Kuanzia 11-16 Mei utafanyika mkutano Mkuu wa Caritas Internationalis
Na Angella Rwezaula, - Vatican.
Mkutano Mkuu wa 22 wa Caritas Internationalis utafanyika mjini Roma kuanzia tarehe 11 hadi 16 Mei 2023 kwa ushiriki wa takriban wajumbe 400 wanaowakilisha mashirika 162 ya Caritas yanayofanya kazi katika nchi na maeneo 200 duniani kote. Mkutano Mkuu wa Caritas Internationalis hufanyika kila baada ya miaka minne, pia kuchagua Rais, Katibu Mkuu, Mweka Hazina, Halmashauri Kuu na Baraza la Wawakilishi la Shirikisho. Wakati wa Mkutano Mkuu wa 2023 ambao mada yake, itaongozwa na “Kujenga njia mpya za udugu”, imechochewa na Waraka wa Fratelli Tutti kwa viongozi ambao wataongoza Shirikisho la Caritas kwa miaka minne ijayo, hadi 2027, watachaguliwa. Wakati wa hafla hiyo, wajumbe wa Caritas pia watatafakari jinsi mashirika ya Caritas yanaweza kufanya kazi pamoja kwa ufanisi zaidi katika kuwahudumia maskini zaidi na walio hatarini zaidi katika ulimwengu ulioathiriwa na majanga mengi: kutoka kwa vita vya Ukraine hadi janga la COVID-19, kutoka kwa athari za mabadiliko ya tabianchi na kukithiri kwa uhaba wa chakula.
Kwa mujibu wa taarifa za waandaaji , Mkutano huo pia utazinduliwa tarehe 11 Mei na mkutano wa faragha pamoja na Papa Francisko. Asubuhi ya tarehe 12 Mei 2023 kutakuwa na tafakari ya “Changamoto za Ulimwenguni na jukumu la Caritas”, na hotuba za: Askofu Mkuu Paul Richard Gallagher, Katibu wa Vatican wa Mahusiano na Mataifa na Mashirika ya Kimataifa ya Balozi Gabriel Ferrero y de Loma-Osorio, Rais wa Kamati ya Usalama wa Chakula Duniani, na wawakilishi wa Caritas kutoka Ghana, Myanmar na Ireland. Katika siku zitakazofuata, vikao vingine vya mada vitafanyika ambavyo vitazingatia mada tatu muhimu za Shirikisho: sinodi, uundaji wa kikanda na ushirikiano wa kidugu. Vikao hivyo vitajumuisha hotuba za wawakilishi wa Caritas kutoka sehemu mbalimbali za dunia na wageni wa nje, akiwemo Kardinali Mario Grech, Katibu Mkuu wa Sekretarieti Kuu ya Sinodi, na Sista Alessandra Smerilli, Katibu wa Baraza la Kipapa la kuhamaisha huduma ya Maendeleo Fungamani ya Binadamu.