Askofu Mkuu Fortunatus Nwachukwu:jitihada za jumuiya ya kimataifa ni muhimu!
Na Angella Rwezaula; - Vatican.
Mwakilishi wa Kudumu wa Vatican katika ofisi za Umoja wa Mataifa na mashirika ya kimataifa, huko Geneva, kwenye mada ya majadiliano kwa ngazi za juu ili kutathibimi maendeleo kuongeza kinga, utambuzi na ubashiri wa VVU na TB kwa Watoto. Askofu Mkuu alianza kwa kuwashukuru waandaaji kwa mwaliko wao mzuri wa kujumuika kwenye mkutano huu ulioitishwa ili kupanua dhamira ya mashirika ya kimataifa, serikali, sekta binafsi, asasi za kiraia, viongozi wa dini na taasisi ili kukomesha maafa ya maisha yaliyosababishwa na VVU na TB wakati matibabu madhubuti na utambuzi wa hali hizi sasa zinapatikana katika sehemu zote za ulimwengu. Juhudi zao za awali, kupitia utayarishaji na utekelezaji wa Mpango Kazi wa Roma, tayari zimeongeza utafiti na uundaji wa zana za uchunguzi na dawa ambazo zinaweza kubadilishwa vyema kwa matumizi ya watoto. Hata hivyo, tayari tumesikia changamoto ambazo bado zinahitaji kushughulikiwa, na hivyo amependa kushukuru miundo ya Vatican ambayo iwapatia fursa hii ya kuendeleza mazungumzo na kuweka mikakati ya hatua madhubuti za kiutendaji kufikia malengo yaliyowekwa.
Mada aliyopewa kujadili ni kujitolea kwa Vatican kwa watoto. Dhamira hiyo inatokana na ujumbe wa Injili na mfano wa Yesu ambaye, Yeye mwenyewe akiwa mtoto wa miaka kumi na miwili, alikuwa na ujasiri wa kuwahutubia viongozi wa kidini wa Kiyahudi katika Hekalu la Yerusalemu kuhusu upendo na utunzaji kwa watu wote wa Baba yake wa mbinguni(Lk 2:48-50 ). Wakati wa huduma yake ya umma Yesu aliwaagiza mitume Wake: “Waacheni watoto wadogo waje kwangu… kwa maana Ufalme wa Mungu ni wao” (Mk 10:14). Watoto, hasa watoto wachanga, wanajumuika katika maumbile yao (siyo lazima katika tabia zao, Mt 11:16-17) sifa za kiantolojia zinazoashiria wanafunzi wa kweli wa Yesu, wanaostahili Ufalme wa Mbinguni (upya au kufanywa upya, usafi wa kimwili, uchi au kujitenga, udogo au unyenyekevu, hisia ya kuhusika, utegemezi wa kuaminika au utambuzi wa udhaifu wetu na hitaji la wengine). Yesu pia aliwashirikisha watoto katika mazungumzo na kuangazia akili zao kuhusu hadhi yao ya kipekee kwani wao, kama sisi sote, wameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu.
Askofu Mkuu Fortunatus Nwachukwu aidha alisema tunasoma katika Maandiko Matakatifu kwamba Yesu alikwenda huku na huko akiwaponya wagonjwa na wale waliokuwa katika taabu (Mt 9:35; Mdo 10:38). Jumuiya za kwanza za Kikristo ziliteua mashemasi ili kuwatunza wajane na yatima miongoni mwao (Mdo 6:1-7), na desturi hii hatimaye ilipelekea Kanisa kuanzisha miundo mbalimbali ya malezi ili kuwahudumia washiriki walio katika mazingira magumu zaidi ya binadamu, familia, bila kujali kabila, utaifa, rangi, au uhusiano wa kidini; kwa hakika, miongoni mwa waliopewa kipaumbele zaidi kwa matunzo hayo ni watoto, hasa wagonjwa na/au wale ambao hawajalindwa na wazazi wa kibaiolojia au walezi. Ripoti ya Ofisi ya Takwimu ya Vatican 2022 inakadiria karibu hospitali na zahanati 20,000, nyingi zikiwa na huduma maalum za uzazi na watoto, pamoja na huduma zingine 20,000 za malezi ya watoto chini ya usimamizi wa miundo ya Kanisa Katoliki katika kila kanda ya Dunia.
Baadhi ya majengo kama hayo yaliibua wito wa wazi wa zana za uchunguzi na dawa zinazofaa zaidi na zinazoweza kufikiwa kwa urahisi na nafuu kwa ajili ya matunzo ya VVU na TB kwa watoto na hii ilisababisha Mpango Kazi ambao tunauzungumzia leo. Kwa hadhi yake ya Mwakilisho katika Shirika la Umoja wa Mataifa na uanachama wake kamili katika baadhi ya Mashirika Maalumu, Vatican ilikuwa mojawapo ya nchi zilizotia saini Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Haki za Mtoto. Katika ripoti zake kwa Kamati ya Haki za Mtoto, Askofu Mkuu Fortunatus Nwachukwu amebainisha kwamba Vatican imetoa kipaumbele kwa mahitaji ya afya ya watoto, ikiwa ni pamoja na yale yanayohusiana na VVU na TB kwa watoto. Utume wa uwakilishi wa Kudumu wa Vatican huko Geneva umefuatilia kwa karibu sana juhudi zilizopelekea Mpango Kazi wa Roma. Mnamo mwaka wa 2018, Shirika la Mfuko wa Caritas in Veritate, ambao linahusishwa kwa karibu na Utume huko Geneva, lilichapisha karatasi ya kina ya Upatikanaji wa Madawa, Tafakari ya Maadili juu ya Kukomesha kwa VVU kwa Watoto, pamoja na michango ya kitaalamu kutoka kwa washiriki wengi wa Mazungumzo ngazi za juu.
Papa Francisko, na watangulizi wake, wamedumisha hitaji la Mataifa kuheshimu haki ya afya na matibabu, kama ilivyojumuishwa ndani ya marudio ya jumla zaidi ya haki ya kufurahia kiwango cha maisha cha kutosha, katika Azimio Ulimwengu la haki za Binadamu. Utume mbalimbali wa Vatican katika Umoja wa Mataifa na mashirika mengine ya kimataifa huchukua kila nafasi kuzungumzia wajibu huo wakati wa mikutano ya serikali mbalimbali inayohusiana na afya, biashara, hati za malimiliki na maendeleo. Kwa maana hiyo Askofu Mkuu Fortunatus Nwachukwu alisema ni vema basi kutumaini kwamba mazungumzo haya ya sasa yataanzisha upya na kuimarisha azimio lao la kutoa utambuzi wa mapema na matibabu kwa watoto wanaoishi na VVU na TB na kuzuia maambukizi hayo kwa kutoa matibabu sawa kwa wanawake wajawazito. Na maneno haya ambayo Papa Francisko aliyahutubia mapema mwaka huu 2022 kwa Kikosi cha Wanadiplomasia kilichoidhinishwa na Vatican yanaweza kuwa msaada katika kuongoza mazungumzo yenu: “kujitolea kwa kina kwa upande wa jumuiya ya kimataifa ni muhimu, ili kwamba idadi ya watu duniani iweze kuwa na upatikanaji sawa wa huduma muhimu za matibabu na chanjo ... Narudia ombi langu kwamba serikali na taasisi za kibinafsi zinazohusika zioneshe hisia ya uwajibikaji, zikitengeneza majibu yaliyoratibiwa katika kila ngazi (ya mtaa, kitaifa, kikanda, kimataifa), kupitia miundo mipya ya mshikamano na zana ili kuimarisha uwezo wa nchi hizo zenye uhitaji mkubwa zaidi.”