Tafuta

Wakimbizi wanapaswa kukaribishwa, kulindwa, kuhamasishwa na kuunganishwa katika jumuiya zinazowapokea. Wakimbizi wanapaswa kukaribishwa, kulindwa, kuhamasishwa na kuunganishwa katika jumuiya zinazowapokea.  (ANSA)

Askofu Mkuu Nwachukwu:kuna udharura wa kupiga vita ubaguzi wa rangi

Tamko la Askofu Mkuu Fortunatus Nwachukwu,Mwakilishi wa Kudumu wa Baraza Kuu kwa Umoja wa Mataifa na Mashirika Mengine ya Kimataifa huko Geneva katika Mkutano wa 52 wa Mjadala wa Baraza la Haki za Kibinadamu katika kuadhimisha Siku ya Kimataifa ya Kutokomeza Ubaguzi wa Rangi tarehe 29 Machi 2023.

Na Angella Rwezaula, - Vatican.

Kwa kuwa mwaka huu unaadhimisha miaka 75 tangu kupitishwa kwa Tamko la Kimataifa la Haki za Binadamu, ni vyema Baraza hili likapitia hatua iliyofikiwa na changamoto zinazokabili kutokomeza ubaguzi wa rangi pamoja na athari zake katika kukuza na kulinda binadamu na haki zake. Alisema hayo Askofu Mkuu Fortunatus Nwachukwu, Mwakilishi wa Kudumu  wa Baraza Kuu kwa Umoja wa Mataifa na Mashirika Mengine ya Kimataifa huko Geneva katika Mkutano wa 52 wa Mjadala wa Baraza la Haki za Kibinadamu,  tarehe 29 machi 2023 katika kuadhimisha Siku ya Kimataifa ya Kutokomeza Ubaguzi wa Rangi ikiongozwa na mada: “Udharura wa kupiga vita ubaguzi wa rangi katika miaka 75 baada ya kupitishwa kwa Azimio la Kimataifa la Haki za Kibinadamu.

Ubaguzi ni virusi vibaya zaidi ya Uviko-19

Askofu Mkuu ambaye hata hivyo meteuliwa hivi karibuni na Papa kuwa Katibu Mkuu wa Baraz ala Uinjilishaji kitengo cha Makanisa mapya alisema Ingawa bila shaka mafanikio yamepatikana katika juhudi za kimataifa za kuondoa ubaguzi wa kila aina, inakatisha tamaa kuona ni matukio mangapi ya wasifu na ubaguzi wa rangi bado yapo, licha ya taratibu za ulinzi wa kitaifa na kimataifa, hali hizi za ubaguzi wa rangi zinaendelea kutuaibisha, kwa kuwa zinaonesha kwamba maendeleo yetu ya kijamii si ya kweli au ya uhakika kama tunavyofikiri. Mbaya zaidi kuliko janga la UVIKO-19, ni ubaguzi wa rangi ambao  ni virusi ambavyo hubadilika haraka na, badala ya kutoweka, hujificha, na kuvizia.

Wakimbizi wanapaswa kukaribishwa na kuunganishwa

Askofu Mkuu Nwachukwu amebainisha kuwa Cha kusikitisha ni kwamba katika njia mbalimbali za wahamaji tumeona matukio ya ubaguzi wa rangi huku wahamiaji na wakimbizi wakati mwingine wakitendewa isivyo haki na maafisa wa doria mpakani, mashirika ya misaada ya kibinadamu na jumuiya zinazowapokea. Kwa njia hiyo, watu hawa, ambao wengi wao tayari wanateseka na ugumu wa vita, pia wanakabiliwa na ubaguzi kutokana na rangi ya ngozi zao. Bila shaka, wakimbizi wanapaswa kukaribishwa, kulindwa, kuhamasishwa na kuunganishwa katika jumuiya zinazowapokea, bila kujali rangi zao, jinsia, nchi ya asili, utamaduni au dini na kamwe wasichukuliwe kama mzigo.

Vatican katika mapambano dhidi ya ubaguzi

Kwa njia hiyo Askofu Mkuu Nwachukwu alisema Vatican  inajali hasa aina mpya na ya hila ya ubaguzi ambayo mara nyingi inahusiana na rangi na hasa utamaduni wa jadi, jambo ambalo Papa Francisko amelishutumu kama ukoloni wa kiitikadi. Badala ya kuheshimu maadili na tamaduni za wakazi wa huko, baadhi ya nchi za Magharibi hulazimisha itikadi zao kwa nchi kutoka Kusini mwa Ulimwengu, wakati fulani zikizuia usaidizi wa kifedha na misaada ya kibinadamu isipokuwa nchi hiyo ikubali na kutekeleza misimamo yao. Ingawa mazungumzo ya kweli kuhusu maadili na mitazamo tofauti yanapaswa kukaribishwa kila mara, hakuna nchi inayopaswa kulazimishwa kuchagua kati ya kuacha maadili yake yenyewe au kukataa uungwaji mkono wa kimataifa, ambao ni muhimu kwa ajili ya kukuza manufaa ya wote katika nchi zinazoendelea.

Hotuba ya Askofu Mkuu Nwachukwu dhidi ya Ubaguzi
31 March 2023, 17:57