Upeo wa udugu kwa mabadiliko ya dhana katika Kanisa na ulimwengu
Na Angella Rwezaula- Vatican.
Askofu Mkuu Vincenzo Paglia, rais wa Chuo cha Kipapa cha Maisha na Kansela mkuu wa Taasisi ya Kipapa ya Yohane Paulo wa Pili, alitambulisha uwasilishaji wa kitabu chenye kichwa: “Kuanzia kwa Wengi. Upeo wa mawazo ya kidugu”, kilichochapishwa na LEV na kuhaririwa na mtaalimungu Monsinyo Pierangelo Sequeri. Kwa hiyo katika hotuba yake Askofu Mkuu Paglia alisema “Tuna jukumu mikononi mwetu kutoka nje ya maboma yetu ya kawaida. Sio suala la kwenda kwenye ua tofauti, ni lazima, kinyume chake, tuache ua wote ili kwenda kila mahali kujenga udugu.” Kitabu hiki ni sehemu ya Mpango wa ‘Salvare la Fraternità–Insieme, yaani “Tuokoe Udugu–Pamoja“, uliozinduliwa mwezi Juni 2011 kwa kuchapishwa kwa wito kwa ajili ya wanaume na wanawake wa wakati wetu uliofafanuliwa na kundi la wataalimungu kumi wakiratibiwa na Askofu Mkuu Paglia na Monsinyo Sequeri wenyewe. Kwa hiyo kitabu kinakusanya michango kumi inayotoa maoni juu ya Wito huo. Uwasilishaji wa kitabu hicho ulifanyika mchana tarehe 27 Machi 2023 katika ukumbi wa Marxoni kwenye Jengo la Pio ambalo ni makao makuu ya Radio Vatican, kwa ushiriki wa Kadinali wa Luxembourg Jean-Claude Hollerich, rais wa zamani wa COMECE na mratibu Mkuu wa Sinodi ya Maaskofu. Pia alinganishwa kutoka New York, mwanauchumi Mariana Mazzuccato, mjumbe wa Chuo cha Kipapa cha Maisha.
Wito wa Papa: pumzi ya udugu inadhoofika
Askofu Mkuu Paglia ambaye alitia saini utangulizi wa kitabu alisisitiza kwamba kitabu hicho kinajibu wito ambao Papa alitoa unabii kwa Chuo hicho wakati wa maadhimisho ya miaka 25 ya kundwa kwake. Pumzi ya udugu inaonekana kudhoofika sana, ilikuwa ni uchunguzi wa Papa, akiamini kwamba udugu ndio na ungekuwa mpaka mpya wa Ukristo. “Vita ni kinyume kabisa, alisema Askofu Paglia ambaye alieleza jinsi baada ya muda kundi la wataalimungu liliundwa ambalo walitafakari juu ya maisha kwa maana pana sana, zaidi ya masuala madhubuti ya kibiolojia. “Tukikabiliwa na hatari inayokaribia kwamba ubinadamu unaweza kujiangamiza yenyewe kwa nguvu za nyuklia, na athari kwa tabianchi, na teknolojia mpya, tunahisi muungano wa haraka kati ya wasomi wa maarifa ya kidini na wasomi wa maarifa ya kisayansi”. Kwa kuongeza Askofu Mkuu Paglia alisema “Inashangaza kwamba msaada kwa vita unakuja zaidi kutoka kwa serikali kuliko kutoka kwa watu, ingawa watu wanahisi kashfa ya vita hivi”.
Hollerich: kugundua tena msingi wa kawaida wa mwanadamu
Naye Kadinali Jean-Claude Hollerich, rais wa zamani wa Comece, alitamka kwamba “ Kanisa lazima lifanye mabadiliko ya dhana. Mahubiri yetu hayaeleweki tena kwa watu. Usekula unaendelea kwa kasi, hasa katika Benelux, lakini pia nchini Italia. Ukristo unazidi kuwa dhaifu. Watu wanapendezwa na Injili, na wanataka Kanisa linalotenda kama Yesu.” Kardinali wa Luxembourg alizingatia mfano wa Msamaria mwema unaofungua waraka wa Fratelli tutti kwamba: “Tuna hatari ya kukengeushwa”. Kwa hiyo ushauri wake ni kwenda kwa vijana ambao wamehudhuria katekisimu lakini hawaamini kwa sababu wanaona ulimwengu uliovunjika, wenye ubinafsi una nguvu. “Hawatuoni kama suluhisho, lakini kama sehemu ya shida: dini hazizingatii masuala ya ulimwengu, kwa sababu zinapigana vita. Ni lazima basi tugeuke ili kusaidia wanaume na wanawake waliojeruhiwa,” Kardinali Hollerich alitoa mwalino. “Tunapomtunza mtu yeyote, awe Myahudi au Mbudha, basi vijana hututhamini. Hata pale ambapo hakuna dini (tena), lazima tugundue upya misingi ya kawaida ya binadamu, vinginevyo maneno yetu ya 'dini' hayana maana tena”, Kardinali Kama Mjumbe Mkuu wa Baraza Kuu la XVI la Kawaida la Sinodi ya Maaskofu, alisisitiza pia kwamba sinodi ndiyo njia hasa ya kutufanya tubadilike, kwa sababu kwa kusikilizana, mambo yanaweza kubadilika. Hakika, sinodi inaonesha “si ulimwengu unaokula ibada bali ulimwengu katika mazungumzo. Hatupaswi tena kujibu maswali ambayo hakuna mtu anayetuuliza bali kusikiliza na kisha kukusanyika kwa sababu ubinadamu unatuhitaji sisi sote. Uongofu kwa ubinadamu daima ni uongofu kwa Mungu”, alihitimisha.
Sequeri: kukaa kwa umati
Mtaalimungu Monsinyo Pierangelo Sequeri alianza kwa uchochezi kwamba taalimungu lazima iwindwe: “Hatujui imeenda wapi: ilianza kuwekwa chumbani Mungu alipoanza kuwa mada ya upendeleo. Leo ni hivyo. Moyo wa usemi wake unategemea hasa wazo la kidugu ambalo limeegemezwa hasa juu ya shauku ya kutomtaka Mungu, jaribio lililoenea. “ Taalimungu kwa hiyo lazima ifanye kila kitu kushawishi kwamba hakuna chama cha Mungu, lazima isambaze mtazamo huu. Mungu hana chama, siku akitakiwa kuwa na chama, asingekuwa Mungu tena”. Katika upeo wa mawazo ya kidugu pia kuna maana ya utayari wa kuishi na wale walio tofauti na wao wenyewe. “Kimsingi ni makazi ya Yesu ni kanuni ya Kanisa tunayopokea kutoka kwa Yesu. Na akamalizia kwa uhakikisho ambao pia ni onyo kuwa “Si suala la idadi ya miito ya ukuhani, ambayo kwa kawaida hufikiriwa kuwa haitoshi, bali ya kuitumia vizuri. Ni suala la kukaa katika umati. Na kukaa pamoja na wanafunzi tu Kanisa halijengwi. Kwa umati tu kanisa halijengwe bali linajengwa kweli kwa Pamoja", alihitimisha Monsinyo Sequeri.