Padre Emile Mushosho Matabaro ni Askofu mpya wa Jimbo la Doruma Dungu,DRC
Na Angella rwezaula – Vatican.
Baba Mtakatifu Francisko amemteua Askofu wa Jimbo la Doruma-Dungu nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo(DRC), Padre Emile Mushosho Matabaro, wa Bukavu ambaye hadi uteuzi huo alikuwa ni msimamizi wa kitume wa jimbo hilo. Mheshimiwa Padre Emile Mushosho Matabaro alizaliwa mnamo tarehe 5 Machi 1967 huko Bukavu. Alijiunga na Seminari ndogo ya Mugeri -Katana, Seminari Kuu ya Busimba huko Goma na baadaye seminari kuu nyingine ya Mtakatifu Pio X, Murhesa. Alipewa daraja la ukuhani mnamo tarehe 17 Septemba 2000 kwa ajili ya jimbo Kuu la Bukavu.
Shughuli za kichungaji
Kuanzia 2007 hadi 2012 aliendelea na masomo ya Taalimungu ambapo kuanzia mwaka 2013 hadi 2017 alipata uzamivu huko Dámaso (UESD), Madrid Hispania. Alijikita katika shughuli za kichungaji kama makamu Paroko na na paroko wa Ciherano (2000-2003); Paroko wa Mtakatifu Pierre huko Cibimbi (2003-2007) na wa parokia ya Bagira (2011); Mkurugenzi wa Ofisi ya Jimbo kwa ajili ya shughuli za Kijamii na kwa ajili ya Maendeleo (2011-2012); Rais wa Umoja wa Makleri Jimbo (2011-2013); Mweka hazina na Mratibu wa Tume ya Jimbo la Beni (2017-2018); Makamu Askofu na Mhudumu wa Uchumi na kansela (2018- 2019); Makamu Mkuu wa Jimbo Kuu la Bukavu (2019- 2021). Tangu 2021 amekuwa msimamizi wa kitume Jimbo hilo la Doruma-Dungu hadi uteuzi huo.