Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania: Taarifa ya Kurugenzi ya Mawasiliano ya Jamii
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, TEC., kuanzia Dominika 14 Mei hadi tarehe 21 Mei 2023 linafanya Hija ya Kitume “Ad Limina Apostolorum Visitatio,” kwa kifupi, “Ad Limina” inayofanyika kila baada ya miaka mitano. Lengo kuu ni: Kukutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko pamoja na kutoa taarifa ya Maandishi kwa Baraza la Kipapa la Maaskofu kuhusu mwenendo mzima wa maisha na utume wa Kanisa katika Jimbo husika. Ni fursa pia ya kujadiliana na wakuu wa Mabaraza ya Kipapa kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya Kanisa la Kristo Yesu kama sehemu ya ujenzi wa Kanisa la Kisinodi. Ni wakati wa sala na tafakari ya kina kuhusu maisha na utume wa Kanisa la Tanzania katika ujumla wake. Maaskofu Katoliki Tanzania wamekwisha kutembelea Mabaraza ya Kipapa na kupata nafasi ya kuzungumza na wakuu wa Mabaraza haya. Jumanne, tarehe 16 Mei 2023, Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania limetembelea Baraza la Kipapa la Mawasiliano na kuzungumza na wakuu wake chini ya uongozi wa Dr. Paolo Ruffini, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Mawasiliano. Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican wanasema, Mama Kanisa anajua kwamba vyombo vya mawasiliano ya jamii vikitumiwa vizuri vyaweza kuleta faida kubwa kwa binadamu. Vinatoa mchango mkubwa katika ukuzaji na ustawishaji wa nafsi za watu na pia katika uenezaji na uimarishaji wa Ufalme wa Mungu. Lakini pia vyombo hivi vikitumiwa kinyume cha lengo la Mungu Muumbaji vinaweza kudhuru. Kanisa husikitishwa kwa huzuni ya kimama na uharibifu huo, ambao matumizi maovu ya vyombo hivyo uharibu jumuiya ya watu. Kanisa mwaka 2023 linaadhimisha kumbukizi la Miaka 60 tangu Mababa wa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican walipochapisha Waraka wa Inter Mirifica yaani “Kati ya Mambo ya Ajabu” Tamko kuhusu Vyombo vya Upashanaji Habari. Vyombo vya mawasiliano na mitandao ya kijamii ni nyenzo muhimu sana katika mchakato wa uinjilishaji. Rej. IM, 2.
Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania limeendelea kusoma alama za nyakati kwa kutumia kikamilifu vyombo vya mawasiliano na mitandao ya kijamii kama vile: Radio za Majimbo, Tumaini TV, na Gazeti la Kiongozi katika ngazi ya Kitaifa. Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania limekuwa na ushirikiano mzuri na vyombo vya mawasiliano ya jamii vinavyomilikiwa na kuendeshwa na Vatican kama sehemu ya uinjilishaji. Limekuwa likipokea ruzuku ya vyombo vya mawasiliano ya jamii kutoka SIGNIS na kwamba, kuna ushirikiano mkubwa kati ya Radio Vatican na vyombo vya mawasiliano ya jamii vinavyoendeshwa na Maaskofu Katoliki Tanzania. Kuna vituo 14 vya Radio za Kanisa na hivi karibuni kumeanzishwa Radio Hekima inayoendeshwa na kumilikiwa na Jimbo Katoliki Mbinga na Radio Taa Bora ya Jimbo kuu la Tabora. Kumbe, Kanisa Katoliki lililoanzishwa na Kristo Yesu kwa madhumuni ya kuleta wokovu kwa watu wote, linasukumwa na wajibu wa kuihubiri na kuishuhudia Habari Njema ya Wokovu kwa kutumia pia vyombo vya mawasiliano na pia kuwafundisha watu wa Mungu kuvitumia vyombo hivi kwa namna inayofaa, kwa ajili ya wokovu wa wao wenyewe na wa familia nzima ya mwanadamu. Rej. IM. 3. Vyombo vya mawasiliano ya jamii vinavyomilikiwa na kuendeshwa na Kanisa Katoliki vimekuwa ni msaada mkubwa katika mchakato wa Uinjilishaji.
Askofu Eusebius Alfred Nzigilwa wa Jimbo Katoliki la Mpanda ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kurugenzi ya Mawasiliano Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, amesema kwamba, Maaskofu wako mbioni kuboresha matangazo yanayorushwa na Tumaini TV pamoja na Radio za Majimbo sanjari na kuanzisha Kituo cha Uchapaji cha Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania. Kwa upande wake, Dr. Paolo Ruffini, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Mawasiliano amekazia umuhimu wa kujenga na kudumisha umoja na ushirikiano katika mchakato wa uinjilishaji kwa kutumia vyombo vya mawasiliano ya jamii pamoja na kuhakikisha kwamba, rasilimali watu na vitu vinatumika barabara kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya Kanisa la Kristo. Leo hii kuna changamoto kubwa katika tasnia ya mawasiliano ya jamii na matumizi ya akili bandia sanjari na kuibuka kwa habari za kugushi, yote haya yanahitaji ushuhuda na umakini unaoonesha msimamo na mtazamo wa Kanisa kwa kuzingatia Maandiko Matakatifu pamoja na tunu msingi za Kiinjili, kiutu na kimaadili. Uinjilishaji hauna budi kwenda sanjari na mafundisho makini ya katekesi inayomwilishwa katika maisha ya Liturujia, Maisha ya Sala pamoja na shughuli za kichungaji. Kanisa linapaswa kutangaza na kushuhudia ukweli. Dr. Paolo Ruffini ameangalisha pia uwepo wa ukoloni wa kiitikadi unaoweza kubeba sura ya kielimu, kiuchumi na kisiasa.