Vatican News na mapya hata “YouTube Shorts”!
Na Angella Rwezaula- Vatican.
Intaneti ni kama Jukwaa jipya la kutangaza Injili. Ndicho kilikuwa kichwa cha Ujumbe wa Mtakatifu Yohane Paulo II mnamo mwaka 2002 katika Siku ya XXXVI ya Mawasiliano Duniani. Baba Mtakatifu wakati ule aliwaalika Wakatoliki wote duniani kutumia mtandao wa intaneti, ambayo ilikuwa ni njia changa ya wakati huo, kueneza Neno la Mungu. Tarehe 12 Desemba 2012, Papa Mstaafu Benedikto XVI alifungua akaunti ya @Pontifex kwa tweet yake ya kwanza. Papa Francisko, ambaye ameeleza kwamba mtandao ni zawadi kutoka kwa Mungu, ndiye Papa wa kwanza kuwa na akaunti ya Instagram.
Kwa maana hiyo baada ya Facebook, Instagram na Twitter, vyombo vya habari vya Vatican sasa vinatua kwenye ‘YouTube Shorts’ambalo ni jukwaa la kijamii zaidi la Google. Kutokana na hilo bado kutakuwa na maudhui katika lugha nne: Kiingereza, Kihispania, Kireno na Kiitaliano. ‘Shorts’ ambazo ni video za muda usiozidi sekunde sitini, katika muundo wa wima, unaoweza kutumika kupitia simu za mkononi mahiri(smartphone). Vatican News itakuwa inachapisha nne kwa juma, katika jukwaa hilo pekee la YouTube. Ikiwa bado hujawa mshiriki wa jumuiya yetu, jiandikishe hapa: iscriviti al nostro canale YouTube Vatican News!