Silaha za nyuklia ni hatari kwa ulinzi na usalama; ustawi, maendeleo na mafao ya wengi Silaha za nyuklia ni hatari kwa ulinzi na usalama; ustawi, maendeleo na mafao ya wengi 

Mkutano Mkuu wa 66 Wakala Wa Kimataifa wa Nguvu za Atomic, IAEA: Ulinzi na Usalama Hatarini

Vatican itaendelea kunogesha mchakato wa majadiliano ili kudumisha utamaduni wa utunzaji bora wa mazingira unaotoa kipaumbele cha kwanza kwa utu, heshima na haki msingi za binadamu. Ni mwaliko kwa Jumuiya ya Kimataifa kuendelea kujizatiti ili hatimaye, kutokomeza mambo yote yanayosababisha chokochoko, kinzani na hatimaye, vita kati ya watu wa Mataifa. Ulinzi na Amani.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Askofu mkuu Paul Richard Gallagher, Katibu mkuu wa Mambo ya Nchi za Nje, Ushirikiano na Mashirika ya Kimataifa akichangia hoja kwenye mkutano mkuu wa 66 wa Wakala wa Kimataifa wa Nguvu za Atomic, IAEA, amewapongeza Wakala kwa mchango wake katika mchakato wa kudhibiti utengenezaji, ulimbikizaji na matumizi ya silaha ya kinyuklia ili kusaidia mchakato wa maendeleo endelevu ya binadamu kwa njia ya ushirikiano wa kimataifa. Lengo kuu ni kuiwezesha Jumuiya ya Kimataifa kujikita zaidi katika ulinzi na usalama kwa sababu maafa yanayoweza kusababisha na silaha za kinyuklia ni makubwa sana kwa maisha ya binadamu na mazingira yake. Nishati ya atomic inapaswa kutumiwa kwa ajili ya kunogesha mchakato wa maendeleo fungamani ya binadamu na wala si kuwa ni chanzo cha: maafa na majanga kwa watu na mali zao. Kuna uhusiano wa karibu sana kati ya udhibiti wa utengenezaji, matumizi, usambazaji na ulimbikizaji wa silaha za kinyuklia na upigaji rufuku wa silaha hizi, kwa ajili ya mchakato wa kujenga na kudumisha amani na utulivu duniani. Ujumbe wa Vatican katika mkutano huu, unawahimiza wadau kuendelea kujikita katika majadiliano katika ukweli na uwazi ili kuondokana na maamuzi mbele na hivyo kuendelea kunogesha: amani, ustawi, maendeleo na mafao ya wengi; kwa kuheshimu na kujali tofauti msingi zinazojitokeza kuwa ni sehemu ya amana na utajiri wa Jumuiya ya Kimataifa.

Ulinzi na usalama vipewe kipaumbele cha kwanza
Ulinzi na usalama vipewe kipaumbele cha kwanza

Vatican itaendelea kunogesha mchakato wa majadiliano ili kudumisha utamaduni wa utunzaji bora unaotoa kipaumbele cha kwanza kwa utu, heshima na haki msingi za binadamu. Ni mwaliko kwa Jumuiya ya Kimataifa kuendelea kujizatiti ili hatimaye, kutokomeza mambo yote yanayosababisha chokochoko, kinzani na hatimaye, vita kati ya watu wa Mataifa. Baba Mtakatifu, Jumapili, tarehe 24 Novemba 2019 alizungumzia kuhusu mateso na maafa makubwa yaliyosababishwa na mashambulizi ya mabomu ya atomiki, changamoto na mwaliko kwa Jumuiya ya Kimataifa kusimama kidete kulinda na kudumisha misingi ya: usalama, amani na utulivu. Ni mwaliko wa kuondokana na wasi wasi pamoja na hofu inayotawala akilini na nyoyoni mwa watu kiasi cha kushindwa kuaminiana, na hivyo, kudhohofisha mafungamano ya watu wa Mataifa pamoja na mchakato wa majadiliano. Amani na utulivu wa kimataifa vinaweza kujengeka katika msingi wa mshikamano na ushirikiano wa haki kwa ajili ya huduma kwa kutambua kwamba, watu wanategemeana na kukamilishana; na wanapaswa kuwajibika kama wamoja kwa ajili ya ustawi wa familia nzima ya binadamu. Amani ya kweli inasimikwa katika kanuni maadili, utu wema na mshikamano wa udugu wa kibinadamu, tayari kusimama kidete kulinda na kutunza mazingira nyumba ya wote.

Silaha za nyuklia ni tishio kwa usalama, amani na mafungamano.
Silaha za nyuklia ni tishio kwa usalama, amani na mafungamano.

Wakala wa Kimataifa wa Nguvu za Atomic, IAEA ni chombo kinachopaswa kulindwa na kuendelezwa, ili kudhibiti utengenezaji, ulimbikizaji na usambazaji na matumizi ya silaha za maangamizi. Nishati ya atomic isaidie maboresho katika huduma ya afya, uzalishaji na usalama wa chakula na katika medani mbalimbali za maisha ya mwanadamu. Watu wanapaswa kuaminiana na kuthaminiana, ili waweze kushikamana na kushirikiana, kwa ajili ya ujenzi wa amani na usalama, ili dunia iweze kuondokana na hofu ya mashambulizi ya silaha za nyuklia. Askofu mkuu Paul Richard Gallagher, Katibu mkuu wa Mambo ya Nchi za Nje, Ushirikiano na Mashirika ya Kimataifa anasema, maambukizi makubwa ya Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19 yamepelekea madhara makubwa: Kimaadili, kijamii, kiuchumi na kisiasa na wanaoteseka zaidi ni “akina yakhe pangu pakavu tia mchuzi” yaani maskini. Vatican inapania kuona mfumo wa maendeleo unaojikita katika udugu wa kibinadamu na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Nishati ya Atomic isaidie maboresho katika tiba ya mwanadamu; mchakato wa uzalishaji na usalama wa chakula duniani; kwa kukabiliana na athari za mabadiliko makubwa ya tabianchi, ili hatimaye, kuwa na uhakika wa usalama wa chakula na maji safi. Nishati ya Atomic isaidie mapambano dhidi ya ugonjwa wa Saratani duniani. Ni katika muktadha huu mchakato wa kudhibiti utengenezaji, ulimbikizaji na matumizi ya silaha ya kinyuklia utaiwezesha Jumuiya ya Kimataifa kudumisha: Ulinzi na usalama; amani na matumizi bora ya teknolojia kwa ustawi, maendeleo na mafao ya wengi.

Nguvu za Atomic
27 September 2022, 16:59