Tafuta

Siku ya 60 ya Kuombea Miito Duniani: Shirika la Mabinti wa Maria Msaada wa Wakristo: Le Figlie di Maria Ausiliatrice Siku ya 60 ya Kuombea Miito Duniani: Shirika la Mabinti wa Maria Msaada wa Wakristo: Le Figlie di Maria Ausiliatrice 

Siku ya Kuombea Miito 2023: Shirika la Mabinti wa Maria Msaada wa Wakristo

Tunafahamika kama Masista Wasalesian wa Mtakatifu Yohane Bosco. “Salesian Sisters; au Daughters of Mary Help of Christians, F.M.A”; Hili ni Shirika lililoanzishwa tarehe 5 Agosti 1872 huko nchini Italia na Mtakatifu Yohane Bosco pamoja na Mtakatifu Maria Domenica Mazzarello, ili kutoa elimu kwa wasichana hasa wale wenye uhitaji lengo likiwa kuakisi shirika la Mapadre Wasalesiani waliokuwa wameanziswa kuwahudumia vijana wa kiume huko Valdoco-Torino! Miito Itika!

Na Sr. Sofia Gura, FMA., - Roma.

Ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko wa Siku ya 60 ya Sala Kwa Ajili ya Kuombea Miito ndani ya Kanisa kwa Mwaka 2023 unanogeshwa na kauli mbiu: Wito: Neema na Utume.” Huu ni mwaliko wa kutafakari kwamba, watu wameumbwa, wa upendo, kwa ajili ya upendo na kwa upendo. Mimi ni utume katika dunia hii, hiyo ndiyo sababu ya kuwepo kwangu mimi katika ulimwengu, kuwa pamoja na wengine na kwa ajili ya wengine. Tunaitwa kuwa wamoja ili kuunda jumuiya ya wamisionari mitume kwa ajili ya kutangaza na kushuhudia upendo kwa ajili ya wengine kwa kutambua kwamba, neema na utume ni zawadi na dhamana. Kama sehemu ya maadhimisho ya Siku ya 60 ya Kuombea Miito Duniani, leo katika makala haya, tutasikia historia ya Shrika la Masista Wasalesian wa Mtakatifu Yohane Bosco; Karama na Utume wao na hatimaye, uwepo wao sehemu mbalimbali za dunia. Baba Mtakatifu Francisko katika Wosia wake wa Kitume Furaha ya Injili, “Evangelii gaudium” anasema, furaha ya Injili huijaza mioyo na maisha ya wote wanaokutana na Kristo Yesu. Wale wanaoikubali zawadi yake ya ukombozi wanawekwa huru kuondokana na dhambi, uchungu, utupu wa ndani na upweke. Pamoja na Kristo Yesu, daima furaha inazaliwa upya.” Evangelii gaudium, 1. Tunafahamika kama Masista Wasalesian wa Mtakatifu Yohane Bosco. “Salesian Sisters; au Daughters of Mary Help of Christians, F.M.A”; Hili ni Shirika lililoanzishwa tarehe 5 Agosti 1872 huko nchini Italia na Mtakatifu Yohane Bosco pamoja na Mtakatifu Maria Domenica Mazzarello, ili kutoa elimu kwa wasichana hasa wale wenye uhitaji lengo likiwa kuakisi shirika la Mapadre Wasalesiani waliokuwa wameanziswa kuwahudumia vijana wa kiume huko Valdoco-Torino.

Shirika Lilianzishwa tarehe 5 Agosti 1872
Shirika Lilianzishwa tarehe 5 Agosti 1872

Asili ya shirika letu ni kutoka ndani ya moyo na akili ya Mtakatifu Yohane Bosco na kwa uaminifu na ubunifu wa Mtakatifu Maria Domenica Mazzarello pamoja na Masista wa kwanza ambao walitimiza nia ya Don Bosco, ya kuwa kumbukumbu hai na shukrani kwa Mama Bikira Maria kwa maongozi yake katika maisha ya Don Bosco ndiyo maana tunaitwa Mabinti wa Bikira Maria Msaada wa Wakristo. “Kwa kipawa cha Roho Mtakatifu na maongozi ya moja kwa moja ya Bikira Maria, Mtakatifu Yohane Bosco alianzisha shirika letu kama jibu la wokovu na matumaini makubwa kwa watoto na wasichana. Alilijalia urithi wa kiroho uliochochewa na upendo wa Kristo, Mchungaji Mwema, na kulipa hadhi ya umisionari.” (Const. FMA 1). Tumewekwa wakfu kwa Mungu ili kumtumikia Yesu Kristo katika jumuiya, tunajitolea maisha yetu kwa ubinadamu na kutoa elimu ya kisalesian kwa vijana. Don Bosco alituchagulia Bikira Maria, msaada wa Wakristo, ambaye walijua jinsi ya kupata mwili na kuishi mafundisho ya ‘kutunza’, ambayo yanahitimisha shauku yetu ya elimu kwa vijana na kutufanya sisi wanawake ambao huzalisha maisha katika moyo wa taamuli. Roho ya Kisalesian umejikita katika Ekaristi Takatifu, Ibada kwa Bikira Maria na uaminifu kwa Mamlaka fundishi ya Kanisa yaani “Magisterium.”

Historia: Ukomavu wa nia ya Don Bosco katika  kuanzisha shirika la watawa wa kike  kwa ajili ya elimu ya wasichana wadogo ulitokana na  kuzingatia mazingira ya wakati ule hali ya umaskini ambayo wasichana wengi walijikuta; katika kuwasiliana na mashirika  mbalimbali ya watawa wa kike; uthibitisho wa Papa Pius IX aliyemtia moyo katika uchaguzi huu; kupitia ‘ndoto’ za kujirudia-rudia na matukio mengi ambayo yeye mwenyewe alisimulia; na kutokana na kina cha ibada yake kwa Bikira Maria: "Watunze, ni mabinti zangu” (Istitute of FMA, Cronistoria, vol 1 p.25). Wakati Don Bosco akikomaa katika mradi huu, huko Mornese, Alessandria, kulikuwa na binti mmoja akiitwa Mari Domenica Mazzarello, mshiriki wa Chama cha Mabinti wa Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili alikuwa akihuisha kikundi cha wasichana waliojitolea kwa wasichana wa mji huo kwa lengo la kuwafundisha ushonaji, na zaidi ya yote, kuwaongoza wawe Wakristo wema na raia waaminifu. Ndoto hizi mbili zilikuwa zikikutana kwenye hali inayofanana: kuanzishwa shirika la watawa wa kike kwa ajili ya malezi ya wasichana na vijana ndani ya familia ya Wasalesiani kama walivyokuwa wakifanya mapadre wasalesiani kwa vijana wa kiume: karama mpya ya elimu katika Kanisa. Kwa msingi huu, Don Bosco alichagua kikundi cha mabinti wa Maria Imakulata. Ambapo Maria Domenica Mazzarello alikuwa Mwanzilishi Mwenza katika kutoa sura na maendeleo kwa shirika hili jipya. Tarehe 5 Agosti 1872 huko Mornese kundi la kwanza la wasichana kumi na mmoja liliweka nadhiri zake za kwanza kuwa ndani ya Kanisa na katika jamii, waelimishaji wa wasichana wadogo, hasa wale wenye uhitaji zaidi. Walibaki katika Nyumba mama kutoka mwaka 1872 hadi 1879.

Mtakatifu Yohane Bosco alijisadaka kwa ajili ya malezi na makuzi ya vijana
Mtakatifu Yohane Bosco alijisadaka kwa ajili ya malezi na makuzi ya vijana

Katika kipindi hicho kifupi walitoa utambulisho ulioakisi jina lake kwa usahihi kama asili ya mji huo mdogo, roho ya Mornese. Wakiongozwa na malezi bora na busara ya Mama Mazzarello, FMA kwa ubunifu iliochanganywa na “Mfumo Kinga wa Don Bosco” katika mahitaji ya elimu kwa wanawake na watoto, pamoja na uwepo hai shuleni na katekesi makini. Walipata kibali na katiba ya Jimbo kutoka kwa Askofu wa Acqui, mnamo Januari 23, 1876, FMA wakihimizwa na bidii ya kimisionari walianza kuondoka kutoka Mornese hadi Uruguay mnamo 1877 na kisha Argentina. Tangu wakati huo shirika lilienea zaidi na zaidi nchini Italia, na nchi nyingine za Bara la Ulaya, na Amerika. Tangu 1891 FMA walienda Asia,1893 walifika Barani Afrika na 1954 huko Australia. Utume wa FMA unafanywa kwa sehemu kuu katika sekta ya elimu ili kukuza na kudumisha majadiliano ya kidini na kitamaduni; ustawi wa jamii na maendeleo ya wanawake na wasichana. Mnamo 1911, baada ya miaka 39 ya kuanzishwa kwake, Papa Pius X alitoa idhini kwamba, Shirika hili liwe na hadhi ya Shirika la Kipapa.

Lengo la Shirika ni kutoa elimu kwa wasichana.
Lengo la Shirika ni kutoa elimu kwa wasichana.

Karama na Utume: Sisi Mabinti wa Maria Msaada wa Wakristo, tunafanya kazi kwa nia na moyo mmoja kwa ajili ya Wokovu wa vijana, tukikabiliana kwa ujasiri na changamoto za ulimwengu. Katika nyayo za Don Bosco na Maria Domenica Mazzarello tunajitolea kwa vijana ambao ni wahitaji zaidi, yaani, wale ambao kwa sababu mbalimbali wana uwezo mdogo wa mafanikio na kwa hiyo wanakabiliwa na hatari na changamoto pevu katika malezi na makuzi yao. Don Bosco, alikuwa na maono ya mbeleni katika kuzuia, yaliyokusudiwa kuelimisha, kukuza uwezo wa mtu wa kutoa maana ya maisha kupitia uzoefu mzuri na kutenda kwa uaminifu maamuzi anayoyachukua. Uinjilishaji miongoni mwa vijana ndio dhamira yetu ya msingi na tunaitekeleza kwa njia mbalimbali, lengo zaidi likiwa ni Elimu. Tunaelimisha vijana kwa kutumia “Mfumo wa Kinga”, kiini cha urithi wa Don Bosco kwa familia yote ya Wasalesiani. Mfumo wa Kinga kama hali ya kiroho umekita mizizi yake ndani ya Moyo Mtakatifu wa Yesu, Mchungaji Mwema na kama mbinu una vipengele vikuu vitatu vya msingi: sababu, dini, na fadhili zenye upendo. Kwa sababu, vijana husaidiwa kusitawisha fikra zao na kuwa na mtazamo wa utambuzi ambao utawawezesha kufanya maamuzi ya akili, na maamuzi ya kimaadili. Kwa njia ya dini vijana huambatana na kuwa na uhusiano wa kina na wa kudumu na Kristo Yesu kwa njia ya: Sala, maisha ya Sakramenti na kwa malezi ya dhamiri nyofu. Don Bosco alisisitiza “Elimu ni jambo la moyo, ambalo Mungu ndiye Mwalimu mkuu”, kwa hiyo Mfumo wa Kinga umejengwa juu ya fadhila ya Injili ya wema wenye upendo. Hizi ndizo nguzo tatu za ulimwengu tunazojenga kwa vijana. Kauli mbiu ya Don Bosco, “da mihi animas cetera tolle” (Nipe roho na mengineyo chukua), ndiyo iliyomtia motisha Mama Mazzarello, na pia ndiyo msukumo kwa kila mtawa Msalesian leo kujitolea kikamilifu kwa vijana, hasa wenye uhitaji katika jamii. Kama mabinti wa Maria tunajiweka katika ibada kamili ya kimwana chini ya mwongozo na ulinzi wa Mama yetu Mtakatifu, Bikira Maria Msaada wa Wakristo.

Malezi na Majiundo makini kwa wasichana ni muhimu
Malezi na Majiundo makini kwa wasichana ni muhimu

Tukihuishwa na karama ya Wasalesian yenye sifa maalum ya 'Roho ya Mornese', FMA lengo la kazi yetu ni ukuaji kamili wa watu, kuambatana na vijana katika safari yao ya ukomavu katika mradi wao wa maisha, malezi katika imani, na elimu kwa uraia hai Elimu ya msichana ni kipaumbele cha FMA ambacho kinafanywa katika Nchi mbalimbali: malezi ya kitamaduni na uinjilishaji, kuingizwa katika ulimwengu wa ajira, kukuza vyama vya ushirika vya wanawake katika utume ili kuwasaidia wasichana ambao ni waathirika wakuu wa mifumo ya utumwa mamboleo kama vile: Ukahaba, biashara haramu ya binadamu na viungo vyake; kwa kuwaongoza kusimama kidete kupigania utu, heshima na haki zao msingi. Miongoni mwa kazi na utume unaotekelezwa na FMA: Ni kuendesha vituo vya malezi na elimu kwa vijana; shule na vituo vya ufundi; Vyuo vikuu na Taasisi za elimu ya juu; Vituo vya mafunzo ya Kazi kwa wasiojiweza na maskini. Masista pia wanaendesha vituo vya malezi na maisha ya kiroho; Vituo vya maendeleo ya wanawake; Chama cha Maendeleo ya Elimu ya Wanawake wa Kujitolea Kimataifa. (VIDES), Ofisi ya Haki za Binadamu, Hosteli za Vyuo vikuu na Taasisi za elimu ya juu pamoja na huduma kwa wakimbizi. Kazi hizi huzihusisha Jumuia za Kuelimisha za FMA zinazochochewa na kauli mbiu “Da mihi animas cetera tolle” yenye usikivu wa kike, ikichochewa na haiba ya Shirika, iliyo wazi kwa ushirikiano na familia, Taasisi, watu wote wenye mapenzi mema wanaoshiriki katika utume wetu. Kwa kushirikiana na moyo wa vijana, tunasikiliza ili kupambanua ‘mahali pengine’ ambapo tunaweza kuishi mantiki ya Injili ya karama na udugu. Tunajiruhusu kupata changamoto zote za kibinadamu, kwa kuzingatia hasa hali ya wasichana, wakimbizi na wahamiaji, utunzaji bora wa mazingira, nyumba ya wote, mazingira ya kidigitali, utafutaji na ukuzaji wa: amani, haki, upatanisho, ustawi na maendeleo ya wengi.

Papa Francisko alipotembelea Wasalesiani, Torino
Papa Francisko alipotembelea Wasalesiani, Torino

UWEPO NA UTUME WETU SEHEMU MBALIMBALI ZA DUNIA.

Mwaka 2022 tumeadhimisha miaka 150 tangu kuanzishwa kwa Shirika letu ambapo idadi ya watawa ni 10,741kadiri ya takwimu za Mwezi Desemba 2022.  Masista wa Salesian ni mojawapo kati ya Mashirika makubwa ya watawa wa kike katika Kanisa Katoliki, tunafanya utume katika nchi 97 ndani ya Mabara 5. Bara la Amerika: Tupo watawa 3110, katika nchi 23. Bara la Ulaya: Tupo watawa 4202, katika nchi 22. Bara la Asia: Tupo watawa 2777, katika nchi 22. Bara la Oceania: Tupo watawa 55, katika nchi 4. Barani Afrika: Tupo watawa 597, katika nchi 26 nazo ni: Angola, Benin, Burkina Faso, Cameroon, Congo Brazzaville, Congo DRC, Pwani ya Pembe, Misri, Ethiopia, Gabon, Ghana, Guinea Equatorio, Kenya, Lesotho, Madagasca, Mali, Msumbiji, Nigeria, Rwanda, Afrika ya Kusini; Sudan ya Kusini, Sudan Kongwe, Tanzania, Togo, Tunisia na Zambia. Katika Kanda ya Afrika Mashariki tupo nchini: Kenya, Rwanda na Tanzania. Tunafundisha katekesi maparokiani na somo la dini shuleni, Tunafundisha katika shule za awali hadi sekondari na katika Chuo cha Tangaza, kilichoko Jijini Nairobi, Tuna vituo vya malezi kwa watoto na vijana; shule za ufundi, vikundi vya maendeleo, ustawi wa jamii kwa akina mama, nyumba za malezi kwa watoto yatima. Nchini Tanzania: Tunafanya utume wetu katika Jimbo kuu la Dar es Salaam na Jimbo Katoliki la Morogoro. Tunafundisha katekesi maparokiani, shule ya awali na msingi ya “Mary Our Help”, Chuo cha Ufundi Cha Matumaini. Tunafundisha dini katika shule za msingi na sekondari zinazoongozwa na kumilikiwa na Serikali zilizoko jirani na jumuiya zetu, malezi kwa Chama Cha Utoto Mtakatifu na Kituo cha Vijana cha Don Bosco Temeke Mikoroshoni.

Bikira Maria Msaada wa Wakristo ni Msimamizi na Mwiombezi wetu
Bikira Maria Msaada wa Wakristo ni Msimamizi na Mwiombezi wetu

Mpango Mkakati wa Malezi

•        Ukandidati

•        Uaspiranti

•        Upostulanti

•        Unovisi

•        Nadhiri za muda ambazo zinafuatiwa na nadhiri za daima.

Je, ungenda kuwa mmoja wetu? Unahitaji msukumo wa ndani wa kumtumikia Mwenyezi Mungu, vijana na watoto. Uwe ni mtu mwenye furaha na upendo kwa vijana na watoto, mambo yanayohitaji tabia na afya njema: kiroho na kimwili. Jitahidi uwe na elimu ya sekondari na ufaulu mzuri ili kuweza kukabiliana na changamoto mamboleo katika maisha ya kitawa katika ulimwengu wa utandawazi na maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia. Jitahidi uwe na umri kati ya miaka 18 hadi 25, hapo utaweza kufurahia hatua mbalimbali za malezi na makuzi ya kitawa. Ukipenda unaweza kuwasiliana nasi kwa namba zifuatazo:

KENYA : +254 799 258 092.

TANZANIA:+255 757 330 089.

RWANDA :+250 791206 990.

Miito Duniani
26 April 2023, 14:05