Maaskofu Tanzania wako Roma kati hija ya kitume.Hija hii ina historia ndefu!
Na Angella Rwezaula, - Vatican.
Baraza la Maakofu Katoliki nchini Tanzania (TEC) wako katika Hija ya Kitume mjini Vatican kuanzia tarehe 14-21 Mei 2023. Kiutamaduni hija za kitume zimekuwa zikitekelezwa na Maaskofu wa majimbo kutoka pande za dunia mjini Vatican angalau kila baada ya miaka mitano, japokuwa kwa miaka mitatu iliyopita, iliingiliwa na janga baya ya Uviko,ambalo halikuruhusu miaka hiyo kufanya hija hizi, hadi tulipoondokana na balaa hilo.
Hija hiyo kwa kilatino inatwa “Ad Limina Apostolorum Visitatio” ambapo katika siku hizi watakutana pia na Baba Mtakatifu Francisko. Kwa kawaida hija hiyo za kitume ni mara baada ya kuzungukia mabaraza ya kipapa hukutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu pamoja na kutoa taarifa ya Maandishi kwa Baraza la Kipapa la Maaskofu kuhusu mwenendo mzima wa maisha na utume wa Kanisa katika majimbo husika. Vile vile ni fursa nzuri kwa maaskofu hao kutembelea Mabaraza ya Kipapa yalipo mjini Vatican ili kufahamu kazi zao wanazojikita nazo kwa karibu, na kutokana na kwamba maaskofu mahalia ndiyo Injini ya Kanisa la Ulimwengu ni vema wakajua mabaraza haya wanayoshirikiana nayo kwa karibu. Kwa hiyo kwa siku hizi za hija yao zitaongozwa kwanza kabisa na maadhimisho ya Misa Takatifu kila siku.
Kwa hiyo Jumatatu asubuhi saa 2.30 Tarehe 15 Mei, Askofu Mkuu Paul Ruzoka wakati wa Ibada ya Misa, takatifu, amemkabidhi Mama Maria, hija yao ya kichungaji, akimwomba Mama Maria awasindikize. Waliudhuria pia baadhi ya wawakilishi wa Jumuiya ya Watazania, japokuwa ni siku ya masomo lakini wamejitahidi kuwapo na kuongoza nyimbo. Hata hivyo kulikuwa na mgeni anayefanya hija yake katika nchi Takatifu, Bwana Venance Salvatory Mabeyo, aliyekuwa Mkuu wa majeshi Tanzania, na ambaye amesoma somo la kwanza na zaburi. Kwa hakika ulikuwa ni wakati mzuri wa kushiriki karamu ya Bwana wetu Yesu Kristo, katika Kikanisa hicho cha Picha ya Bikira Maria Afya ya Warumi, ambacho ni pendwa sana kwa Baba Mtakatifu Francisko.
Historia ya hija hii (ad limina visita) inakaziwa katika barua ya Mtakatifu Paulo kwa Wagalatia: “Baadaye, baada ya miaka mitatu, nilikwenda Yerusalemu ili kushauriana na Kefa, na nikakaa kwake siku kumi na tano” (Gal 1:18) Wakati wa ziara hii, Paulo aliweza kueleza kwa Petro na Yakobo matatizo yaliyopatikana katika uinjilishaji katika baadhi ya maeneo ya Yudea. Huu unaweza kuchukuliwa kuwa mkutano wa kwanza wa kusaidiana na majadiliano juu ya masuala fulani. Kuhusu usemi ad limina apostolorum, ulianzia karne za kwanza za historia ya Kanisa; kiukweli, katika lugha ya kisheria, pamoja na limina apostolorum inasikika tayari katika karne za kwanza kwani lugha ya kikanoni ilikuwa inaelekeza makaburi ya mitume Petro na Paulo, kwa hiyo hija hizi zilitimizwa na waamini ambao walikuwa na lengo lile lile la kufika katika makaburi. Neno hilohilo lilionesha ziara ambayo maaskofu wote waliopaswa kufanya huko Roma, kulingana na kile kilichoanzishwa katika Mtaguso wa Roma, mnamo mwaka wa 745, chini ya Papa Zakaria.
Kwa karne nyingi desturi hiyo ilidhoofika, ikapata nguvu tena mnamo 1585 tu, chini ya Papa Sixtus V ambaye, pamoja na katiba Romanus Pontifex ya tarehe 20 Desemba, alirejesha wajibu wa ziara hizo, akizifanya kila baada ya miaka mitatu; “ziara hiti ” zilithibitishwa baadaye na Papa Benedikto XIV kwa katiba Quod sancta ya tarehe 23 Novemba 1740. Haya yote yalifanyika katika muktadha wa uimarishaji wa upapa katika udhibiti wa kazi ya kiaskofu katika kipindi cha mageuzi.
Na mnamo tarehe 31 Desemba 1909, kwa tamko la Mkutano wa Makaridinali(Consistorial A remotissima), zunguko wa ziara ya ad limina apostolorum visita uliwekwa hadi miaka 5 na (10 kwa Jumuiya za mashirika yasiyo ya Ulaya), na ilianzishwa kuwa sio tu maaskofu wa majimbo lakini pia wenye majukumu yanayolingana nayo kwa hiyo (maasisi wa majimbo na abati, wasimamizi wa majimbo na wawakilishi wa kitume). Kunako mwaka 1975, Baraza la Kipapa la Maaskofu lilipanga tena “ziara kwa Tamko la Ad Romanam Ecclesiam, la tarehe 29 Juni, kugawanya maeneo kwa miaka mitano, mitano.
Katika Kanuni ya Sheria ya Kanisa ya 1983, hija ya ad limina apostolorum zimeagizwa na kanoni mbili kifu cha (399 na 400) kuwa: “Kila baada ya miaka mitano Askofu wa jimbo anatakiwa kuwasilisha ripoti kwa Baba Mtakatifu kuhusu hali ya Jimbo alilokabidhiwa, na kulingana na umbo na wakati uliowekwa na Makao Makuu Vatican(...)Askofu wa jimbo katika mwaka anaotakiwa kuwasilisha taarifa hiyo kwa Baba Mtakatifu,isipokuwa kama imethibitishwa vinginevyo na Makao Makuu ya Kitume, aweze kwenda mjini kufanya hija katika makaburi ya wenyeheri Mitume Petro na Paulo na kujiwasilisha kwa Papa wa Kirumi.
Kwa hiyo ikumbukwe Tanzania ina majimbo Makuu saba: Jimbo Kuu la Dar Es Salam, Tabora, Songea, Dodoma, Mbeya, Mwanza na Arusha na majimbo mengine ya kawaida. Kama ratiba ilivyopangwa, Jumatatu tarehe 15 Mei 2023, Maaskofu wa Tanzania wameudhuria Misa Takatifu katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Maria Mkuu, kwenye kikanisa cha Bikira Maria, Afya ya Waroma (Salus Populi Romani). Baada ya hapo waliendelea na ratiba yao kwa kuongozwa na Katibu wa Baraza la Maaskofu Tanzania, Padre Charles Kitima, Katibu Msaidizi Padre Cesco Msaga, (CPPS).
Wafahamu maaskofu wa Tanzania (TEC)
Kwa ufahamu zaidi, Maaskofu wa Tanzania ni: Askofu Mkuu Gervaz Nyaisonga(Mbyeya), Askofu Askofu Mkuu Isaac Amani (Arusha), Askofu Mkuu Jude Thaddeus Ruwa’ichi (Dare Es Salaam), Askofu Mkuu Renatus Nkwande (Mwanza, Askofu Mkuu Dallu (Songea), Askofu Antony Lagwen (Mbulu), Askofu Augustin Shao (Zanzibar), Askofu Eusebius Nzigilwa (Mpanda), Askofu Bernadin Mfumbusa (Kondoa), Askofu Joseph Mlola Kigoma, Askofu Filbert Mhasi (Tunduru–Masasi), Askofu Michael Nsonganzila (Musoma), Askofu Tarsisius Ngalalekumtwa(Iringa), Askofu Rogath Kimaryo (Same), Askofu Almachius Rweyongeza (Kayanga), Askofu Wolfagang Pisa, O.F.M. Cap. (Lindi), Askofu Agapitus Ndorobo (Mahenge), Askofu Salutaris Libena (Ifakara), Askofu Flavian Kassala(Geita), Askofu Mkuu Beatus Kinyaiya (Dodoma).
Askofu Mkuu Paul Ruzoka (Tabora), Askofu Simon Masondole (Bunda); Askofu Edward Mapunda (Singida), Askofu Stephano Musomba, O.S.A (Msaidizi wa Jimbo Kuu Dar Es Salaam), Askofu Titus Mdoe (Mtwara), Askofu Methodius Kilaini (Msimamizi wa Jimbo la Bukoba), Askofu Beatus Urassa (Sumbawanga), Askofu Lazarus Msimbe, S.D.S (Morogoro), Askofu Ludovick Minde, ALCP/OSS (Moshi), Askofu Prosper Lyimo (Askofu Msaizidi Arusha), Askofu Liberatus Sangu (Shinyanga), Askofu John Ndimbo (Mbinga), Askofu Henry Mchamungu (Askofu Msaidizi Dar Es Salaam), Askofu Severine NiweMugizi (Rulenge-Ngara), Askofu Christopher Ndizeye(Kahama), Mheshimiwa Padre Thomas Kiangio, msimamizi wa kitume wa Jimbo la Tanga.