Papa Francisko tarehe 20 Oktoba 2022 amekutana na kuzungumza na Iris Xiomara Castro Sarmiento wa Jamhuri ya Honduras. Papa Francisko tarehe 20 Oktoba 2022 amekutana na kuzungumza na Iris Xiomara Castro Sarmiento wa Jamhuri ya Honduras. 

Rais Iris Xiomara Castro Sarmiento Akutana na Papa Francisko Mjini Vatican: MChango wa Kanisa

Baba Mtakatifu na Rais Iris Xiomara Castro Sarmiento wa Jamhuri ya Watu wa Honduras, katika mazungumzo yao, wamejielekeza katika madhara makubwa yanayosababishwa na mabadiliko ya tabianchi, mapambano dhidi ya umaskini na umuhimu wa kuendelea kujikita katika kusimamia ustawi, maendeleo na mafao ya wengi, huku upatanisho wa Kitaifa vikipewa msukumo wa pekee.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko, Alhamisi tarehe 20 Oktoba 2022 amekutana na kuzungumza na Rais Iris Xiomara Castro Sarmiento wa Jamhuri ya Watu wa Honduras, ambaye baadaye amekutana na kuzungumza pia na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican aliyekuwa ameambatana na Askofu mkuu Paul Richard Gallagher, Katibu mkuu wa Mambo ya Nchi za Nje, Ushirikiano na Mashirika ya Kimataifa. Katika mazungumzo yao, Baba Mtakatifu na mgeni wake, wameridhishwa na mahusiano mazuri ya kidiplomasia kati ya nchi hizi mbili na kwa pamoja wametia nia ya kuyaimarisha, kwa kuongezea makubaliano kati ya Serikali ya Honduras na Vatican.

Mchango wa Kanisa katika huduma ya elimu na afya ni muhmu.
Mchango wa Kanisa katika huduma ya elimu na afya ni muhmu.

Viongozi hawa wamegusia pia mchango muhimu unaotolewa na Kanisa nchini Honduras hasa katika sekta ya elimu na afya sanjari na huduma ya upendo inayotoa kipaumbele cha kwanza kwa wakimbizi, wahamiaji na watu wasiokuwa na makazi maalum, bila kuwasahau maskini ambao utu, heshima na haki zao msingi zinasiginwa na ugumu wa maisha. Baba Mtakatifu na Rais Iris Xiomara Castro Sarmiento wa Jamhuri ya Watu wa Honduras, katika mazungumzo yao, wamejielekeza katika madhara makubwa yanayosababishwa na mabadiliko ya tabianchi, mapambano dhidi ya umaskini wa hali na kipato na umuhimu wa kuendelea kujikita katika kusimamia ustawi, maendeleo na mafao ya wengi, huku umoja na upatanisho wa Kitaifa vikipewa msukumo wa pekee.

Honduras
20 October 2022, 16:33