Papa atafanya ziara ya Kitume huko Hungaria Aprili,28-30
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Katika ziara ya kitume hiyo ikumbukwe kwamba mnamo tarehe 12 Septemba miaka miwili iliyopita alikuwa ametua na kusimama hapo kwa muda wa saa saba tu, muda ambao ulikuwa ni kuongoza Misa kwa ajili ya kuhitimisha Kongamano la Ekaristi Takatifu la Kimataifa na kuwa na mikutano kadhaa na Maaskofu mahalia, pamoja na wawakilishi wa Baraza la Kiekumene la Makanisa na baadhi ya jumuiya za Wayahudi, kabla ya kuchukua tena ndege kurudi Slovakia, katika hatua ya pili ya ziara yake hiyo ya kitume. Kwa hiyo sasa Papa Francisko atarudi Hungaria ili kukumbatia nchi nzima na jumuiya yake ya kikanisa. Kwa mujibu wa Ofisi ya Vyombo vya Habari vya Vatican, Dk. Matteo Bruni ametangaza Jumatatu tarehe 27 Februari 2023, mpango wa ziara ambayo Papa Francisko ataifanya katika ardhi kuanzia Ijumaa tarehe 28 hadi Dominika 30 Aprili 2023.
Ratiba ya ziara ya Baba Mtakatifu jijini Budapest
Katika ziara yake ya kitume Baba Mtakatifu anatarajia kuondoka kwa ndege katika Uwanja wa Kimataifa wa Fiumicino, majira ya saa 2.10 asubuhi Ijumaa tarehe 28 Aprili na takriban saa mbili baadaye Baba Mtakatifu Francisko atatua katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Budapest. Saa moja baadaye, saa 5.00, itakuwa wakati wa kukaribishwa rasmi katika uwanja wa Jumba la ‘Sándor’, ambayo ni makazi ya rais wa Hungaria, Bi Katalin Éva Novák. Kufuatia na mikutano ya itifaki itakuwa ni mkuu wa nchi, Waziri Mkuu Viktor Orban na mamlaka na wawakilishi wa mashirika ya kiraia na mashirika ya kidiplomasia. Siku hiyo itafungwa saa kumi na moja jioni ambapo Papa atakutana na wakleri, watawa na waseminari katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Stefano.
Jumamosi 29 Aprili 2023
Asubuhi ya siku ya pili, Jumamosi 29 Aprili, itakuwa na utimilifu wake wa nyakati mbili kati ya zile zinazosubiriwa kila wakati kwa hamu maalum na Papa, ni ziara ya kibinafsi ya faragha saa 2.45 kwa watoto vipofu ambao ni wageni wa taasisi ya Mwenyeheri László Batthyány-Strattmann iliyopewa jina la daktari wa macho wa Hungaria wakati wa kutangazwa mwenyeheri mnamo mwaka 2003, ikifuatiwa na mkutano na maskini na wakimbizi katika Kanisa la Mtakatifu Elizabeth wa Hungaria. Pia kutakuwa na mikutano mingine miwili alasiri, saa 10.30 jioni, wa mkutano na vijana katika jengo la mchezo la László Papp Budapest na saa 12.00 jioni katika Ubalozi wa Vatican nchini humo, mkutano wa faragha na wanashrika wa Shirika Kijesuit.
Dominika 30 Aprili 2023
Dominika tarehe 30 Aprili 2023 ratiba inaonesha kuwa itakuwa wakati wa maadhimisho ya Misa Takatifu, ambayo Baba Mtakatifu Francisko ataongoza kuanzia saa 3.30 asubuhi katika Uwanja wa Kossuth Lajos kwa kuhitimishwa na Sala ya Malkia wa Mbingu, na baadaye alasiri saa 10.00, kutakuwa na mkutano wa mwisho na wawakilishi wa ulimwengu wa chuo kikuu na utamaduni kabla ya kuondoka kurudi Vatican. Kwa hiyo anatarajiwa kuruka na ndega saa 12.00 jioni na kuwasili Roma katika Uwanja wa Ndege wa Fiumicino saa 1.55 za usiku.