Tafuta

Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, TEC., kuanzia Dominika 14 Mei hadi tarehe 21 Mei 2023 linafanya Hija ya Kitume “Ad Limina Apostolorum Visitatio,” kwa kifupi, “Ad Limina” Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, TEC., kuanzia Dominika 14 Mei hadi tarehe 21 Mei 2023 linafanya Hija ya Kitume “Ad Limina Apostolorum Visitatio,” kwa kifupi, “Ad Limina”  

Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania TEC., Laanza Hija ya Kitume Mjini Vatican

Hija ya Kitume ya Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania: Lengo kuu ni: Kukutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu pamoja na kutoa taarifa ya Maandishi kwa Baraza la Kipapa la Maaskofu kuhusu mwenendo mzima wa maisha na utume wa Kanisa katika Jimbo husika. Ni fursa pia ya kujadiliana na wakuu wa Mabaraza ya Kipapa kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya Kanisa la Kristo Yesu kama sehemu ya ujenzi wa Kanisa la Kisinodi. Ni wakati wa sala na tafakari ya kina

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Papa Sixtus wa V kunako mwaka 1585 alianzisha hija za kitume zinazotekelezwa na Maaskofu Jimbo mjini Vatican walau kila baada ya miaka mitano, yaani “Ad Limina Apostolorum Visitatio” na kwa kifupi, “Ad Limina.” Kwa busara yake ya kichungaji akaamuru Maaskofu wote Katoliki kutembelea mjini Vatican walau kila baada ya miaka mitano. Hii ni nafasi ya kutembelea na kusali kwenye Kaburi la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Kukutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu pamoja na kutoa taarifa ya Maandishi kwa Baraza la Kipapa la Maaskofu kuhusu mwenendo mzima wa maisha na utume wa Kanisa katika Jimbo husika. Ni fursa pia ya kujadiliana na wakuu wa Mabaraza ya Kipapa kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya Kanisa la Kristo Yesu kama sehemu ya ujenzi wa Kanisa la Kisinodi. Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican wanasema, katika Kanisa hili la Kristo Yesu, Kuhani Mkuu wa Roma, aliye mwandamizi wa Mtakatifu Petro, ambaye Kristo Yesu alimkabidhi kondoo na wanakondoo wake ili awachunge, kwa agizo la kimungu amepokea mamlaka ya juu kabisa, kamili na yanayojitegemea na ya jumla kwa ajili ya huduma ya roho za watu “Curam animalum.” Hivyo basi, kwa kuwa amewekwa kuwa mchungaji wa waamini wote, ili kukuza manufaa ya wote na ya Kanisa zima na pia ya Makanisa mahalia, anashika mamlaka ya juu ya kawaida juu ya Makanisa yote. Kwa upande mwingine na Maaskofu wamewekwa na Roho Mtakatifu kuwa waandamizi wa Mitume kama wachungaji wa watu, na pamoja na Baba Mtakatifu na chini ya Mamlaka yake, wanao utume wa kudumisha kazi ya Kristo Mchungaji wa milele, kwa sababu Kristo Yesu aliwapa Mitume na waandamizi wao agizo na mamlaka ya kuwafundisha mataifa yote, ya kuwatakatifuza watu katika ukweli na kuwachunga. Rej. Christus dominum, n. 2-3.

Ad Limina Visit: Muda wa kukutana, kuzungumza, kusali na kutafakari
Ad Limina Visit: Muda wa kukutana, kuzungumza, kusali na kutafakari

Ni katika muktadha huu, Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, TEC., kuanzia Dominika 14 Mei hadi tarehe 21 Mei 2023 linafanya Hija ya Kitume “Ad Limina Apostolorum Visitatio,” kwa kifupi, “Ad Limina” inayofanyika kila baada ya miaka mitano. Maaskofu Katoliki Tanzania ambao wamegawanyika katika makundi makuu mawili chini ya uongozi wa Askofu mkuu Gervas John Mwasikwabhila Nyaisonga, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, TEC pamoja na Askofu Flavian Matindi Kassala. Pamoja na kutembelea Mabaraza mbalimbali ya Kipapa, Maaskofu pia wataadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwenye: Kanisa kuu la Bikira Maria Mkuu; Casa San Juan de Avila, Kanisa kuu la Mtakatifu Yohane mwa Lateran, na Kanisa kuu la Mtakatifu Paulo Nje ya Kuta za Roma. Jumatano tarehe 17 Mei 2023 Maaskofu watautembelea Ubalozi wa Tanzania nchini Italia, ili kukutana na kuzungumza na Mheshimiwa Balozi Mahmoud Thabit Kombo pamoja na wafanyakazi Ubalozini hapo.

Maaskofu wanakutana na watanzania tarehe 21 Mei 2023
Maaskofu wanakutana na watanzania tarehe 21 Mei 2023

Ijumaa tarehe 19 Mei 2023 Askofu mkuu Gervas John Mwasikwabhila Nyaisonga ataongoza Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican na baadaye, Maaskofu Katoliki Tanzania watakutana kwa faragha na Baba Mtakatifu Francisko. Jumamosi tarehe 20 Mei 2023, Maaskofu Katoliki Tanzania “watajichimbia kwa faragha” siku nzima ili kufanya tafakari ya kina juu ya hija yao ya kitume mjini Vatican. Tafakari hii itaongozwa na “Opera della Chiesa.” Dominika tarehe 21 Mei 2023 Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania litakutana na kuzungumza na “Umoja wa Watanzania Wakatoliki wanaoishi Italia”, lakini kabla ya mkutano huu, Askofu mkuu Gervas John Mwasikwabhila Nyaisonga ataongoza Ibada ya Misa Takatifu itakayoadhimishwa kwenye Chuo Kikuu cha Kipapa cha Mtakatifu Paulo, majira ya saa 5:00 za Asubuhi kwa saa za Ulaya.

Ad Limina TEC

 

 

14 May 2023, 11:40