Askofu mkuu Mauricio Rueda Beltz, Balozi wa Vatican Pwani ya Pembe
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Baba Mtakatifu Francisko amemteuwa Askofu mkuu Mauricio Rueda Beltz, kuwa Balozi mpya wa Vatican nchini Pwani ya Pembe. Hayo yamesemwa na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican kwa wafanyakazi wa Sekretarieti kuu ya Vatican tarehe 16 Juni 2023. Kabla ya uteuzi huu, Askofu mkuu Mauricio Rueda Beltz alikuwa ni Katibu mkuu msaidizi wa Mambo ya Nchi za Nje, Ushirikiano na Mashirika ya Kimataifa. Itakumbukwa kwamba, Askofu mkuu Mauricio Rueda Beltz, alizaliwa tarehe 8 Januari 1970 Jimbo kuu la Bogotà, nchini Colombia. Baada ya masomo na majiundo yake ya Kikasisi, tarehe 19 Desemba 1996 akapewa Daraja takatifu ya Upadre kwa ajili ya Jimbo kuu la Bogotà nchini Colombia.
Tarehe 1 Julai 2004 akaanza utume wake wa kidiplomasia mjini Vatican na kubahatika kupelekwa nchini Guinea, Chile, Marekani na Yordani. Baadaye alihamishiwa mjini Vatican kwenye Sekretarieti kuu ya Vatican, kitengo cha Mambo ya Nchi za Nje, Ushirikiano na Mashirika ya Kimataifa na hatimaye tarehe 17 Desemba 2020 akateuliwa na Baba Mtakatifu Francisko kuwa Katibu mkuu msaidizi Mambo ya Nchi za Nje, Ushirikiano na Mashirika ya Kimataifa kama Mratibu maalum wa Hija za Kitume za Baba Mtakatifu. Tarehe 16 Juni 2023 akateuliwa na Baba Mtakatifu Francisko kuwa Balozi mpya wa Vatican nchini Pwani ya Pembe.