Wito Kwa Jukwaa la Kimataifa la Vijana Wakatoliki: Utu, Heshima na Haki Msingi za Binadamu
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Jukwaa la Kimataifa la Vijana Wakatoliki "Forum Internazionale di Azione Cattolica, FIAC., kuanzia tarehe 26-27 Novemba 2022 linafanya mkutano unaohudhuriwa na wanachama kutoka Bara la Amerika, Ulaya, Asia; na Bara la Afrika linawakilishwa na nchi za: Burkina Faso, Burundi, Cameroon, Kenya, Nigeria, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Rwanda, Senegal, Zambia na Zimbabwe. Maadhimisho ya Jukwaa hili yananogeshwa na kauli mbiu: Matendo ya Vijana wa Katoliki: Shauku ya ubinadamu uliopyaishwa katika Kristo Yesu, Jukwaa la Kimataifa la Vijana Wakatoliki. Wakati wa Sinodi; katika ulimwengu uliojeruhiwa; Pamoja na kila mtu na kwa kila mtu. Kardinali Michael Czerny SJ, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Huduma ya Maendeleo Endelevu na Fungamani ya Binadamu amekazia umuhimu wa ujenzi wa utamaduni wa kusikilizana na majadiliano; mawasiliano na hatimaye, marejesho.
Haya ni mahusiano na mafungamano yanayojikita katika udugu wa kibinadamu unaosimikwa katika mapendo kwa Mungu na jirani. Majadiliano yanalenga kutafuta na kuambata ukweli kama sehemu ya mchakato wa kukabiliana na changamoto mamboleo kama vile wimbi kubwa la wakimbizi, wahamiaji na wale wanaotafuta hifadhi ya kisiasa. Kardinali Michael Czerny SJ., anakaza kusema, amani ya kweli inasimikwa katika matumaini; katika msingi wa uchumi fungamani na haki jamii pamoja na kuwa na uwezekano wa kupata na kutumia fursa mbalimbali zinazojitokeza kwa ajili ya kudumisha ikolojia ya mwanadamu pamoja na utunzaji bora wa mazingita nyumba ya wote. Mafungamano ya urafiki wa kijamii ni muhimu sana kwani yanavuka mipaka ya nchi, tamaduni, dini, imani na mafao binafsi, kwa kujenga na kuturubisha uwajibikaji sanjari na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Mambo msingi hapa ni majadiliano, udugu wa kibinadamu, urafiki wa kijamii, kwa ajili ya kumwendeleza mwanadamnu; Kiroho na kimwili.