Askofu Bob John Hassan Koroma wa Jimbo Katoliki Makene, Sierra Leone
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Katika Maadhimisho ya Siku ya 31 ya Wagonjwa Duniani, sanjari na Kumbukumbu ya Bikira Maria wa Lourdes, Baba Mtakatifu Francisko amemteuwa Mheshimiwa sana Padre Bob John Hassan Koroma kuwa Askofu mpya wa Jimbo Katoliki la Makeni, nchini Sierra Leone. Kabla ya uteuzi huu, Askofu mteule Bob John Hassan Koroma alikuwa ni Makamu Askofu Jimbo Katoliki la Makeni. Itakumbukwa kwamba, Askofu mteule Bob John Hassan Koroma alizaliwa tarehe 17 Novemba 1971 huko Kamabai. Baada ya masomo na majiundo yake ya Kikasisi, tarehe 25 Aprili 1999 akapewa Daraja Takatifu ya Upadre kwa ajili ya Jimbo Katoliki la Makeni, nchini Sierra Leone.
Baadaye alitumwa na Jimbo lake kujiendeleza zaidi katika Sayansi ya Maandiko Matakatifu kwenye Taasisi ya Biblia na hatimaye, kujipatia Shahada ya Uzamivu kwenye Taalimungu ya Maandiko Matakatifu, kutoka Chuo Kikuu cha Kipapa cha Urbaniana, Roma. Katika maisha na utume wake, amekuwa mshiriki mzuri wa kuandaa tafakari za Neno la Mungu Radio Vatican, Jalimu wa Maandiko Matakatifu na Dekano wa Masomo Seminari kuu ya “St. Paul” iliyoko mjini Freetown kati ya mwaka 2008 hadi mwaka 2014. Ameshiriki kutoa huduma huko “St. Catherine of Siena na Little Compton pamoja na St. Madeleine” huko mjini Tiverton nchini Marekani kati ya mwaka 2005 hadi mwaka 2013. Kuanzia mwaka 2015 akateuliwa kuwa Makamu Askofu Jimbo Katoliki la Makene na kuanzia mwaka 2016 akateuliwa kuwa Msimamizi wa Kanisa kuu la Jimbo Katoliki la Makene. Tarehe 11 Februari 2023 Baba Mtakatifu Francisko akamteuwa kuwa Askofu mpya wa Jimbo Katoliki la Makene nchini Sierra Leone.