Baraza la Kiswahili la Taifa, BAKITA Kushirikiana na Radio Vatican Kukuza Lugha ya Kiswahili
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa, UNESCO katika mkutano wake wa 41 uliofanyika mjini Paris, Ufaransa, tarehe 23 Novemba 2021 uliamua kwamba, tarehe 7 Julai ya kila mwaka itakuwa ni Siku ya Kiswahili Duniani. Azimio hili lilipitishwa na wanachama wote wa UNESCO bila kupingwa. Waswahili kutoka sehemu mbalimbali za dunia, wakafurahia sana tamko hili, kwa Umoja wa Mataifa kuamua kutoa kipaumbele cha pekee kwa Lugha ya Kiswahili. Hii ni lugha ya kwanza ya mawasiliano kutoka Barani Afrika kutambuliwa rasmi na Umoja wa Mataifa na kutengewa siku maalum ya kuadhimishwa Kimataifa. Kiswahili kinatambulikana kuwa ni lugha rasmi kwenye Umoja wa Afrika, Jumuiya ya Afrika Mashariki pamoja na Bunge la Afrika. Lakini, ikumbukwe kwamba, Kiswahili ni lugha iliyopitishwa kutumiwa na Umoja wa Jumuiya ya Maenedeleo Kusini mwa Afrika (SADC). UNESCO inakaza kusema, Kiswahili ni lugha inayotumika kuibua fursa mbadala inayolenga kukidhi mtazamo wa dunia kwa ujumla. Kukua kwa Kiswahili kunatoa historia ya karne ya mabadiliko duniani. Kiswahili ni miongoni mwa lugha kumi zinazozungumzwa zaidi duniani na hivyo kujenga utengamano miongoni wa jamii na Mataifa mbalimbali, lugha ya kurushia habari na lugha ya elimu. Kiswahili ni lugha ya kidiplomasia na kama lugha rasmi ya Umoja wa Afrika. Kiswahili kinachangia kusukuma ajenda ya Afrika ya mwaka 2063 ambayo pia ni kipaumbele cha UNESCO. Lugha ya Kiswahili huchangia kuleta utengamano na amani na UNESCO ina jukumu la kuimarisha na kuleta amani duniani.
Kiswahili ni lugha rasmi ya Taifa katika nchi za Tanzania, Uganda na Kenya. Kiswahili kinatumiwa na Idhaa za redio na runinga zaidi ya 300. Kiswahili kinafundishwa katika vyuo zaidi ya 150 duniani kote. Lugha hii kwa sasa inakadiriwa kuwa na wazungumzaji zaidi ya milioni 200. Itakumbukwa kwamba Kiswahili ni lugha ya nane duniani na lugha ya kwanza Afrika kupewa siku maalumu ya kuadhimishwa duniani na UNESCO. Kwa upande wake, Rais Samia Suluhu Hassan wa Tanzania aliupongeza Ubalozi wa kudumu wa Tanzania nchini Marekani na Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni UNESCO kwa kuandaa maadhimisho makubwa ya kwanza ya Siku ya Kimataifa ya Kiswahili Duniani na kusema kuwa wameitendea haki lugha ya Kiswahili ambayo ni alama ya: Uhuru, Amani na Umoja. Kiswahili ni Lugha ya Uhuru, Rais Samia amesema kwamba, Kiswahili kilitumika kama lugha ya ukombozi hasa Kusini mwa Afrika na hivyo ilichangia sana kuleta uhuru na umoja.” Pia ameeleza namna lugha hiyo ilivyotumika kujenga umoja wa kitaifa na mshikamano na kutatua migogoro katika Ukanda wa Afrika Mashariki, Kati na Kusini. Akizungumzia Kiswahili na Malengo ya Maendeleo Endelevu ya Umoja wa Mataifa SDGs amesema Kiswahili ni nyenzo muhimu kwenye utekelezaji wa malengo hayo ya SDGs ifikapo mwaka 2030 na ajenda ya Umoja wa Afrika ya mwaka 2063.
Ni katika muktadha huu, DR. Fatma Abdalah Mlaki, Mchunguzi Lugha kutoka Baraza la Kiswahili la Taifa, Tanzania katika mahojiano maalum la Radio Vatican anafafanua kwa kina na mapana mpango mkakati wa kukuza lugha ya Kiswahili 2022-2032, Kongamano la Maadhimisho ya Siku ya Kiswahili Duniani, na litafanyika 7 Julai 2023 Zanzibar. BAKITA inaratibu na kuendesha Makongamano ambayo yana mchango mkubwa katika kuendeleza na kukuza lugha ya Kiswahili. Kongamano la Idhaa zote duniani zinazorusha matangazo yake kwa Lugha ya Kiswahili, ambalo hufanyika mwezi Machi ya kila mwaka, mwaka 2022 lilifanyika Jijini Arusha na Mwaka 2023 limeadhimishwa Zanzibar. DR. Fatma Abdalah Mlaki, anakaza kusema, Kiswahili kimekuwa na kina wingi wa watumiaji, inafahamika na ni lugha ambayo imesambaa na kupokeleka na swengi na kwamba, ni lugha pekee inayofundishwa kwa wingi katika vyuo vikuu vya Kimarekani na Ulaya na kwamba, Kiswahili ni lugha inayosomwa na wengi. Hii ni changamoto kwa wadau mbalimbali kuhakikisha kwamba, wanatumia fursa kuwekeza katika lugha ya Kiswahili kama mbinu mkakati wa kuendeleza lugha sanjari na kujipatia kipato. Ikumbukwe kwamba, Kiswahili ni ajira, bidhaa na ni chanzo cha kipato. BAKITA inaomba ushirikiano na Radio Vatican ili kukuza na kuendeleza lugha ya Kiswahili.
DR. Fatma Abdalah Mlaki amesema, hivi karibuni alikuwa nchini Italia kutoa mafunzo ili kuimarisha stadi za kufundishia lugha ya Kiswahili kwa wageni, watu wa diaspora wanaoishi nchini Italia. Kozi hii imehudhuriwa na washiriki kutoka Chuo Kikuu cha Torino na Chuo kikuu cah Napoli pamoja na kuwashirikisha wafanyakazi wa Ubalozi wa Tanzania nchini Italia. Washiriki wameonesha ari na mwamko mkubwa wa kuendeleza lugha ya Kiswahili kwa wageni. Itakumbukwa kwamba, Ubalozi wa Tanzania nchini Italia, tangu mwaka 2019 umekuwa ukifundisha Lugha ya Kiitalia. Ni matarajio yake kwamba, baada ya kozi hii, itasaidia kuleta mabaresho kwa kuongeza kasi, ari na mwamko pamoja na weledi. Kwa hakika Kiswahili kimetandawaa, kimeenea na kinafahamika. Kiswahili ni lugha yenye fursa nyingi kwani hii ni lugha ya kazi: Umoja wa Afrika; Umoja wa Jumuiya ya Maenedeleo Kusini mwa Afrika (SADC) pamoja na Bunge la Afrika Mashariki. Kiswahili pia ni lugha rasmi nchini Kenya, Tanzania. Kumbe, kuna fursa ya kufanya tafsiri, ukalimani, kufundisha na kuandaa machapisho mbalimbali. Kumbe, Lugha ya Kiswahili ni fursa kwa wachapishaji, waandishi na wasambazaji.