wa ajabu kwa imani yake, kwa Injili na kwa tunu za manufaa ya wote, maisha ya familia, amani na maelewano kati ya watu.

Fadhila ya huruma kwa watu wake

Fadhili na huruma yake kwa watu, zawadi zake kama kiongozi wa serikali na upendo kwa watu wake katika nchi nyingi, tamaduni na dini nyingi za Jumuiya ya Madola zimeshuhudia uhusiano usiovunjika na wa kipekee wa kujitolea kwa huduma ya wengine ulipendwa na kila mtu. Kufuatia ahadi aliyoitoa kwenye kipindi chake maarufu cha radio akiwa na umri wa miaka 21 mnamo mwaka 1947, alisimama kidete hadi wakati wa kifo chake, akitimiza maneno yake mwenyewe: 'Natangaza mbele yenu nyote kwamba maisha yangu yote, marefu au mafupi kwamba ama, nitajikita katika huduma yenu”.

 

09 September 2022, 13:16