Kard.Krajewski,kwa mara ya 4 anawakilisha Papa nchini Ukraine
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Taarifa kutoka katika Baraza la Kipapa la Huduma ya Upendo, tarehe 9 Septemba 2022 imebainisha kuwa katika siku hizi, Mkuu mpya wa Baraza hili Kardinali Konrad Krajewski, atakwenda kwa mara ya nne nchini Ukraine kwa niaba ya Baba Mtakatifu kuonesha ukaribu na msaada wa watu ambao wanazidi kuelewa na matatizo. Kwa mara hii ataelekea maeneo ya Odessa, Žytomyr, Charkiv na sehemu nyingine mahalia Mashariki wa Ukraine ili kuwatembelea na kusaidia baadhi ya jumuiya za waamini, mapadre, watawa na maaskofu wao ambao kwa siku zaidi ya 200 wanaendelea kubaki katika mahali pa huduma yao licha ya hatari ya vita.
Ni ziara ya ukimya na kiinjili, kwa ajili ya kukaa na watu wanaoteseka, kusali na kuwatia moyo kila mmoja wao, kwa kuonesha kweli kwamba uwepo wao hawako peke yao katika hali hiyo ambayo wanapeleka mbele ya uharibifu na kifo. Hata hivyo safari hii pia imesindikizwa na msaada wa dhati kupitia Caritas mbali mbali za majimbo.