Tafuta

Mama Kanisa kila mwaka ifikapo tarehe 21 Oktoba, anaadhimisha Kumbukumbu ya Mt. Gaspari del Bufalo mfano bora wa uinjilishaji wa kina unaojikita katika ushuhuda na utakatifu wa maisha. Mama Kanisa kila mwaka ifikapo tarehe 21 Oktoba, anaadhimisha Kumbukumbu ya Mt. Gaspari del Bufalo mfano bora wa uinjilishaji wa kina unaojikita katika ushuhuda na utakatifu wa maisha. 

Ndoto ya Mtakatifu Gaspari del Bufalo Bado Inaendelea...!

Mtakatifu Gaspari del Bufalo ni mfano bora wa uinjilishaji wa kina unaojikita katika ushuhuda na utakatifu wa maisha; kwa kusikiliza na kujibu kilio cha damu ya maskini, wagonjwa na wale wote wanaonyanyaswa na kusukumizwa pembezoni mwa vipaumbele vya jamii. Kwa wote hawa Mtakatifu Gaspari del Bufalo akawa ni ndugu, rafiki na mlinzi wa daima, ndoto yake bado inaendelea...!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mama Kanisa kila mwaka ifikapo tarehe 21 Oktoba, anaadhimisha Kumbukumbu ya Mtakatifu Gaspari del Bufalo mfano bora wa uinjilishaji wa kina unaojikita katika ushuhuda na utakatifu wa maisha; kwa kusikiliza na kujibu kilio cha damu ya maskini, wagonjwa na wale wote wanaonyanyaswa na kusukumizwa pembezoni mwa vipaumbele vya jamii. Kwa wote hawa Mtakatifu Gaspari del Bufalo akawa ni ndugu, rafiki na mlinzi wa daima. Mtakatifu Gaspari ni mtume hodari wa Damu Azizi ya Yesu, chemchemi ya huruma, upendo na ukombozi wa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti. Katika maisha na utume wake, alibahatika kusimama kidete na kwa ujasiri mkubwa, akapambana na madhulumu dhidi ya Kanisa wakati wake, huku akiwa amejiaminisha na kujikabidhi chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria, Msaada wa Wakristo, Mama wa Mungu na Kanisa. Alikuwa ni mhubiri maarufu wa Neno la Mungu lililoacha chapa ya kudumu katika maisha ya wale wote waliolisikiliza, kati ya hawa ni Mtakatifu Maria De Mattias, Mwanzilishi wa Shirika la Masista Waabuduo Damu Azizi ya Yesu, ASC.

Kijiji cha Matumaini Dodoma ni ushuhuda wa huruma na upendo wa Mungu
Kijiji cha Matumaini Dodoma ni ushuhuda wa huruma na upendo wa Mungu

Mtakatifu Gaspari del Bufalo alijisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya kutangaza Habari Njema ya Wokovu, akawa na ujasiri wa kuweza kusikiliza na kujibu kilio cha maskini na wale wote waliokuwa wametengwa na jamii kutokana na kukengeuka na hatimaye kutopea katika dhambi. Mtakatifu Gaspari del Bufalo alizaliwa tarehe 6 Januari 1786 mjini Roma. Tangu wakati wa ujana wake, alionesha ari na mwamko wa kutaka kutangaza na kushuhudia Injili ya Kristo Yesu, miongoni mwa maskini, wagonjwa na wakulima. Alipewa Daraja Takatifu ya Upadre tarehe 31 Julai 1808 na wakati wa madhulumu ya Mfalme Napoleone Bonaparte alipelekwa uhamishoni na kufungwa gerezani huko Piacenza. Baada ya Ufalme wa Napoleone Bonaparte kuporomoka, Papa Pio VII akampatia dhamana ya kupyaisha maisha na utume wa Mapadre na watu wa Mungu Jimboni Roma katika ujumla wao. Akautekeleza utume huu kwa uaminifu mkubwa kwa njia ya mahubiri na mafungo ya kiroho. Tarehe 15 Agosti 1815 akaanzisha Shirika la Wamisionari wa Damu Azizi ya Yesu, C.PP.S. Akafariki dunia tarehe 28 Desemba 1837 na kutangazwa kuwa Mtakatifu na Papa Pio XII tarehe 12 Juni 1954. Ndoto ya Mtakatifu Gaspari bado inaendelea sehemu mbalimbali za dunia.

Kanisa nchini Tanzania limeendelea kuchangia katika ustawi na maendeleo ya watu.
Kanisa nchini Tanzania limeendelea kuchangia katika ustawi na maendeleo ya watu.

Kumekuwepo na maendeleo makubwa sana katika huduma ya afya inayotolewa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tangu watanzania walipojipatia uhuru wao. Licha ya maboresho katika sekta ya afya, bado Kanisa litaendelea kuwekeza katika huduma kwa wagonjwa, kama sehemu ya utekelezaji wa dhamana na utume wake wa kinabii, kwa ajili ya maskini wapya katika sekta ya afya! Yaani: wagonjwa wanaosumbuliwa na magonjwa sugu; magonjwa nasibu, wagonjwa wa afya ya akili, wazee na maskini wanaoteseka kupata huduma bora ya tiba. Katika mchakato huu, Shirika la Wamisionari wa Damu Azizi ya Kristo linalomiliki na kuendesha Hospitali ya Rufaa ya Mtakatifu Gaspar, iliyoko, Itigi, Manyoni, Singida nchini Tanzania kwa miaka kadhaa imejipambanua kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa huduma bora ya tiba kwa watoto wadogo, amana na utajiri wa taifa la Tanzania. Ikumbukwe kwamba, utambulisho huu unapata chimbuko lake kutoka katika Injili ya huruma ya Mungu, “nilikuwa mgonjwa, mkaja kunitazama”. Haya ni matendo ya huruma: kiroho na kimwili, kielelezo cha imani tendaji. Hii ndiyo changamoto changamani ambayo imefanyiwa kazi na Mama Kanisa kwa kuanzisha vituo vya huduma kwa ajili ya wagonjwa na maskini, kama sehemu ya utekelezaji wake wa utume wa kinabii: kwa kusoma alama za nyakati, kusikiliza na hatimaye, kujibu kilio cha maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii mintarafu mwanga wa Injili.

Wamisionari wa Damu Azizi ya Yesu ni mashuhuda wa Uinjilishaji Tanzania
Wamisionari wa Damu Azizi ya Yesu ni mashuhuda wa Uinjilishaji Tanzania

Kumbukizi la Miaka 20 tangu kuanzishwa kwa Kijiji cha Matumaini kwa ajili ya watoto wanaoishi katika mazingira magumu na hatarishi, tarehe 17 Agosti 2022, ni sehemu ya ndoto kubwa ya Mtakatifu Gaspari del Bufalo ya kujibu kilio cha maskini. Kijiji cha Matumaini kinachoendeshwa na kusimamiwa na Masista Waabuduo Damu Azizi ya Yesu kwa kushirikiana na Wamisionari wa Damu Azizi ya Yesu Tanzania, kilizinduliwa rasmi tarehe 17 Agosti 2002. Mwaka 2022, kinaadhimisha kumbukizi la Miaka 20 ya Huruma, Upendo na Matumaini yanayomwilishwa katika uhalisia wa watoto wanaoishi katika hali na mazingira magumu. Kumbukizi hii ni kielelezo cha shukrani kwa Mwenyezi Mungu, aliyewawezesha Padre Vincent Boselli na Sr. Maria Rosaria Gargiulo, ASC kutumia vipaji na karama zao, kwa kushirikiana na watu wenye mapenzi mema, kuanzisha Kijiji cha Matumaini. Kijiji kilianza na watoto watatu, waliokuwa wameathirika kwa Ugonjwa wa Ukimwi. Leo hii, Kijiji cha Matumaini kina watoto 145, kati yao kuna wavulana 62 na wasichana 83 wanaoishi na kutunzwa kwenye nyumba 13 zinazohudumiwa kwa mtindo wa familia, ili kuhakikisha kwamba, watoto wote walau wanaonja huruma na upendo kutoka kwa wazazi wao, wanaojisadaka kwa ajili ya ustawi na maendeleo yao: kiroho, kimwili na kiakili.

Kanisa limewekeza sana katika huduma ya afya nchini Tanzania
Kanisa limewekeza sana katika huduma ya afya nchini Tanzania

Wamisionari wa Shirika la Damu Azizi ya Yesu, licha ya huduma Parokiani, Mafungo na shughuli za kiroho, lakini pia wameendelea kujikita katika huduma ya maji safi na salama. Maji safi na salama ni sehemu ya haki msingi za binadamu kwani ni muhimu sana katika maisha ya viumbe hai, ustawi na maendeleo endelevu ya binadamu katika Nyanja mbali mbali za maisha. Maji ni kito cha thamani ambacho Mwenyezi Mungu amemkirimia mwanadamu na kichocheo kikubwa cha maendeleo ya kiuchumi na ustawi wa jamii ya binadamu. Maji ni hitaji muhimu sana la binadamu linalopaswa kulindwa, kutunzwa na kuendelezwa kama anavyokazia Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake wa kitume, “Sifa iwe kwako “Juu ya utunzaji wa nyumba ya wote”, bila maji, maisha ya binadamu yako mshakani na hatarini sana! Kanisa katika Mafundisho Jamii linakazia umuhimu wa matumizi ya maji safi na salama kama njia makini ya kulinda na kudumisha utu na heshima ya binadamu. Kumbe, maji yanapaswa kupatikana kwa wote katika umbali unaokubalika na kwamba, huduma hii iwe ni endelevu! Uchafuzi wa vyanzo vya maji ni hatari sana kwa maisha ya binadamu na ekolojia nzima. Wamisionari wanaendelea kuwekeza katika sekta ya elimu na ufundi stadi, bila kusahau sekta ya mawasiliano ya jamii, kwa kuanzisha na kuendesha Kituo cha Radio Mwangaza, FM, Dodoma, kama sehemu ya mchakato wa uinjilishaji kwa njia za mawasiliano ya kisasa!

Ndoto inaendelea
21 October 2022, 16:54