Tafuta

Baraza la Kipapa la Majadiliano ya Kidini limetoa ujumbe kwa waamini wa dini ya Kiislam unaonogeshwa na kauli mbiu “Wakristo na Waislam Wahamasishaji wa Upendo na Urafiki:” Baraza la Kipapa la Majadiliano ya Kidini limetoa ujumbe kwa waamini wa dini ya Kiislam unaonogeshwa na kauli mbiu “Wakristo na Waislam Wahamasishaji wa Upendo na Urafiki:”  

Ujumbe wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani na Sherehe ya Id Al Fitri kwa Mwaka 2023

Mfungo wa mwezi Mtukufu wa Ramadhan na hatimaye maadhimisho ya Sikukuu ya ‘Id al-Fitr 1444 H. / 2023 A.D., yalianza tarehe 23 Machi 2023. Baraza la Kipapa la Majadiliano ya Kidini limetoa ujumbe kwa waamini wa dini ya Kiislam unaonogeshwa na kauli mbiu “Wakristo na Waislam Wahamasishaji wa Upendo na Urafiki.” Lengo ni kujizatiti katika ujenzi wa jamii inayosimikwa katika msingi wa amani, maridhiano na furaha kama sehemu ya ujenzi wa familia kubwa zaidi.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Katika dini ya Kiislamu, kuna nguzo kuu tano ambazo ni muhimu katika imani yao, nazo ni: Shahada (kukiri Imani), Sala, Zakat, Sawm, na Hija. Kalenda ya dini ya Kiislamu inaanza baaada ya Hija ya Mtume Muhammad (Salah Allah alaghi wa salaam – amani iwe kwake) kutoka Mecca kwenda Medina mwaka 622 AD na kuanzisha jumuiya ya kwanza ya Kiislamu (Ummah). Huo ndio mwaka mpya wa Kiislamu 622 (Anno Hegirae AH). Kwa hiyo kalenda ya dini ya Kiislamu inajulikana kama Hijri au Lunar kwa vile inafuata mwandamo wa Mwezi. Hii ndiyo inayotumika katika matukio ya imani na tamaduni zao, kama sikukuu na mfungo. Ramadhani inatokana na neno la Kiarabu “ان‎, Ramida au ar-ramad” likimaanisha, ukavu. Ramadhani ni kati ya miezi muhimu sana katika dini ya Kiislamu. Ramadhani ni mwezi mtukufu kwa waamini wa dini ya Kiislam kwa sababu ni katika mwezi huu Mungu (Allah) alimpa Mtume Muhammad (Salah Allah alaghi wa salaam) sura ya kwanza ya Kuruani Tukufu mwaka 610. Sura hiyo al fatihah yaani ufunguzi, inasomwa yote katika kila sala kwa mwamini wa dini ya Kiislam. Hivyo ni maarufu kama Mama wa Kitabu au Mama wa Kuruani (Umm al Kitabu au umm al kuruani). Hii ni Sura inayomwalika mwamini wa dini ya Kiislam kutambua Ukuu wa Mungu muweza wa yote, kuomba ulinzi na huruma yake na kuendelea kumsifu. Ramadhani ni mwezi wa tisa katika Kalenda ya dini ya Kiislamu, ambapo Waislamu wanaalikwa kufunga, kuacha anasa na kusali zaidi ili kuwa karibu na Mwenyezi Mungu (Allah). Japo Waislamu wanasali kila siku tena mara tano inaaminika sala katika kipindi cha Mwezi Mtukufu wa Ramadhani inabeba uzito zaidi, kwa kuwa ni katika mwezi huu Mtume alikutana na Allah.

Kufunga ni nguzo ya nne ya dini ya Kiislam
Kufunga ni nguzo ya nne ya dini ya Kiislam

Ramadhani inaanza rasmi baada ya kiongozi wa dini kutangaza kuona mwezi mpya. Hiki ni kipindi kwa Waislamu cha kusoma Kuruani, kutafakari na kukua kiroho yaani kupata thawabu. Sala ya usiku katika kipindi hiki kadiri ya ahadi ya Mwenyezi Mungu anayeisali kwa imani na kuomba rehema, dhambi zake za nyuma zote zitafutwa. Ramadhani ni kipindi cha kujenga umoja kwa kuonesha mshikamano kwa Waislamu wote duniani kwa njia ya mfungo na sala. Kufunga ni nguzo ya nne ya imani ya dini ya Kiislamu. Katika Mwezi Mtukufu wa Ramadhani, mwamini wa dini ya Kiislam anapaswa kufunga, kuacha chakula na maji kuanzia jua linapochomoka mpaka linapozama. Kwa tamaduni mfungo huvunjwa kwa maji na tende jua linapozama, mlo wa kuvunja mfungo unaitwa iftar (futari). Mfungo unawakumbusha Waislamu kwamba, mtu siyo mwili tu bali roho pia. Ramadhani ni kipindi cha Waislamu kutoa huduma kwa jamii mfano kusaidia maskini na kushirikishana kile walichojaliwa na wahitaji. Wanaalikwa kuadhimisha kila Ramadhani kwa uadilifu kama ndio ya mwisho kwa kila mwamini, ili Mwenyezi Mungu aweze kuwasamehe maovu waliyotenda. Ili mfungo ufanikiwe ni lazima kuweka niyyah na kufuata sheria za mfungo (Surat Al-Baqarah, aya 183). Kama mwamini ambaye amevunja mfungo mfano wanawake kwenye siku zao basi inabidi kulipizia baada ya kumaliza mfungo.

Mwezi Mtukufu wa Ramadhani ni wakati wa kusali na kufunga
Mwezi Mtukufu wa Ramadhani ni wakati wa kusali na kufunga

Mwezi wa tisa katika Kalenda ya dini ya Kiislamu unajulikana kama mwezi wa Ramadhani au Ramazan. Mwezi huu mtukufu unaadhimishwa kama mwezi wa mfungo wa waamini wa dini ya Kiislam. Kushika saumu katika mwezi huu kunachukuliwa kuwa moja ya nguzo tano za dini ya Kiislam. Kuanzia mwezi mpevu unapoonekana kwa mara ya kwanza hadi siku inayofuata, sherehe za Ramadhani Kareem hudumu kwa takriban siku 29 au 30. Mwezi huu mtukufu kimsingi ni mfano wa nidhamu ya kibinafsi ambapo watu sio tu kwamba wanakata tamaa ya maji na chakula lakini pia hutumia wakati huu kuzama zaidi katika sala, matendo mema, hisani na huduma za jamii ambazo kimsingi huwasogeza waamini karibu zaidi na Mwenyezi Mungu. Mwezi mtukufu wa Ramadhan ukizingatiwa kuwa nguzo ya nne ya dini ya Kiislam umejengwa juu ya kanuni kama vile kujirekebisha, utakaso wa mawazo, kuwasaidia wenye shida na kupyaisha imani. Kwa mujibu wa Quran tukufu, huu ni mwezi wa maana sana kwani Mtume Mohammad alipokea aya za kwanza za Maandiko matakatifu. Kwa hiyo, mwezi huu unatajwa kuwa wakati muafaka wa kufunga na kusali kwa bidii na shauku kubwa. Kwa mujibu wa dini ya Kiislam, matendo mema yanayotekelezwa katika mwezi Mtukufu wa Ramadhani huleta ustawi na mafanikio. Pia, inaaminika kuwa katika mwezi Mtukufu wa Ramadhani, milango ya mbinguni hufunguliwa na mashetani hufungwa minyororo.

Ujumbe: Upendo na Urafiki
Ujumbe: Upendo na Urafiki

Mfungo wa mwezi Mtukufu wa Ramadhan na hatimaye maadhimisho ya Sikukuu ya ‘Id al-Fitr 1444 H. / 2023 A.D., yalianza tarehe 23 Machi 2023. Ni katika muktadha huu, Baraza la Kipapa la Majadiliano ya Kidini limetoa ujumbe kwa waamini wa dini ya Kiislam unaonogeshwa na kauli mbiu “Wakristo na Waislam Wahamasishaji wa Upendo na Urafiki.” Lengo ni kujizatiti katika ujenzi wa jamii inayosimikwa katika msingi wa amani, maridhiano na furaha kama sehemu ya ujenzi wa familia kubwa ya binadamu. Ujenzi wa jamii inayosimikwa katika upendo na urafiki ni mchakato unaokabiliwa na changamoto kubwa hasa kutokana na baadhi ya watu kutaka kupanda “ndago” za chuki na uhasama kati ya Wakristo na Waislam kwa mafao yao binafasi. Lakini Wakristo na Waislam wanapaswa kuimarisha upendo na urafiki kati yao na kamwe wasiruhusu tofauti zao msingi kutokana na dini, kabila, tamaduni, lugha au misimamo yao ya kisiasa kuwa ni chanzo cha kinzani na mipasuko ya kijamii. Tofauti zao ni mambo msingi, lakini kuna makubwa zaidi yanayowaunganisha. Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican wanasema, “Maana, watu wote ni jumuiya moja tu. Wenyewe, asili yao ni moja, kwa sababu Mungu aliwaweka wote wakae juu ya uso wa nchi yote; tena wao wanacho kikomo kimoja tu, yaani Mungu, ambaye maongozi yake, ushuhuda wa wema wake, na azimio lake la wokovu yawaelekea watu wote, hadi wateule wapate kukusanyika katika Mji Mtakatifu, ambao utukufu wa Mungu utautia nuru, na ambapo Mataifa watatembea katika nuru yake.” Nostra aetate. N.1.

Ujumbe na matashi mema kutoka kwa Baraza la kipapa
Ujumbe na matashi mema kutoka kwa Baraza la kipapa

Huu ni mwaliko wa kuondokana na tabia ya kutiliana shaka, kinzani, woga na wasiwasi, ubaguzi, tabia ya kuwatenga na kuwanyanyasa wengine; dhuluma, matusi na kejeli, kinyongo na kutetana. Haya ni mambo ambayo kwa kiasi kikubwa yanachochewa na vyombo vya mawasiliano ya jamii, kiasi cha kujenga chuki na uhasama; tabia ya kuchafuana na kutaka kulipiza kisasi. Kumbe, Wakristo na Waislam wanapaswa kujikita katika tabia ya kuheshimiana, utu wema, upendo na urafiki; kwa kusaidiana kidugu; kusameheana, kushirikiana kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Ni wajibu wa waamini wa dini hizi mbili kuwasaidia maskini na wahitaji zaidi: kiroho na kimwili; kwa pamoja wajizatiti kulinda, kutunza na kuendeleza mazingira bora nyumba ya wote, ili dunia iweze kuwa ni mahali bora zaidi pa kuishi mintarafu misingi ya haki, amani na furaha. Tabia ya watu kuchukiana na kujengeana uhasama, iwekwe kando na badala yake, waamini wa dini hizi mbili wajenge utamaduni wa upendo, urafiki na elimu makini kwa vijana wa kizazi kipya. Ikumbukwe kwamba, vijana wengi wanafundwa zaidi na mitandao ya kijamii pamoja na vyombo vya mawasiliano ya kijamii. Lakini waamini wa dini hizi wajielekeze zaidi katika malezi na makuzi yanayoanzia kwenye familia, shuleni, nyumba za ibada na baadaye kwenye mitandao ya kijamii. Mahali ambapo kuna haki na amani; udugu wa kibinadamu, ustawi na maendeleo ya wengi, hapo Mwenyezi Mungu yupo na hivyo kuwa ni chemchemi ya furaha na mwaliko kwa waamini wote kushiriki kikamilifu. Baraza la Kipapa la Majadiliano ya Kidini linawatakia waamini wa dini ya Kiislam Mfungo mwema wa mwezi Mtukufu wa Ramadhan na hatimaye, maadhimisho ya Sikukuu ya ‘Id al-Fitr 1444 H. / 2023 A.D., ili Mwenyezi Mungu awakirimie furaha inayopata chimbuko lake kutokana na uaminifu kwa Mungu na upendo wake wa daima.

Mwezi wa Ramadhani

 

21 April 2023, 15:36