Tafuta

Kardinali Cantalamessa Mahubiri yake katika Kipindi cha Majilio kwa Mwaka 2022 yanajikita katika fadhila za Kimungu yaani: Imani, Matumaini na Mapendo.  Ameanza na Imani Kardinali Cantalamessa Mahubiri yake katika Kipindi cha Majilio kwa Mwaka 2022 yanajikita katika fadhila za Kimungu yaani: Imani, Matumaini na Mapendo. Ameanza na Imani 

Mahubiri ya Kipindi cha Majilio Mwaka 2022: Fadhila ya Imani

Kardinali Raniero Cantalamessa kwa muhtasari amefafanua: Fadhila za Kimungu, Kristo Yesu asili na utimilifu wa fadhila ya imani, changamoto za maendeleo ya sayansi na teknolojia, lakini mwenye haki ataishi kwa imani yake. Fadhila za Kimungu: Imani, Matumaini na Mapendo ni tunu ambazo Mamajusi kutoka Mashariki ya mbali walizichukua ili kumpelekea Mtoto Yesu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Kardinali Raniero Cantalamessa, Mhubiri wa nyumba ya Kipapa katika kipindi cha Majilio anasema, mahubiri yake katika Kipindi cha Majilio kwa Mwaka 2022 yanajikita katika fadhila za Kimungu yaani: Imani, Matumaini na Mapendo. Mahubiri haya yananogeshwa na kauli mbiu “Inueni vichwa vyenu, enyi malango, Inukeni, enyi malango ya milele, Mfalme wa utukufu apate kuingia. Ni nani Mfalme wa utukufu? BWANA mwenye nguvu, hodari, BWANA hodari wa vita.” Zab 24: 7-8. Kardinali Raniero Cantalamessa katika mahubiri yake, Ijumaa tarehe 2 Desemba 2022, kwa muhtasari amefafanua kuhusu fadhila za Kimungu, Kristo Yesu asili na utimilifu wa fadhila ya imani, changamoto za maendeleo ya sayansi na teknolojia, lakini mwenye haki ataishi kwa imani yake. Fadhila za Kimungu yaani: Imani, Matumaini na Mapendo ni tunu ambazo Mamajusi kutoka Mashariki ya mbali walizichukua vibindoni mwao ili kumpelekea Mtoto Yesu, yaani: Dhahabu, Uvumba na Manemane. Hizi ni fadhila muhimu sana katika Kipindi hiki cha Majilio, waamini wanapoinuka tayari kumfungulia Kristo Yesu malango ya maisha yao, ili aweze kuingia.

Tafakari Kipindi cha Majilio Mwaka 2022: Imani
Tafakari Kipindi cha Majilio Mwaka 2022: Imani

Mlango huu ni imani, mwaliko kwa waamini kumfungulia malango ya maisha yao, ili kweli Kristo Yesu aweze kuingia kama alivyowahi kusema Mtakatifu Yohane Paulo II, jambo la msingi ni kuombea msaada wa Mungu na mwamini kushirikiana kikamilifu na Mwenyezi Mungu ili kufungua malango ya maisha. Imani ni fadhila ambayo imetajwa sana kwenye Maandiko Matakatifu wakati wa majaribu na utimilifu wake ni Kristo Yesu mwenye kuanzisha na mwenye kutimiza imani hiyo ambayo imekuwa ni chanzo cha wokovu kwa watu wengi. Rej. Ebr 12: 2. Hii ni imani inayopyaisha maisha baada ya kutangazwa na kushuhudiwa. Hii ni imani inayokuja baada ya mtu kusikiliza “fides ex auditu” na maamuzi haya yanapitia katika moyo wa mtu anayeamini “Corde creditur” na hatimaye, katika midomo ya mwamini anayekiri imani hiyo “Ore fit confessio” na hatimaye, kuimwilisha katika uhalisia wa maisha kama kielelezo cha imani tendaji. Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican wanawahimiza Wakristo kwa busara na mapendo kwa njia ya majadiliano ya kidini na kiekumene pamoja na ushirikiano na dini nyinginezo watoe ushuhuda wa imani na wa maisha ya Kikristo, na tena watambue, wahifadhi na kukuza mema ya kiroho na ya kimaadili; na tunu za kijamii na za kitamaduni, ambazo zinapatikana kati ya wale ambao si Wakristo. Rej. Nostra aetate, 2.

Ushuhuda wa imani: Majadiliano ya kidini na kiekumene
Ushuhuda wa imani: Majadiliano ya kidini na kiekumene

Kristo Yesu ametumwa na Baba wa milele na kwa njia yake, watu wote wapate wokovu. Hawa ni wale wanaomtafuta kwa moyo mnyofu na kama ilivyokuwa kwa watoto mashuhuda waliouwawa na Mfalme Herode aliyekuwa anamtafuta Mtoto Yesu kati yao. Imani kwa Kristo Yesu ni chanzo cha wokovu. Uinjilishaji unaotekelezwa na Mama Kanisa katika mapambazuko ya Millenia ya tatu ya Ukristo unajikita katika mchakato wa majadiliano ya kiekumene na kidini ili kujenga na kudumisha: utu, heshima, haki msingi za binadamu, ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu katika ujumla wao. Baba Mtakatifu Francisko anakazia uekumene wa: damu, maisha ya kiroho, sala na huduma kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Ikumbukwe kwamba, uekumene wa utakatifu wa maisha unafumbatwa katika toba na wongofu wa ndani; kwa kujikana na kujivika fadhila ya unyenyekevu; moyo wa ukarimu na udugu; upole, uvumilivu na kutumikia bila ya kujibakiza. Wakristo wanakumbushwa kwamba, kadiri wanavyojitahidi kuishi maisha matakatifu mintarafu Injili, ni kwa kadiri ile ile wataweza kuhamasishana kutekeleza mchakato wa ujenzi wa umoja wa Wakristo na udugu kati yao. Uekumene wa damu unajikita katika ushuhuda wa imani kwa Kristo Yesu na Kanisa lake.

Kumekuwepo na maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia
Kumekuwepo na maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia

Katika mapambazuko ya Karne ya Ishirini na Moja, kumekuwepo na maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia, matendo makuu ya Mungu katika maisha ya mwanadamu. Tafakari hizi ni kwa ajili ya kuwaimarisha waamini katika imani, matumaini na mapendo thabiti, ili hatimaye, wapate kujua hakika ya mambo waliyofundishwa. Rej. Lk 1:4. Mtume Paulo anakaza kusema, “Kwa kuwa katika yeye vitu vyote viliumbwa, vilivyo mbinguni na vilivyo juu ya nchi, vinavyoonekana na visivyoonekana; ikiwa ni vitu vya enzi, au usultani, au enzi, au mamlaka; vitu vyote viliumbwa kwa njia yake, na kwa ajili yake. Naye amekuwako kabla ya vitu vyote, na vitu vyote hushikana katika yeye.” Kol 1:16-17. Hii ni furaha inayopatikana baada ya kuamini. Kardinali Raniero Cantalamessa anasema mwenye haki ataishi kwa imani yake hata katika madhulumu, nyanyaso na mateso kutoka kwa wadhalimu dhidi ya mwadilifu kama ilivyo wakati huu wa vita kati ya Urusi na Ukraine. Mwenyezi Mungu daima ni mwenye Haki na Mtakatifu na kamwe hataruhusu udhalimu uwe na neno la mwisho katika maisha ya waja wake.

Mwenye haki ataishi kwa imani yake
Mwenye haki ataishi kwa imani yake

Katika muktadha huu, Mama Kanisa hana budi kuwa ni sauti ya maskini na wanyonge katika jamii bila kuwasahau wote wanaoteseka kutokana na vita sehemu mbalimbali za dunia na wala hakuna sababu ya kuwa na vita ya kidini, ndiyo maana dini zinapaswa kuwa ni vyombo na mashuhuda wa haki, amani na maridhiano kati ya watu. Jambo la msingi kwa waamini ni kuhakikisha kwamba, wanaishi kadiri ya imani yao. Leo hii dhamana ya imani imekuwa finyu kiasi kwamba kwa wanandoa imani yao imebaki ikining’inia kwenye kidole cha pete ya ndoa. Roma iliyokuwa kuwa inajulikana kama kama mji mkuu ulimwenguni, “Caput mundi”, leo hii umebaki “Caput fidei” mji mkuu wa imani katika uhalisia na uthabiti wake. Imani inapaswa kutangazwa na kushuhudiwa na wengi kwa kuendelea kujiaminisha chili ya Mungu. Waamini wajiandae kikamilifu kwenda kumlaki Kristo Yesu kwa imani kama sehemu ya utimilifu wa unabii.

Kardinali Imani
02 December 2022, 16:18