Papa atashiriki Mkutano kuhusu "Kilio cha Amani"
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Kwa kujibu mswali ya waandishi wa habari Dk. Matteo Bruni , Jumanne tarehe 11 Okotba 2022, amesema kuwa Baba Mtakatifu atashiriki Mkutano wa Sala kimataifa kwa ajili ya kuombea Amani duniani na wawakilishi viongozi wakuu kidini Ulimwenguni, ulioandaliwa na Jumuiya ya Mtakatifu Egidio, ambao unaongozwa na kauli mbiu: Kilio cha Amani,” utakofanyika tarehe 25 Oktoba katika Magofu jijini Roma. Mkutano wa mwaka jana ulianza tarehe 6 hadi 7 Septemba 2021 kwa ushiriki na uwepo wa viongozi wakuu wa kidini kutoka sehemu mbalimbali za duniani, akiwemo Baba Mtakatifu Francisko ambapo uliongozwa na kauli mbiu “Watu ndugu, Ardhi ya baadaye.”
Amani ya kweli inajengwa katika msingi wa maendeleo endelevu ya binadamu: kiroho na kimwili; kanuni maadili na utu wema; utawala wa sheria na haki msingi za binadamu! Vita, sawa na mipasuko ya kijamii ni hali halisi ya maisha ya binadamu yanayopaswa kufanyiwa kazi kwa kujikita katika kanuni maadili, sheria za kimataifa ikiendana na ujenzi wa siasa ya amani duniani ambayo inajikita na majadiliano katika ukweli na uwazi. Baba Mtakatifu Francisko amekuwa akikazia hayo na kwamba Jumuiya ya Kimataifa haina budi kuwekeza katika mchakato wa ujenzi wa utamaduni wa amani duniani; upendo na mshikamano wa udugu wa kibinadamu majadiliano pamoja kwa kulinda na kudumisha haki msingi za binadamu, uhuru pamoja na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya pamoja.