Askofu Msaidizi Yohane Suzgo Nyirenda wa Jimbo Katoliki Mzuzu
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Baba Mtakatifu Francisko amemteuwa Mheshimiwa sana Padre Yohane Suzgo Nyirenda kutoka Jimbo Katoliki la Mzuzu kuwa Askofu msaidizi wa Jimbo Katoliki Mzuzu, nchini Malawi. Hadi kuteuliwa kwake tarehe 5 Mei 2023 Askofu mteule Yohane Suzgo Nyirenda alikuwa ni Gambera wa Nyumba ya Malezi ya Kasina. Itakumbukwa kwamba, Askofu mteule Yohane Suzgo Nyirenda alizaliwa tarehe 20 Juni 1970, huko Wozi, Wilaya ya Mzimba, Jimbo Katoliki la Mzuzu. Baada ya masomo na majiundo yake ya Kikasisi, tarehe 19 Julai 2008, akapewa Daraja Takatifu ya Upadre kwa ajili ya Jimbo Katoliki la Mzuzu. Tangu wakati huo kama Padre amefanya utume ufuatao: Paroko-usu wa Parokia ya Katete kuanzia mwaka 2008 hadi mwaka 2010, Paroko-usu wa Parokia ya Mzambazi, kati ya mwaka 2010 hadi mwaka 2014., Paroko wa Parokia ya Mtakatifu Augustine kati ya mwaka 2014-2017 na hatimaye Mkurugenzi wa miito kati ya mwaka 2012-2017.
Baadaye alitumwa kwenda kujiendeleza zaidi kwenye masuala ya Sheria za Kanisa kwenye Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha Afrika Mashariki na Kati, CUEA kati ya mwaka 2016 hadi mwaka 2018. Aliporejea Jimboni mwake akateuliwa kuwa ni Gambera wa Kituo cha Maisha ya kiroho cha “Christ the King Formation Centre” kati yam waka 2017-2018. Baadaye alitumwa Jimbo kuu la Arusha kwa ajili ya kuweza kujipatia Diploma kutoka katika Chuo cha Lumen Christi Institute kati ya mwaka 2018-2019. Tangu mwaka 2019 hadi kuteulia kwake na Baba Mtakatifu Francisko tarehe 5 Mei 2023 alikuwa ni Gambera wa Nyumba ya Malezi ya Kasina.