Thomas John Kiangio Askofu Jimbo Katoliki la Tanga! Kumenoga!
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Baba Mtakatifu Francisko amemteuwa Mheshimiwa sana Padre Thomas John Kiangio, Msimamizi wa Kitume wa Jimbo Katoliki la Tanga, kuwa Askofu mpya wa Jimbo Katoliki la Tanga. Askofu mteule Thomas John Kiangio wa Jimbo Katoliki la Tanga alizaliwa tarehe 17 Machi 1965 huko Mazinde Ngua, Jimbo Katoliki la Tanga. Alipata malezi na majiundo yake ya Kipadre kutoka Seminari kuu ya Mtakatifu Antony, Ntungamano Jimbo Katoliki la Bukoba na Karol Lwanga, Segerea Jimbo Kuu la Dar es Salaam. Mazoezi ya Mwaka wa kichungaji aliyafanyia Parokia ya Mlingano, Jimbo Katoliki la Tanga, akashiriki kwa mwaka mmoja kozi ya Shughuli za kichungaji, Hospitali ya Rufaa ya Kanda Bugando Mkoani Mwanza. Na ilipotimia tarehe 16 Julai 1997 akapewa Daraja Takatifu ya Upadre kwa ajili ya Jimbo Katoliki la Tanga.
Tangu wakati huo, amebahatika kutekeleza utume wake kama Paroko-usu, Parokia ya Lushoto kati yam waka 1997-1998. Baadaye akateuliwa kuwa ni mlezi, mwalimu na Gambera Msaidizi na hatimaye Gambera wa Seminari Ndogo ya Mtakatifu Yosefu Soni, Tanga kati ya mwaka 1998-1999 na kati ya mwaka 2004 hadi mwaka 2013. Baadaye kati ya mwaka 1999 hadi mwaka 2003 alitumwa kuendelea na masomo ya juu Chuo kikuu cha Kipapa cha Urbaniana, kilichoko mjini Roma. Baadaye kati ya mwaka 2013 hadi mwaka 2020 aliteuliwa kuwa Katibu wa Jimbo na kati ya mwaka 2020 hadi kuteuliwa kwake aliteuliwa kuwa Msimamizi wa Kitume wa Jimbo Katoliki la Tanga kufuatia kifo cha Askofu Anthony Mathias Banzi aliyefariki dunia tarehe 20 Desemba 2020.