Bikira Maria wa Fatima: Ujumbe: Sala, Toba na Wongofu wa Ndani
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Mama Kanisa kila mwaka ifikapo tarehe 13 Mei anaadhimisha kumbukumbu ya Bikira Maria wa Fatima. Hii ni kumbukumbu ya Bikira Maria alipowatokea Watoto watatu wa Fatima: Francis, Yacinta Marto na Lucia dos Santos, tarehe 13 Mei 1917 na kujitambulisha kuwa ni Bikira Maria wa Rozari Takatifu, kwa kuwakabidhi watoto hawa ujumbe wa matumaini kwa binadamu wote, akiwataka wajizatiti katika kupambana na ubaya, kwa kusimama kidete kulinda, kutetea na kushuhudia imani kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Ujumbe wa Bikira Maria kwa Watoto wa Fatima unaweza kufupishwa kwa maneno makuu matatu: Sala, Toba na Wongofu wa ndani! Sala ni majadiliano ya kina kati ya mwamini na Muumba wake; majadiliano yanayomwongoza mwamini kuelekea katika maisha ya uzima wa milele. Waamini wanachangamotishwa na Mama Kanisa kutubu na kumwongokea Mwenyezi Mungu kwa kuwa na mwelekeo mpya katika maisha yao. Bikira Maria wa Fatima anawaalika waamini kuchuchumilia utakatifu na kuendelea kusali kwa ajili ya toba na wongofu wa ndani; kwa kujiweka wakfu kwa Moyo wake usiokuwa na doa! Bikira Maria anawaalika waamini kusali Rozari Takatifu ili kuombea amani duniani! Hii ni cangamoto endelevu hata kwa watu wanaoishi katika ulimwengu mamboleo! Ujumbe wa Bikira Maria kwa Watoto wa Fatima unafumbatwa kwa kiasi kikubwa katika Injili, kiasi kwamba, Fatima inakuwa ni shule ya imani na ushuhuda wa maisha ya Kikristo, na Bikira Maria ndiye Mwalimu wake mkuu! Anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuwa na imani kwa Kristo Yesu na kamwe wasikatishwe tamaa na Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia; majanga katika maisha ya watu; tawala za kifashisti na kikomunisti, tawala ambazo zimedhalilisha haki msingi, utu na heshima ya binadamu; kiasi hata cha kutaka kumng’oa Mungu katika maisha na vipaumbele vya waamini. Kilio cha waamini kilikuwa ni kumwomba Mwenyezi Mungu asimame mwenyewe na kujitetea!
Ujumbe wa Bikira Maria kwa Watoto wa Fatima ulijikita zaidi katika Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia na Vita Kuu ya Pili ya Dunia; vita ambavyo vimesababisha madhara makubwa kwa maisha ya watu sehemu mbalimbali za dunia. Siri zote za Bikira Maria kwa Watoto wa Fatima zikafunuliwa hadharani kunako Mwaka 2000 kwa kuonesha madhara makubwa yaliyosababishwa na Urussi kwa wakati ule kwa kupandikiza “ndago” za Ukanimungu; dhuluma, nyanyaso na mauaji ya kikatili dhidi ya Wakristo! Katika kipindi hiki cha utawala wa giza na chuki dhidi ya imani ya Kikristo, hapa kukaibuka makundi ya Wakristo waliosimama imara kutangaza na kushuhudia imani yao kwa Kristo Yesu, aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu! Jeuri ya maisha yao ya kiroho! Mtakatifu Yohane Paulo II, kunako tarehe 13 Mei 1981 akiwa kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican akapigwa risasi katika jaribio la kutaka kumuua na kumfutilia mbali kutoka katika uso wa dunia! Lakini akasalimika na kwamba, huu ni muujiza wa pekee kabisa aliotendewa na Bikira Maria wa Fatima. Akaamuru hata ile Siri ya Tatu ya Fatima iwekwe hadharani! Ni siri ambayo ilionesha kwamba kulikuwa na mapambano makali dhidi ya Kanisa. Mtakatifu Yohane Paulo II akachukua risasi iliyotoka mwilini mwake na kuiweka kwenye taji ya nyota kumi na mbili zinazopamba kichwa cha Bikira Maria wa Fatima.
Tarehe 25 Machi 1984 Mtakatifu Yohane Paulo II akauweka ulimwengu na kwa namna ya pekee kabisa, Urussi chini ya ulinzi na tunza ya Moyo Safi wa Bikira Maria. Ujumbe wa Bikira Maria kwa Watoto wa Fatima ni endelevu hata kwa watu wa nyakati hizi kwani unafumbatwa katika Injili ya Kristo na Kanisa lake; Unahimiza Ibada kwa Bikira Maria, Toba, Wongofu wa ndani, Utakatifu wa maisha na umuhimu wa kusali Rozari Takatifu ili kuombea amani duniani. Waamini watambue daima kwamba, hata katika shida na mahangaiko yao, Mwenyezi Mungu daima yuko pamoja nao hadi utimilifu wa dahali! Bikira Maria anataka kuwaachia watoto wake, ujumbe wa matumaini, wokovu, amani na kwamba, Mwenyezi Mungu apewe kipaumbele cha kwanza katika maisha ya mwanadamu! Ni katika muktadha wa Maadhimisho ya kumbukumbu ya Bikira Maria wa Fatima, Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican ameshiriki katika mkesha, maadhimisho ya kumbukukumbu na hatimaye, Dominika, tarehe 14 Mei 2023 akaadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kanisa “Parque das Nações” Jimbo kuu la Lisbon, nchini Ureno na kama sehemu ya maandalizi ya Maadhimisho ya Siku ya Vijana Ulimwenguni itakayoanza kutimua vumbi kuanzia tarehe 1 hadi 6 Agosti 2023 kwa kunogeshwa na kauli mbiu “Akaondoka kwa haraka” Lk 1:39. Mkazo ni vijana kuendelea kujiandaa kikamilifu kwa sala, kazi, majitoleo yao, kwani vijana ni jeuri ya Kanisa na kwa njia ya furaha na shauku yao, wanalipatia Kanisa nguvu mpya!
Liturujia ya Neno la Mungu Dominika ya Sita ya Kipindi cha Pasaka Mwaka A wa Kanisa inamzungumzia Roho Mtakatifu, ambaye Kristo Yesu anamwita “Msaidizi,” kadiri ya maana ya neno “Yule ambaye anaitwa awe jirani,” Wakili (Advocatus) na Mfariji, Kristo Yesu akiwa ndiye Mfariji wa kwanza. Bwana Mwenyewe anamwita Roho Mtakatifu kuwa ni Roho wa kweli. Rej. KKK. 692. Kuna umuhimu wa kutekeleza Amri za Mungu katika maisha kama kielelezo cha upendo wa kweli. Maandalizi ya Maadhimisho ya Siku za Vijana Ulimwengu ni magumu na yana changamoto zake, lakini Mwenyezi Mungu anapenda kuwahakikishia waja wake, uwepo wake wa daima na kwa msaada wa daima wa Roho wa kweli. Maadhimisho ya Siku ya Vijana Ulimwenguni ni tukio kubwa la sherehe inayowakutanisha vijana kutoka sehemu mbalimbali za dunia, ni siku ya kutangaza bna kushuhudia imani, matumaini na mapendo kwa Kristo Yesu na Kanisa lake “Mwe tayari siku zote kumjibu kila mtu awaulizaye habari za tumaini lililo ndani yenu; lakini kwa upole na kwa hofu.” 1 Pet 3:15. Ni ushuhuda kwa Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu ili kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti, ili hatimaye, aweze kuwaongoza watu kwa Mungu Baba. Vijana wengi wanakabiliwa na changamoto ya utupu katika maisha yao, huu ni mwaliko wa kuwakaribisha vijana kusafiri, pamoja na maswali na mahangaiko yao, ili waweze kupanua tumaini walilopewa na Kristo Yesu anayeishi ndani ya nyoyo zao! Huu ni mwalilo wa kuendelea kujiinjilisha na kuwainjilisha vijana, ili kupata furaha ya kweli kwa uwepo wa Roho Mtakatifu ndani mwao! Huu ni mwaliko kwa kukuza na kudumisha mawasiliano, ushirikianano na ukarimu. Ni matumaini ya Mama Kanisa kwamba, Maadhimisho ya Siku ya Vijana Ulimwenguni kwa Mwaka 2023 yatakuwa ni chemchemi ya matumaini kwa vijana wengi, watakaofika kutafuta maana halisi ya maisha, huku wakiyaelekeza matarajio yao kwa Mwenyezi Mungu. Vijana hawana budi kujizatiti barabara katika maisha na kamwe wasikate wala kukatishwa tamaa.