Askofu mkuu João Carlos Hatoa Nunes Mwandamizi Jimbo kuu la Maputo, Msumbiji
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Baba Mtakatifu Francisko amemteua Askofu mkuu João Carlos Hatoa Nunes kuwa Askofu mkuu Mwandamizi mwenye haki ya kurithi Jimbo kuu la Maputo, Msumbiji. Itakumbukwa kwamba, Askofu mkuu mwandamizi João Carlos Hatoa Nunes alizaliwa tarehe 8 Machi 1968 Jimbo kuu la Beira, Msumbiji. Baada ya masomo na majiundo yake ya Kikasisi, tarehe 17 Julai 1995 akapewa Daraja takatifu ya Upadre kwa ajili ya Jimbo kuu la Maputo, Msumbiji.
Tarehe 25 Mei 2011, Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI akamteuwa kuwa Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu la Maputo na kuwekwa wakfu ili kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu tarehe 10 Julai 2011. Tarehe 12 Januari hadi tarehe 29 Juni 2012 akateuliwa na Baba Mtakatifu Benedikto XVI kuwa Msimamizi wa Kitume wa Jimbo kuu la Beira. Ilikuwa ni tarehe 2 Januari 2017 alipoteuliwa na Baba Mtakatifu Francisko kuwa Askofu wa Jimbo Katoliki la Chimoio, nchini Msumbiji. Tarehe 15 Novemba 2022, Baba Mtakatifu Francisko amemteua Askofu mkuu João Carlos Hatoa Nunes kuwa Askofu mkuu Mwandamizi mwenye haki ya kurithi Jimbo kuu la Maputo, Msumbiji.