Kongamano kuhusu miaka 40 ya Divinus perfectionis magister
Na Angella Rwezaula; – Vatican.
Mnamo tarehe 25 Januari 1983 Mtakatifu Yohane Paulo II katika mwaka wake wa 5 wa Upapa aliandika Katiba ya Kitume iitwayo Divinus Perfectionis Magister yaani Bwana wa Ukamilifu wa Kimungu, kuhusiana na sheria mpya za mchakato wa kuwatangaza watakatifu. Katika hati hiyo inaeleza kwamba Bwana mwenye umungu wa ukamilifu na kielelezo, Kristo Yesu, ambaye pamoja na Baba na Roho Mtakatifu “mtakatifu mmoja”, alilipenda Kanisa kama bibi-arusi akajitoa kwa ajili yake, ili kulitakasa na kulifanya liwe tukufu machoni pake. Kwa hiyo, akiisha kuwapa wanafunzi wake wote agizo, kwamba wauige utimilifu wa Baba, alimtuma Roho Mtakatifu juu ya wote, ili awatie moyo wa ndani, wapate kumpenda Mungu kwa mioyo yao yote, na ili wapendane jinsi yeye anavyowapenda. Wafuasi wa Kristo, kama walivyohimiza kupitia Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican, walioitwa na kuhesabiwa haki katika Yesu Kristo, si kwa kadiri ya matendo yao bali kwa kadiri ya mpango na neema yake, katika Ubatizo wa imani wamefanywa kweli kuwa wana wa Mungu na washiriki wa Umungu asili, na kwa hiyo utakatifu kweli.
Katika muktadha wa kuelekea kumbu kumbu ya miaka 40 tangu kuchapishwa kwa Hati hiyo ya Divinus perfectionis Magister ya Mtakatifu Yohane Paulo II, kuanzia tarehe 9 hadi 11 Novemba 2022, katika Chuo Kikuu cha Kipapa cha Laterano, Baraza la Kipapa la Kuwatangaza Watakatifu pamoja Tume ya Kipapa ya Sayansi za Kihistoria waliandaa na kufanya Kongamono lililoongozwa na Mada “Mitindo ya Utakatifu na kutangazwa Watakatifu baada ya miaka 40 tangu uchapishaji wa Katiba hiyo ya kitume. Katika mchakato wa kongamano hilo mada ya utakatifu iligunduliwa tena katika mtazamo wa taaluma tofauti na kwa kuingilia kati kwa wazungumzaji 30 wakiwemo wanahistoria, wasomi na wataalam kutoka Curia romana. Katibu Msaidizi wa Baraza la Kipapa la Walei Familia na Maisha, Bi Gabriella Gambino alizungumzia juu ya mada ya “Utakatifu na Familia” ambapo kwanza kabisa aliweka wazi jinsi historia ya Kanisa ilivyojaa mifano ya wenzi wa ndoa watakatifu, wazazi watakatifu na familia, na utakatifu wa wanandoa wengi waliotangazwa kuwa watakatifu hadi karne ya 19. Ilikuwa katika karne ya 20 tu ambapo tafakari mpya ya kitaalimungu juu ya ndoa ilipelekea Kanisa kutafakari sana juu ya uwezekano kwamba nafasi ya ndoa inaweza kuwa msingi wa “utakatifu kwa watu wawili”.
Kipengele cha kuvutia kilikuwa ni kwamba sehemu nyingi za familia hizi takatifu bado hazijulikani kwa sehemu kubwa ya ulimwengu leo hii. Sababu msingi ipo katika ukweli kwamba walikuwa “familia” za kawaida, “familia za karibu”, kama Papa Francisko alivyosema katika Wosia wa Gaudete et exsultate,yaani Furahi na Shangilia, kwamba ni ambao hawakufanya mambo ya kushangaza, lakini waliishi kwa urahisi wa maisha yao ya nyumbani, ile njia isiyo ya kawaida na ya kila siku. Akichukua dokezo kutoka katika maandishi yaliyochapishwa na Baraza la Kipapa kuhusu “Utakatifu katika familia za ulimwengu”, Bi Gambino alionesha kwa mifano mbalimbali thabiti jinsi ya utakatifu wa wanandoa hawa ulivyositawi katika hali ya kawaida ya maisha ya familia ambayo inaweza kweli kufanana na familia za leo hii, na matatizo sawa, mahangaiko sawa, shauku sawa ya upendo na maisha ya familia yenye utulivu, inayoelekezwa kwenye utafutaji wa mambo ya kudumu na muhimu, ya pekee ambayo inaweza kutufanya tuwe na furaha. Bila shaka, ni lazima itambuliwe kwamba utakatifu wa wanandoa bado sio sehemu ya hisia za kawaida na ni kipengele kinachopaswa kuchunguzwa kwa tafakari ya kitaalimungu na kwa vitendo vya kichungaji. Si suala la kupendekeza njia ambazo tunaweza, kufafanua kama juu sana au kwa wachache waliochaguliwa, lakini kupendekeza sakramenti ya kuwepo kwa ndoa (...). Katika ngazi ya vitendo vya uchungaji, (...) hatari tunayoendesha ni ile ya kutokuwa na uwezo ili kuwaonesha [vijana] jinsi upendo thabiti ulivyo, ule ulio na mizizi katika mwamba ambao labda ungekuwa upungufu kwa upande wa Kanisa.(...). Kwa hiyo, hatuogopi kuonesha utakatifu wa familia, ambapo unadhihirika, kwa sababu sio tunda la ushujaa ambalo wanadamu tunabeba kama mizigo kwenye mabega ya wenzi wa ndoa Wakristo, lakini ni Upendo ambao Mungu humimina kwa wale wanaotafuta kuwa waaminifu kwake, alihitimisha, Gambino.
Hati hiyo ya Kipapa ya Divinus perfectionis Magister Mwalimu wa Kimungu na Kielelezo cha Ukamilifu, inabainisha kuwa nyakati zote, Mungu huchagua kutoka kwa wengi hawa ambao, wakifuata kwa ukaribu zaidi kielelezo cha Kristo, wanatoa ushuhuda wenye kutokeza kwa Ufalme wa mbinguni kwa kumwaga damu yao au kwa mazoea ya wema wa kishujaa. Kanisa nalo, tangu mwanzo wa Ukristo daima limeamini kwamba Mitume na Mashahidi wameunganishwa nasi kwa ukaribu zaidi katika Kristo na kuwaheshimu, pamoja na Bikira Maria na Malaika watakatifu, kwa ibada ya pekee, wakiwasihi kwa unyenyekevu na msaada wa maombezi yao. Kwa hao waliongezewa upesi wengine pia ambao walikuwa wameiga kwa ukaribu zaidi ubikira na umaskini wa Kristo na, hatimaye, wengine ambao utendaji wao wa kutokeza wa wema wa Kikristo na karama zao za kimungu ziliwapongeza kwa kujitoa uchamungu na kuiga kwa waaminifu.
Mtakatifu Yohane Paulo II anabainisha kwamba tunapofikiria maisha ya wale ambao wamemfuata Kristo kwa uaminifu, tunatiwa moyo na sababu mpya ya kuutafuta Mji unaokuja na tunafundishwa kwa usalama zaidi njia ambayo kwayo, kati ya mabadiliko ya ulimwengu huu na kulingana na hali ya maisha na hali inayofaa kwa kila mmoja wetu, tunaweza kufika kwenye muungano huo mkamilifu na Kristo, ambao ni utakatifu. Tukiwa tumezungukwa na safu kama hiyo ya mashuhuda, ambao kupitia kwao Mungu yuko nasi na kuzungumza nasi, tunavutwa kwa nguvu kuufikia Ufalme Wake mbinguni. Tangu zamani, Vatican imezikubali ishara hizi na imesikiliza sauti ya Bwana wake kwa unyenyekevu na upole mkubwa. Ikiwa mwaminifu kwa jukumu zito alilokabidhiwa la kufundisha, kutakasa na kutawala Watu wa Mungu, anawapendekeza waamini kwa kuwaiga, kuwaomba na kuwaheshimu, wanaume kwa wanawake ambao wamejitokeza katika fahari ya upendo na fadhila nyinginezo za kiinjili, na baada ya hayo, uchunguzi unaostahili, anawatangaza, katika tendo zito la kuwatangaza kuwa watakatifu.
Maelekezo ya mchakato wa sababu za kutangazwa kuwa watakatifu, ambayo Mtangulizi wake Papa Sixtus V alikabidhi kwa Baraza la Kipapa la Kuwatangaza Watakatifu, ambalo yeye mwenyewe alikuwa ameanzisha, yaliboreshwa kila mara kwa kanuni mpya, baada ya muda kupita. Yanayostahili kutajwa kwa namna ya pekee ni yale ya papa Urban VIII,ambayo Prosper Lambertini (baadaye atakuwa Papa Benedict XIV), alitumia uzoefu wa wakati uliopita, kukabidhi kwa vizazi vya baadaye katika kazi yenye kichwa De Servorum Dei beatifιcatione et de Beatorum canonizatione. Kazi hiyo ilitumika kama sheria ya Baraza la Kipapa la Sheria kwa karibu karne mbili. Hatimaye, kanuni hizo zilijumuishwa kwa kiasi kikubwa katika Kanuni ya Sheria ya Kanoni iliyotangazwa mwaka wa 1917.
Kwa kuwa maendeleo ya hivi karibuni katika uwanja wa masomo ya kihistoria yameonesha ulazima wa kulipatia Baraza linalostahiki chombo kinachofaa zaidi kwa kazi yake ili kujibu ipasavyo maagizo ya ukosoaji wa kihistoria, Mtangulizi wake kwa kumbukumbu ya furaha, Papa Pius XI, katika Barua ya Kitume Già da qualche tempo, Motu Proprio, yaani Tayari kwa wakati iliyotolewa mnamo tarehe 6 Februari 1930, ilianzisha "kitenge cha Kihistoria" ndani ya Baraza la Kipapa la Sheria na kuikabidhi uchunguzi wa sababu za "kihistoria". Mnamo tarehe 4 Januari 1939, Papa huyo huyo pia aliamuru kuchapishwa kwa Hati ya Normae servandae katika construeпdis processibus ordinariis super causis historicis, yaani, Kanuni za uhifadhi zimeundwa na michakato ya kawaida kwa misingi ya kihistoria, ambayo ilifanya mchakato wa "kitume" usiwe wa lazima tena bali mchakato mmoja ufanyike kwa mamlaka ya kawaida katika sababu za "kihistoria".
Katika Waraka wa Kitume Sanctitas clarior, yaani Utakatifu ulio wazi Zaidi uliotolewa kama motu proprio mnamo tarehe 19 Machi 1969, Papa Paulo VI alithibitisha kwamba hata katika sababu za karibuni kungekuwapo na mchakato mmoja tu wa utambuzi wa kukusanya uthibitisho, ambao Askofu angefanya kwa idhini ya hapo awali, hata hivyo, kutoka katika Vatican. Papa huyohuyo, katika Katiba ya Kitume Sacra Rituum Congregati, yaani ya Baraza Kipapa la Ibada Takatifu ya tarehe 8 Mei 1969, alianzisha Baraza mbili za Kipapa badala ya Baraza miha la Sheria. Kwa mmoja alioatiwa jukumu lake la kusimamia Ibada ya kimungu na nidhamu ya Sakramenti na nyingine kiwa ni ile ya kushughulikia mchakato wa sababu za kutangwa watakatifu; katika tukio hilo hilo, alibadilisha, kwa kiasi fulani, utaratibu wa kufuatwa katika sababu hizo.
Kwa maana hiyo hati hiyo inabainisha kwamba uzoefu wa hivi karibuni hatimaye, umeonesha manufa ya kurekebisha zaidi namna ya kufundisha mambo na kuunda Baraza la Kipapa kwa ajili ya Mambo ya Watakatifu ili kuweza kukidhi mahitaji ya wataalamu na matakwa ya Ndugu Maaskofu, ambao mara nyingi wameitwa kushiriki katika mchakato rahisi zaidi huku wakidumisha uthabiti wa uchunguzi katika suala ushuhuda mkubwa kama huo. Kwa kuzingatia fundisho la Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican kuhusu ushirikiano, Hati hiyo inabainisha kwamba kuna haja kwamba Maaskofu wenyewe wanapaswa kuhusishwa kwa karibu zaidi na Vatican katika kushughulikia mambo ya watakatifu. Kwa hiyo, baada ya kufuta sheria zote za aina yoyote zinazohusu jambo hilo, tunathibitisha kwamba kanuni hizi zifuatazo zinapaswa kuzingatiwa tangu wakati huo.